Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
SHAIRI: HANI NIPO KITANDANI
#1
HANI NIPO KITANDANI
haloo!hanii halo, Rwaka hani wasikia?
Ndio hapo sawa halo, vipi unaendelea?
Tatizo nililonalo, lazizi ninaugua,
Hani nipo kitandani, taabani hali yangu.

Wala sijahama njia, nitafika huko Rwanda,
Ikinijia afia, na wangu mwili kuwanda,
Basi huko nitatua, unione mie kinda,
Sasa nipo kitandani, taabani hali yangu.

Ila ninayo pumzi, bado moyo unahema,
Bora nikweleze wazi, kinifanyacho kukwama,
Matatizo ya uzazi, ndiyo yaloniandama,
Jua nipo kitandani, taabani hali yangu.

Ina machungu dunia, na mie yamenikuta,
Nusu niage dunia, kwa tumbo kunikeketa,
Japo nimeamkia, bado najivutavuta,
Ila nipo kitandani, taabani hali yangu.

Maradhi yanaghasia, Karagama sikiliza,
Yakishakuangukia, dira unaipoteza,
Mwilini nimelegea, vile nimepata siza,
Love nipo kitandani, taabani hali yangu.

Nitahama nikipona, Tanzania sitarudi,
Na wewe tukionana, itatulia fuadi,
Ila sasa raha sina, Darling I feel bad,
Vile nipo kitandani, taabani hali yangu.

Namshukuru Karima, ningali hai mpenzi,
Ninaungoja uzima, japo kutwa nakuenzi,
Ningelikufa mapema, ungelipata simanzi,
Hapa nipo kitandani, taabani hali yangu.

Na mie napata ganzi, nikikukosa kijana,
Heri kunipiga konzi, utosini nitapona,
Sitahimili majonzi, na wewe tukikosana,
Japo nipo kitandani, taabani hali yangu.

Maumivu yamezidi, yanikataza kutunga,
Kuacha imenibidi, utungo huu kufunga,
Ila ninakuahidi, huko Rwanda nitatinga,
Nikitoka kitandani, iwe njema hali yangu.

Mtunzi Filieda Sanga
Mama B
Mabibo Dsm
0753738704
Mwl Maeda
Reply


Messages In This Thread
SHAIRI: HANI NIPO KITANDANI - by MwlMaeda - 07-30-2022, 02:16 PM

Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)