FASIHI, UANDISHI NA UCHAPISHAJI (6) - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Watunzi wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=17) +--- Thread: FASIHI, UANDISHI NA UCHAPISHAJI (6) (/showthread.php?tid=844) |
FASIHI, UANDISHI NA UCHAPISHAJI (6) - MwlMaeda - 08-14-2021 SEHEMU YA PILI: UANDISHI
5. Lugha Kama Kifaa cha Usanii
Ruth M. Besha
Utangulizi
Matumizi ya lugha ni mojawapo ya mambo muhimu yanayoitofautisha kazi ya fasihi na kazi isiyo ya fasihi. Mwanafasihi ni msanii na katika sawia hii hana tofauti kubwa na msanii wa aina nyingine. Kila msanii anacho kifaa chake ambacho anakitumia, ambacho kinakuwa alama ya usanii wake. Mchoraji anategemea kalamu na/au rangi zake, na mchongaji anao ubao au mti wake. Vivyo hivyo mwanafasihi naye anategemea lugha katika usanii wake. Jinsi mwandishi anavyoitumia lugha yake, na kiwango cha usanii anachofikia, ndiyo alama muhimu inayomtofautisha na mwandishi mwingine wa fasihi.
Katika uhakiki wa kazi za fasihi za hivi karibuni, hasa katika Kiswahili, kumekuwa na msisitizo mkubwa katika maudhui ya kazi hizo, au kwa lugha rahisi, ujumbe unaotolewa na mwandishi. Hivyo maswali yanayoulizwa ni kama: kazi hii ina umuhimu gani katika jamii ya leo; inajengaje tabia, mwenendo na mwelekeo wa jamii; ina maadili gani? Mara nyingi wahakiki hawaulizi jinsi mwandishi alivyofaulu kisanaa, isipokuwa kama jambo la ziada tu mwishoni. Uhakiki wa namna hii hasa umehusu kazi za fasihi zisizo za ushairi, kwa sababu imekubalika kwa muda mrefu kuwa mshairi lazima aitawale lugha yake vizuri ndipo aweze kuleta ule mvuto maalumu unaotakiwa na kufikia viwango vilivyokubalika katika fani hii.
Makala haya yanadai kuwa haiwezekani kutenganisha maudhui na usanii katika kazi yoyote ile ya fasihi. Ujumbe unaotolewa katika kazi ya fasihi unaweza kutolewa na mtu mwingine yoyote kwa njia nyingine, Ujumbe huo unaweza kutolewa kwa njia ya hotuba, au vitabu au kwa maongezi ya kawaida. Kwa vile kazi ya fasihi ni mtindo wa uandishi ambao unategemea sana matumizi maalum ya lugha, makala haya yanajaribu kujibu swali: Ni matumizi gani haya ya lugba yanayoitofautisha kazi ya fasihi na kazi isiyo ya fasihi, na zaidi ya hapo ni vipengde gani vinamtofautisha mwandishi stadi na mwandishidhaifu?
Ujuzi wa Lugha
Katika isimu ya lugha, tunaposema kuwa mwanadamu anaijua lugha yake tuna maana kuwa ‘amemeza’ mfumo wa lugha yake wa matamshi, wa muundo wa maneno, muundo wa sentensi na maana zinazokusudiwa. Ujuzi alio nao mwanadamu huyu ni sawa na ujuzi walio nao wanadamu wengine wa jamii yake wanaozungumza lugha moja. Tukitumia istilahi za mwanaisimu maarufu De Saussure, tunasema wote ni warithi wa langue hiyohiyo. Ujuzi huu wa lugha unadhihirika tu katika matumizi. Kila wakati mtu anapozungumza (au kuandika) anachota tu kiasi kidogo kutoka katika ghala hii ya ujuzi alio nao. Tukitumia istilahi za De Saussure tena tunasema kuwa kila kitendo cha usemi – parole – ni udhihirisho wa ujuzi huu – langue.
Hivyo tukisema kuwa mwanadamu anajua lugha, hatuna maana tu ya kule kuumeza mfumo wa lugha yake, bali ni uwezo wake wa kuitumia katika mahusiano yake na wanajamii wengine. Hivyo vitendo vya utumizi huu – parole – ni muhimu sana katika kutimiza makusudio ya kuwepo kwa lugha katika jamii.
Katika lugha yoyote ile kuna mitindo mingi inayotumika kutegemea kile kinachozungumziwa. Hivyo tunaweza kuwa na mtindo wa siasa, wa sheria, wa dini, n.k. Pia upo mtindowa kawaida unaotumika katika mawasiliano ya kila siku kati ya wanajamii moja. Katika mtindcr huu wa kawaida kuna matumizi ya aina mbalimbali kuhusiana na nyanja tofauti za maisha. Matumizi haya yanaitwa rejesta kwa lugha ya kitaaluma. Rejesta yoyote ile inategemea nani anazungumza nini, na nani, wapi, na kuhusu nini.
Mtu anayeijua lugha yake vizuri, tunamtegemea aweze kuitumia katika mitindo iliyokubalika, na aweze kujua mazingira anayopaswa kutumia mtindo mmoja badala ya mwingine. Katika mahusiano ya kawaida, mtumiaji wa lugha anapaswa kujua ni rejesta gani anapaswa kuitumia kila wakati. Katika mkabala wa makala haya tunaweza kusema kuwa mwandishi wa fasihi lazima awe ‘amefuzu’ katika kuelewa haya matumizi tofauti ya lugha. Anatakiwa kuwa mtafiti ili ajue hata yale matumizi ambayo yeye hana haja nayo katika mahusiano yake ya kawaida, na hivyo aweze kuichora jamii yake inavyostahili katika kazi yake. Sababu kubwa ya kumtaka mwanafasihi kuyajua kinaganaga matumizi tofauti ni ule ukweli kuwa kazi ya fasihi haina mipaka ya utumizi wa lugha. Ni kawaida kukutana na mitindo tofauti na rejesta mbalimbali katika kazi hiyo moja kufuatana na visa vinavyosimuliwa na wahusika walivyo. Ikiwa, kwa mfano, katika riwaya yuko hakimu anayetakiwa kutoa hukumu katika kesi ya uhaini, tutatarajia kumsikia akitumia mtindo wa kimahakama. Na hatutarajii marafiki wawili waliotembeleana waongee katika rejesta rasmi ambayo tungeihusisha na hotuba ya kiongozi wa siasa.
Juu ya yote hayo, ni lazima mwandishi wa kazi ya fasihi ajue jinsi ya kutumia lugha kisanii ili kuhakikisha kuwa kazi yake ina mvuto wa pekee utakaowahamasisha wasomaji au wasikilizaji wake. Ni muhimu kukumbuka kuwa kazi kubwa ya fasihi ni kutoa ujumbe maalumu kwa njia ya kuburudisha.
Tunapoangalia lugha kama kifaa cha usanii cha mwanafasihi yapo mambo muhimu ambayo yanasaidia kufanikisha usanii huo. Hapa tutagusia machache tu.
Matumizi ya Taswira
Wahakiki walio wengi wanakubaliana kuwa mojawapo ya sifa muhimu za kazi ya fasihi ni ufundi wa mwandishi katika matumizi yake ya taswira mbalimbali, na hasa wamesisitiza sitiari.1 Sifa muhimu ya taswira ni ule uhusiano uliopo baina ya maana halisi ya neno au tungo na maana hamishi ya neno hilo au tungo hiyo; yaani uhusiano baina ya ile maana ambayo inakubalika katika matumizi ya kawaida na ile ambayo inafananishwa nayo kwa ajili ya kuleta mvuto maalumu.
Zipo sababu kadhaa ambazo zinafanya taswira, na hasa sitiari, ziwe na umuhimu wa pekee katika kazi ya fasihi. Kwanza, kadka matumizi ya taswira ishara inaweza kuashiria kitu kimoja bila kuacha kuashiria kingine. Yaani ishara hiyohiyo inafanya kazi za aina tofauti bila yenyewe kuathirika. Pili, taswira haionyeshi tu uhusiano ulio wazi kati ya vitu, bali pia huvumbua mahusiano yaliyofichika kati ya vitu vinavyoonekana tofauti sana. Jambo muhimu zaidi ni kwamba matumizi ya taswira yanampa mwandishi uhuru mkubwa sana katika usanii wake. Sababu yake ni kwamba miundo inayoruhusiwa katika sarufi ya lugha yoyote ile ina mipaka yake, na si rahisi kuitanua kupita kiwango fulani. Hata maana halisi zinazobebwa na maneno ya lugha pia zina mipaka, ingawa hapa maneno yenye kufanana katika maana yanaweza kumpa mwandishi uhuru zaidi wa kuchagua neno moja badala ya jingine. Lakini matumizi ya taswira hayana mipaka, na mwandishi ana uhuru wa kuunda sitiari zake kwa kadiri ya ufundi alio nao. Washairi wenye sifa wameweza kutumia uhuru huu kwa kiwango kikubwa sana. Hata waandishi wachache wa riwaya wameonyesha ufundi mkubwa katika kuunda sitiari, ambazo zimezipa ladha za kipekee kazi zao za fasihi.2
Hata hivyo kuna’sharti muhimu ambalo linatawala uwezo wa mwandishi wa kutumia taswira kisanii. Huu ni umilisi alio nao juu ya lugha anayotumia. Kama ilivyoelezwa katika sehemu zilizotangulia, ni muhimu mwandishi aijue lugha yake vizuri sana, na pia awe mtafiti wa matumizi tofauti ya lugha hiyo.
Si rahisi kuwa muundaji wa kitu usichokielewa vizuri. Uundaji unasisitizwa hapa kwa sababu matumizi ya taswira mbalimbali ni jambo la ujumla katika maisha ya kila siku, na katika matumizi ya kawaida ya lugha. Msanii mzuri ni yule ambaye ataunda taswira zenye mchomo usio wa kawaida kwa wasomaji wake. Matumizi ya taswira za kawaida yanaifanya kazi ya fasihi kuwa butu na ya kuchosha.
Ingawa taswira zinaweza kutumika mahali popote katika kazi ya fasihi, lakini matumizi yake ni muhimu sana pale ambapo mwandishi anatoa msimamo wake wa kifalsafa. Hapa tunatofautisha lugha ya maongezi kati ya wahusika, na lugha ya masimulizi hasa mwandishi anapoongelea dhana zenye udhahinisho (abstraction) wa kiwango cha juu. Mawazo ya kidhahinisho katika kazi ya fasihi yakikosa taswira za aina yoyote yanaweza kumkatisha tamaa msomaji ashindwe kuendelea kusoma. Ni vizuri kukumbuka kuwa msomaji hana njia nyingine ya kufidia uchovu wa maandishi au uandishi mbaya.
Katika sehemu hii tumesisitiza zaidi matumizi ya taswira kwa sababu ndizo zinazojitokeza mbele katika kazi ya fasihi, na kukosekana kwake kunaleta hitilafu za wazi katika kazi hiyo. Lakini kuna vigezo vingine vya kisanii ambavyo vina umuhimu wake katika fasihi. Kwa mfano, misemo mbalimbali, methali, vitendawili, na mafumbo, ni tungo zinazoweza kutumiwa kwa ufundi na msanii. Hata hapa msanii bora ni yule atakayeweza kuziunda upya semi hizi, bila kupotosha maana zinazotegemewa na wazungumzaji wengine katika jamii. Matumizi ya semi hizi ni tofauti na matumizi ya taswira. Msanii hawezi kubadili, au kuvuta sana maana zilizopewa semi hizi na kukubalika na jamii nzima, isipokuwa anaweza kuziwekea mazingira ya kuvutia, yanayosadifu utumiaji wake.3
Uteuzi wa Maneno
Uteuzi makini wa maneno ni mbinu nyingine ambayo mwandishi anaweza kuitumia ili kutajirisha utunzi wake na kuupa mwelekeo maalum. Mbinu hii haitofautiani sana na ile ya matumizi ya taswira na tamathali nyingine za usemi, kwa sababu maneno yanaweza kuteuliwa tu kufuatana na mazingira maalumu, na kwa kuhusishwa na maneno mengine katika tungo inayohusika. Hata hivyo tunaweza kuyatenga maneno na kuchambua matumizi yake ili kuona jinsi mwandishi anavyoweza kuyatumia katika kuunda sanaa bora zaidi.
Makundi makubwa ya maneno ambayo yanaleta athari kubwa katika mtindo ni nomino (au majina) na vitenzi. Utumiaji wa vivumishi, vielezi na aina nyingine za maneno ukizidi katika kazi ya fasihi unaifanya kazi ipwaye na kukosa ladha. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa maneno ya aina hii havazidi vale ya makundi makubwa ya mwanzo.
Maneno, kwa asili yake, yana sifa moja kubwa, nayo ni ile ya kuweza kubadilishana nafasi na maneno mengine, na kuleta maana inayofanana. Sifa hii inamsaidia msanii kukwepa kujirudiarudia, ingawaje ni kweli pia kwamba hakuna maneno mawili ambayo ni sawa kabisa katika maana zake.
Tunaweza pia kuangalia uteuzi wa maneno katika viwango vya umbo (matamshi) na pia maana. Neno likitamkwa tu linaweza kuibusha hisia maalumu kwa sababu ya ile maana inayoashiriwa, na msomaji atamtarajia mwandishi amridhishe matarajio yake.4
Pamoja na umbo la neno ni ile maana halisi inayowakilishwa na neno fulani. Lakini wakati huohuo hii ni maana ya ujumla tu. Maneno yanayo tabia moja muhimu ya kuwa na utata. Mwandishi anaweza kuutumia utata huu ili kufumba maana anayokusudia na kumhamasisha msomaji kuigundua maana iliyofichwa.
Pamoja na uteuzi wa maneno, tunaweza kutaja pia uundaji wa maneno mapya. Mwandishi hodari anayo nafasi nzuri ya kutumia mbinu za uundaji wa maneno katika kuongeza msamiati anaoutaka katika kazi yake. Lugha ya Kiswahili inao uhuru mkubwa katika uundaji wa maneno, hasa nomino pamoja na vitenzi. Maneno yanayoundwa kwa kufuata mbinu zilizokubalika katika lugha hayana tatizo la kutoeleweka na wasomaji, na kwa njia hii mwandishi anaweza kuongeza uwezo wake wa kupata maneno anayohitaji. Hapa tena washairi wameweza kuitumia mbinu hii vizuri, na ingefaa wanafasihi wengine pia wawe na ujasiri wa kuitumia.
Uteuzi wa Miundo ya Sentensi
Kila lugha inazo njia zinazokubalika au zinazoruhusiwa za uundaji wa sentensi zake. Lakini makubaliano hayo, kama yale tuliyoyataja kuhusu maana za maneno, ni ya ujumla tu. Kuna uwezekano mkubwa wa kubadilisha na kubuni miundo mipya bila kuasi kabisa miundo hiyo ya ujumla. Wapo hata wanaisimu wanaodai kuwa kila sentensi anayotoa mwanadamu ni mpya kwa kiasi fulani, na hivyo kusisitiza umbuji wa lugha.5 Msanii kama muumbaji wa sanaa yake anao uhuru wa kuutumia umbuji huo wa lugha. Matumizi ya aina maalumu ya miundo ya sentensi ni mojawapo ya sifa kubwa zinazomtofautisha mwandishi mmoja na waandishi wengine. Na kwa kweli wahakiki wakizungumzia kuhusu mtindo wa mwandishi fulani wa fasihi, mara nyingi wanatumia kigezo cha miundo ya sentensi zake. Kati ya vipengele vinavyochunguzwa ni: mahali mwandishi anapoweka taarifa muhimu katika tungo; urefu wa sentensi zake; vihusishi na viunganishi anavyotumia kama alama za mshikamano wa vipashio vinavyounda sentensi zake, na jinsi vishazi vya sentensi vinavyohusiana. Kwa mfano, ni kawaida kufikiria kuwa taarifa yenye umuhimu wa pekee huwekwa mwanzoni mwa tungo, hata ikiwa itakuwa lazima kubadili muundo wa kawaida wa sentensi. Kwa mfano ni jambo la kawaida katika Kiswahili kuanza sentensi na nomino yambwa badala ya nomino kiima bila kubadili upatanisho wa kisarufi katika fungu tenzi, kama mbinu mojawapo ya kutoa umuhimu wa pekee katika nomino yambwa. Au kuanza sentensi na kiarifu badala ya kiima kama wanasarufi wanavyotuasa.
Hata hivyo si rahisi kutoa sheria maalumu kuhusu uteuzi bora wa miundo ya sentensi. Lakini kama ilivyosemwa katika sehemu zilizotangulia, kuna mvuto maalumu katika kukiuka sheria za kawaida katika lugha. Kwa mfano, katika vitabu vya sarufi tunaaswa kuhakikisha kuwa tunatumia sentensi ‘kamili’, hivyo kila sentensi lazima iwe na kiima na kiarifu kinachodhihirika. Lakini mwandishi wa fasihi akitii sheria hii sisisi ataunda kitu duni sana. Hivyo hatustaajabu tukisoma sentensi hii mwanzoni mwa riwaya: “Alifungua mlango taratibu na kutoka nje…” bila kuambiwa a inakuashiria nani, kwa sababu kama wasomaji tunajua kuwa mwandishi lazima atatueleza baadaye, na hatuom ugumu wa kukubali muundo huu.
Waandishi wengine wanao ufundi mkubwa wa kutumia sentensi fupifupi, lakini zenye “mwendo wa haraka”, na wengine wanao ufundi wa kutumia sentensi ndefu kwa kuchagua vizuri uhusishi au uunganishi unaofaa. Lakini matumizi ya sentensi ndefu yanahitaji uangalifu mkubwa zaidi kumwezesha msomaji kufuata kisa mpaka mwisho bila kupotea katikati. Ikiwa msomaji atahitaji kurudia sentensi moja mara mbili au tatu ndipo aielewe, hapo itakuwa dhahiri kuwa mwandishi ameshindwa kushikamanisha vyema vishazi katika sentensi yake.
Hitimisho
Lugha ni mali ya pamoja ya jamii ya wale wanaoizungumza. Wote wamemeza langue moja, na wote wanapaswa kutii sheria na mipaka yake. Lakini pia lugha ina umbuji na unyambulikaji. Ikikumbukwa pia kuwa ni mwanadamu ndiye anaitawala lugha, itakubalika kwa urahisi kuwa mtumiaji wa lugha anao uhuru wa kuibinua misingi yote ya lugha ili ikidhi mahitaji yake. Mwandishi wa fasihi, kama mtumiaji yoyote wa lugha, anashiriki katika uhuru huu. Lakini yeye, kuliko wazungumzaji wengine, anayetakiwa kuwa na kipawa maalumu cha kutumia lugha kisanii na kuunda sanaa itakayodhihirisha kwa kiwango cha juu zaidi utepetevu huu wa lugha. Yeye, zaidi ya yote, ni mtafiti na mchunguzi wa j’.nsi lugha inavyotumika katika mazingira tofauti. Hivyo yeye ni mtumiaji wa nyenzo ambazo wanajamii wengine wanazijua lakini hawana utaalamu wa kuzitumia.
Tanbihi
Quote: Quote: Quote: Quote:Quote: Quote: Quote: Marejeo
Chapman, Raymond. (1980) Linguistics and Literature: An Introduction to Literary Stylistics. Edward Arnold.
Chatman, Seymour (Ed.) (1971) Literary Style: A Symposium. Oxford University Press, Oxford.
Chomsky, N. (1965) Aspects of the Theory of Syntax. M.I.T. Press, Cambridge.
Freeman, Donald C. (Ed.) (1970) Linguistics and Literary Style. Holt, Rinehart and Winston, Inc.
Halliday, M.A.K. (1971) “Descriptive Linguistics in Literary Studies.” Katika Freeman (Ed.) 57-72.
Khamis, S.A.M. (1981) The Aesthetic Idiom of Mohamed Suleiman’s Writings (Literary Discourse). M.A. Dissertation, University of Dar es Salaam.
Ohmann, Richard (1970) “Generative Grammars and the Concept of Literary Style”. Katika Freeman (Ed.), 258-278.
Turner, G.W. (1973) Stylistics. Penguin Books, Harmondsworth.
Ullmann, Stephen (1971) “Stylistics and Semantics” katika Chatman (Ed.) 133 – 152.
|