SHAIRI: KUSANYENI KAZI ZANGU - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: KUSANYENI KAZI ZANGU (/showthread.php?tid=981) |
SHAIRI: KUSANYENI KAZI ZANGU - MwlMaeda - 08-22-2021 KUSANYENI KAZI ZANGU Leo nimewaza mbali, vipi kifo nikihozi, Nimegutuka akili, niwachie kumbukizi, Changu kifo kiwasili, niwachie simulizi, Kusanyeni kazi zangu! Vile nimetunga sana, beti mashazi mashazi, Chunguzeni yenye vina, na mizani mabobezi, Yaharirini kwa kina, hifadhini makavazi, Kusanyeni kazi zangu! Mfano ya Mnyapala, yule bwana mbobezi, Basi siku nikilala, wa milele usingizi, Fanyeni bila kulala, kutafuta tungo hizi, Kusanyeni kazi zangu! Maradhi mengi mwilini, hunijia siku hizi, Uviko nao jueni, waleta maangamizi, Heri niwaambieni, na isiwe shitulizi, Kusanyeni kazi zangu! Nimekaribia kupanga, miswada jozi kwa jozi, Kipato kinanizinga, kinipacho pingamizi, Vile bure ninatunga, tena kuache siwezi, Kusanyeni kazi zangu! Nafahamu wasomaji, sio kama hawawezi, Hao ni kama walaji, na muweni watetezi, Basi muwe wabebaji, kafanyeni uchambuzi, Kusanyeni kazi zangu! Nikikumbuka kaburi, kwacha kutunga siwazi, Kwanza naongeza ari, hili niliseme wazi, Nanyi pia mtakiri, ushairi ni mwokozi, Kusanyeni kazi zangu! Sikumjua Shabani, pasi kuziona kazi, Shabani yu kaburini, ameacha simulizi, Nitaacha kitu gani, mkitie simulizi? Kusanyeni kazi zangu! Mfano leo ajali, ikasimama pumzi, Msilie nyie bali, yafanyeni maongezi, Tangu tungo ya awali, kusanyeni msisizi, Kusanyeni kazi zangu! Bai bai nasimama, shairi siendelezi, Shikeni niliyosema, muhimu habari hizi, Fanyeni bila kukoma, ruhusa siwakatazi, Kusanyeni kazi zangu! Mtunzi Filieda Sanga Mama B Mabibo Dsm 0753738704 |