Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
"MEMORY OF DEPARTURE " ya ABDULRAZAK GURNAH
#1
"MEMORY OF DEPARTURE " ya ABDULRAZAK GURNAH.
Nimemaliza kusoma Riwaya ya Kitawasifu ya  AbdulRazak Gurnah Mshindi wa Tuzo ya Nobel katika Fasihi 2021 inayoitwa  "Memory of Departure".

Wakati wengine wakiendelea na mijadala yao ya ima yeye ni Mtanzania au Mwingereza,mimi nikaona nijikite kutazama yaliyompa hedaya duniani kote.Makubwa na machache niliyoyabaini ni yafuatayo katika Falsafa yake:

1.Nimeishuhudia nguvu kubwa ya Utamaduni katika kujenga aina ya kizazi tutachokitaka ama Utamaduni unavyoweza kuifuta jamii moja au hata Taifa moja na likabaki historia tu katika ndimi za watu.

2.Nimeshuhudia kuanzia mwanzo mpaka mwisho nguvu kubwa ya mama.Kwa namna mama anavyoweza kumfinyanga mwana na akawa vile atakavyo.Mama anavyoweza kuilinda familia.Mama anavyoweza kuifariji familia.

3.Nimeshuhudia kuwa AbdulRazak kifalsafa ni Mmajumui wa Afrika na haya hana katika hilo.Wanaobishana wabishane lakini yeye anaililia Afrika.

4.Nimeishuhudia safari inayoakisi kama yakwake.Laiti angalipata "Scholarships" za Serikali ambazo zilikuwa zinatolewa kwa upendeleo kipindi hiko,katu asingaliondoka Zanzibar kama mkimbizi.Mitihani alifaulu vizuri,alikuwa na malengo ya kusoma nje kama alivyomshawishi Mwalimu wake wa Kiingereza,alifanya harakati za kupata "passport" n.k.

5.Nimeishuhudia namna uchungu nao unavyoweza kumsukuma mtu katika maendeleo.Kwasababu kwa maoni yangu ukiniuliza hasa kilichomkimbiza AbdulRazak Zanzibar nitakwambia ni matendo ya kiutamaduni,kwa maana tabia za watu binafsi wachache,hali ya maisha ya kifamilia (umasikini) kuliko hata hizo vuguvugu za kisiasa zinazotajwa kwamba labda ni hofu ya kuuawa ama vinginevyo.

6.Nimeona jitihada na athari ya kukitambulisha Kiswahili kwa maneno tele ambayo angalitaka angaliyapata tu katika lugha ya Kiingereza.Utaona humo maneno kama:
a)Voti mpeni Jongo.
b)Mbatata
c)Mzambarau.
d)Rizki.
e)Buibui.
f)Khitma.
g)Muadhin.n.k.

Kwa hakika,ninaweza kusema kuwa, kwa uandishi wake na kwa namna nilivyowahi kuwaona waandishi wengine wa Kiswahili,laiti ingalikuwa kazi zetu za Kiswahili za waandishi wetu nguli hapa Tanzania hutafsiriwa katika lugha za kimataifa kama Kiingereza, basi huenda tuzo zenyewe za Nobel zingelikuwa zinatiririkia hapa kwetu tu na hivi sasa ingelikuwa tumeshazizoea huku tukiwashuhudia wenzetu wa nchi jirani zinazotuzunguka wakizimezea mate.Wasalam!.

Mudhihiri Njonjolo.
Lindi.

+255 620 207 336
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)