10-14-2022, 09:12 PM
NINAMUENZI MWALIMU NYERERE KWA KULIA NA MTANZIKO WA LUGHA NCHINI TANZANIA
Uzoefu na Tajiriba ya Mwandishi
*1.0 UTANGULIZI*
Ninayeandika makala hii ni Mwalimu na Mtafiti wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Kwa hiyo, sauti yangu katika uga huu wa lugha (ya Kiswahili na Kiingereza) inaweza ikawa na uzito mkubwa kuliko sauti yangu katika nyuga nyingine za kitaaluma. Msingi wa uchambuzi wa makala yangu umejikita katika uzoefu na tajiriba katika lugha hizi mbili. Ijapokuwa hoja nyingi katika makala hii hazijashadidiwa kwa kurejelea tafiti au maandiko mbalimbali, ninaomba uamini kwamba ni uchambuzi wa mambo wenye ukweli. Lengo langu ni kuwa na makala rahisi fupi isiyochosha kusomwa.
Mwalimu Nyerere ndiye anaweza kutajwa kuwa msingi wa kukifikisha Kiswahili leo hii kilipo. Nyerere alitumia njia nyingi sana za kukikuza, kukieneza na kukiendeleza Kiswahili ikiwemo kukipa hadhi kubwa ya kimatumizi nchini Tanzania. Kiswahili kimekuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi nyingi za Serikali na baadhi ya shule Binafsi huku Kiingereza kikifundishwa kama somo.
Kiingereza, kama tunavyojua, ni lugha iliyotufikia kwa njia ya ukoloni (Waingereza). Ni lugha ambayo ina nafasi kubwa sana kidunia; hii ni lugha ya kufundishia katika ngazi ya elimu ya sekondari na chuo kikuu nchini mwetu ambapo katika ngazi hizo, Kiswahili kinafundishwa au kumakinikiwa kama somo.
*2.0 UFANISI WA LUGHA ZA KUFUNDISHIA*
_2.1 Elimu katika Shule za Msingi_
Katika ngazi ya shule za msingi ambako Kiswahili ni lugha ya kufundishia, ufanisi wa matumizi ya lugha hiyo ni mkubwa kwa maana walimu wanaweza kuitumia lugha hiyo vema kuwafundisha wanafunzi, na wanafunzi wanaweza kuwasikiliza vema walimu wao. Kwa ujumla, majadiliano baina ya walimu na wanafunzi hufanyika vema bila shida yoyote.
Aidha, shule nyingi za msingi (idadi kubwa ikiwa shule za binafsi) zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, nazo zimekuwa zikifanya vema pia katika kutumia lugha ya Kiingereza katika masuala mbalimbali ya kishule.
_1.2 Elimu katika Sekondari na Vyuo Vikuu_
Ufanisi wa matumizi ya lugha ya kufundishia ambayo ni Kiingereza katika ngazi za elimu tajwa si mzuri hata kidogo. Wanafunzi wengi wameripotiwa na tafiti mbalimbali kuwa hawawezi kufuatilia, kujadili na kujielezea kwa lugha ya Kiingereza. Cha kushangaza, tafiti zimebaini kwamba hata baadhi ya walimu hawana uwezo wa kufundisha na kufanya majadiliano na wanafunzi kwa kutumia Kiingereza muda wote. Kinachotokea ni kwamba walimu wamepitisha utaratibu wa kuchanganya msimbo, yaani wanatumia Kiingereza na Kiswahili wanapofundisha na kujadiliana na wanafunzi wao darasani, ofisini au katika vyumba semina (kwa vyuo vikuu).
*2.0 MTANZIKO WA LUGHA NCHINI TANZANIA*
Kama ambavyo umeona hali halisi katika kipengele cha kwanza hususani 1.1 na 1.2 kinavyoeleza hali ya ufanisi wa lugha za kufundishia nchini Tanzania. Kwa ujumla, ufanisi wa lugha ya kufundishia upo katika ngazi ya elimu ya msingi tu. Hapo ndipo mtanziko wa lugha unapoanzia. Mtanziko huu wa lugha upo kwa mapana yake; ambapo unaweza kujidhihirisha katika aina tatu: mtanziko wa lugha ya kufundishia; mtanziko wa lugha ya mawasiliano katika taasisi, asasi na vyama vya kitaaluma; na mtanziko wa matumizi ya lugha rasmi.
_2.1 Mtanziko wa Lugha ya Kufundishia_
Kama ambavyo imeelezwa vema katika 1.2; ijapokuwa sera ya lugha imebainisha wazi kwamba shule za sekondari na vyuo vikuu vitumie Kiingereza kama lugha ya kufundishia, walimu na wanafunzi wanachanganya karibia nusu kwa nusu Kiingereza na Kiswahili katika majadiliano kwa njia ya mazungumzo ya mdomo katika mada mbalimbali. Hii hali imeshamiri na inazidi kuota mizizi sekondarini na vyuoni. Na tusipochukua hatua za makusudi, Tanzania litakuwa Taifa la kwanza linalotumia mfumo wa peke yake wa matumizi ya lugha ya kufundishia ambao ni kuchanganya msimbo ( _code-switching/code-mixing_ ).
_2.2 Mtanziko wa Lugha ya Mawasiliano katika Taasisi, Asasi na Vyama vya Kitaaluma_
Taasisi, asasi, na vyama mbalimbali vya kitaaluma vimekuwa katika mtanziko mkubwa wa matumizi ya lugha. Nyaraka nyingi katika taasisi hizi huandikwa kwa Kiingereza lakini majadiliano hufanywa kwa Kiswahili au kwa kuchanganya Kiswahili na Kiingereza.
Hata vyuo vikuu na vyama vya kitaaluma, ambako watu wanategemea mtanziko huu usiwepo, nako bado vikao mbalimbali na mawasiliano ya kiofisi ambayo yameagizwa kisera/kiutaratibu yafanyike kwa Kiingereza, vinafanywa kwa kuchanganya msimbo. Mathalani, kikao kinaweza kufunguliwa kwa lugha muafaka (Kiingereza) kwa dakika kadhaa kisha lugha inabadilika na kuwa ama Kiswahili au kuchanganya msimbo, kwa maana ya kutumia Kiswahili na Kiingereza kwa wakati mmoja. Cha kushangaza zaidi, hata katika makongamano na midahalo iliyoandaliwa na wanataaluma na kujadiliana miongoni mwao, nyaraka huandikwa kwa Kiingereza lakini majadiliano kwa mazungumzo ya mdomo hufanyika ama kwa Kiswahili au kuchanganya msimbo (Kiswahili na Kiingereza). Hapo sasa unajiuliza: wanataaluma hawa hawajui Kiingereza?
_2.3 Mtanziko wa Matumizi ya Lugha Rasmi/Sanifu_
Hii ni aina nyingine ya mtanziko ambapo Watanzania wengi hawana weledi wa lugha hizi mbili (Kiswahili na/au Kiingereza) wanazotumia. Licha ya wengi wao kufuzu au kumaliza elimu ya sekondari na/au vyuo vikuu ambako walijifunza na/au kufundishwa (kwa) lugha hizi mbili vema, hawana weledi wa matumizi ya lugha hizo katika misingi yake ya urasmi na usanifu. Wengi wao wanabanga tu lugha hizo pale wanapotakiwa kuzitumia kwa kufuata misingi yake sanifu na rasmi. Mtanziko huu umekithiri pia katika vyombo vya habari. Hali ni tete! Ina maana kwamba Watanzania wengi hawakijui Kiswahili sanifu/rasmi wala Kiingereza sanifu (standard British English). Ushahidi wa haya mambo upo wazi kabisa.
Kwa ujumla, jambo ambalo nimelibaini ni kwamba kadiri muda unavyozidi kwenda mbele, weledi wa matumizi ya lugha (na hata katika masuala mengine mengi) miongoni mwetu unapungua kwa kasi sana. Ninafikiri upo ulazima wa kufanya utafiti ili kujua sababu ya jambo hili.
*3.0 SABABU ZA MTANZIKO WA LUGHA*
Sababu za mtanziko huu ni:
(a) Kukosekana kwa muumano wa lugha ya kufundishia kati ya ngazi moja na nyingine ya elimu. Suala la kutumia Kiswahili katika ngazi ya shule ya msingi kisha kutumia Kiingereza katika sekondari na vyuo, linamvuruga mwanafunzi kwa kiasi kikubwa sana. Ikumbukwe kwamba binadamu huamilia lugha ( _a person acquires language_ ) pasi kutumia nguvu akiwa mdogo sana, na akishakuwa mkubwa, uwezo wa kuamilia unakufa na kuhamia katika kujifunza lugha ( _to learn language_ ) na hapo sasa nguvu kubwa hutumika. Kwa hiyo, wakati mwanafunzi huyu ni mtoto mdogo akiwa shule ya msingi anatumia lugha X (Kiswahili) ambapo lugha hiyo inakuwa imeshaota mizizi kichwani mwake; akishakua anajiunga na sekondari, anakutana na lugha X (Kiingereza), inakuwa ni vigumu sana kuingiza misingi mipya ya lugha akilini mwake. Matokeo yake, anabakia na mtanziko wa lugha katika msingi kwamba anakosa fursa ya kuimarisha lugha iliyoota mizizi kichwani mwake na analazimika kuingiza lugha mpya katika kichwa ambacho kinatakiwa sasa kitumie nguvu nyingi kuipokea lugha hiyo na kujiimarisha nayo. Matokeo yake ni kwamba mwanafunzi anakuwa na kazi mbili: kwanza, kujifunza lugha ngeni ambayo haijaimarika kichwani mwake, na pili, kujifunza maarifa husika. Je, unadhani mwanfunzi huyu anaweza kujenga maarifa muafaka pamoja na fikra tunduizi kichani mwake?
(b) Baadhi ya walimu (wa masomo ya lugha na wa masomo mengine) kutokuwa weledi. Ualimu unachukuliwa kama fani ya watu wenye ufaulu duni (wa chini);
© Kukosekana kwa mbinu changamani nzuri za kufundisha na kujifunza somo la Kiingereza; mfano, kukosekana kwa midahalo (debates), kukosekana kwa mashindano ya usomaji wa hadithi na vitabu vya Kiingereza, kukosekana kwa mashindano mbalimbali ya uandishi kwa lugha ya Kiingereza, n.k. ;
(d) Kukosekana kwa usimamizi madhubuti wa matumizi ya lugha yaliyopitishwa kisheria/kisera katika ngazi fulani ya elimu, taasisi, au katika muktadha fulani; na
(e) Mazingira magumu na maslahi duni kwa walimu hasa wa sekondari na shule za msingi.
*4.0 NINI KIFANYIKE KUONDOKANA NA MTANZIKO WA LUGHA?*
Jibu ni rahisi: kutatua changamoto na matatizo yaliyobainishwa katika sehemu ya 3.0
*5.0 HITIMISHO*
Licha ya kwamba ni kweli ili kuondokana na mtanziko huu wa lugha nchini Tanzania, kwa kiasi kikubwa tunategemea mchakato usimamiwe na Serikali; bado mtu binafsi au taasisi inaweza kuwa na mikakati ya kupunguza au kuondokana na kiwango fulani cha mtanziko wa lugha. Kwa hiyo, ninatoa wito kwa watu wote hususani waliobahatika kusoma elimu ya sekondari na/au chuo wafanye jitihada za makusudi za kujikwamua katika mtanziko huu. Yafuatayo ni mambo unayoweza kuyafanya au kuyazingatia ili kuondokana na mtanziko wa lugha:
(a) Kujifunza au kujiimarisha katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili; jipige msasa katika sarufi ya lugha hizo, kama una shida ya kuongea Kiingereza vema; jenga utamaduni wa kusikiliza sana Kiingereza, kusoma & kuandika sana habari za Kiingereza, na kujenga mazoea ya kuongea Kiingereza; na
(b) Jenga nidhamu ya kuheshimu lugha iliyopitishwa kutumika katika miktadha fulani; kama ni Kiingereza, tumia Kiingereza, kama ni Kiswahili, tumia Kiswahili; achana na habari za kuchanganya msimbo bila ulazima wowote.
*Dkt. Issaya Lupogo*
Chuo Kikuu Mzumbe
lupogoissaya1@gmail.com
0712-143909
_#TumuenziBabaWaTaifaKwaKuitumikiaNchiYetuVema#_
14/10/2022

Mwl Maeda