SHAIRI: MAHABA YAKICHACHA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: MAHABA YAKICHACHA (/showthread.php?tid=828) |
SHAIRI: MAHABA YAKICHACHA - MwlMaeda - 08-13-2021 *Mahaba yakichacha* Kama sikio la kufa, Lisivyosikia dawa, Nayo Mahaba yakifa, Mambo yote huuawa, Hata uyatwike sifa, Muhali kufufuliwa, Mahaba yakishachacha, ndimu haiyachachui. Yakizikwa yamezikwa, Kaburile hufukui, Hata kama yangepikwa, Kwa mafuta kwa karai, Ni kama mtu kutekwa, Kafishwa si kuzirai, Mahaba yakishachacha, ndimu haiyachachui. Kutwa nilibembeleza, Machozi nikamwagia, Nikambiwa yameoza, Tabu bure najitia, Maneno sikuyasaza, Kitu sikuambulia, Mahaba yakishachacha, ndimu haiyachachui. Nalia sina bahati, Kwa penzi mimi yatima, Nipo kwenye hatihati, Mapenzi yamenihama, Nipo kwenye kavu kuti, Moyo waenda mrama, Mahaba yakishachacha, ndimu haiyachachui. Ninahitaji kiota, Ndege nipate kutua, Nikilala ninaota, Ndoto za kunisumbua, Niwezesheni kupata, Stara nipate tua. Mahaba yakishachacha, ndimu haiyachachui. *Shaaban Mwinyikayoka* (Mwanaupwa) Iringa 0715439740 |