SHAIRI: BURIANI MWALIMU KASHASHA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: BURIANI MWALIMU KASHASHA (/showthread.php?tid=941) |
SHAIRI: BURIANI MWALIMU KASHASHA - MwlMaeda - 08-20-2021 [attachment=573] MASHAIRI YA JEMADARI Ng'anzi Jr @ 2021 © PIGO KWA WANAMICHEZO Machozi yamiminika, hadi ardhi imetota, Huzuni imetushika, ukomoni imegota, Msiba umetufika, Mola kaitwaa Nyota, Kenda mwalimu Kashasha, pigo kwa wanamichezo. Tulicheka hivi juzi, kwa mzaha wa mahoka, Hivi leo mchambuzi, eti ndipo katutoka, Alikuwa ni mjuzi, kwa kulichambua soka, Kenda mwalimu Kashasha, pigo kwa wanamichezo. Kifo chaja matumatu, wala hodi hakibishi, Kashasha mtu wa watu, mahiri wa tashuwishi, 'Tuto msahau katu, hilo halina ubishi, Kenda mwalimu Kashasha, pigo kwa wanamichezo. Ajiraye TBC, akichambua michezo, Alikuwa na bidii, hayatoshi maelezo, Kwa talanta humwingii, wa juu wake uwezo, Kenda mwalimu Kashasha, pigo kwa wanamichezo. Machozi yanakinzana, na wala hayakauki, Amejifia mchana, sipitali Kairuki, Tulikuwa naye jana, kweli kifo taharuki, Kenda mwalimu Kashasha, pigo kwa wanamichezo. Sifa zake niziweke, ujue japo kidogo, Ndiye bingwa wa makeke, akitia na mikogo, Na ni lazima ucheke, hadi ujirambe chogo, Kenda mwalimu Kashasha, pigo kwa wanamichezo. Namba moja kwenye chati, soka akidadavua, Bingwa wa misamiati, maneno mengi ajua, Leo mwalimu mamati, kifo kimemchukua, Kenda mwalimu Kashasha, pigo kwa wanamichezo. Ng'anzi sinalo? la hasha! Ila papa tamatani, Nenda mwalimu Kashasha, lala pema buriani, Nasi pia twafungasha, tukufate aherani, Kenda mwalimu Kashasha, pigo kwa wanamichezo. Makiwa! Salim Hussein Ng'anzi ( Jemadari ) Simu/Whattsap: 0626 884 160 Facebook: Ng'anzi Junior Jr. E-mail: nganzijunior@gmail.com Moshi-kilimanjaro |