SHAIRI: KAMWAMBIE NAFARIKI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: KAMWAMBIE NAFARIKI (/showthread.php?tid=795) |
SHAIRI: KAMWAMBIE NAFARIKI - MwlMaeda - 08-07-2021 KAMWAMBIE NAFARIKI Shairi ninakutuma, Mwambie sitamaniki, Sasa yanizidi homa, Imenizidi ashiki. Ajila na aje hima, Ajilani nafariki, Mekuwa mwendawazima, Kila mja hanishiki. Uhai unanihama, Naugua sitibiki, Roho bado kunizima, Sadiri haidundiki. Ndiye wangu muadhama, Mwinginewe simtaki, Na awasili mapema, Kumsubiri sichoki? Nazinduka na kuzima, Anambie hanitaki? Ila nikifa mapema, Kamwambie haniziki. Ni yule mtu mzima, Nini hakieleweki? Au mapendo kazima, Siku hizi hayawaki? Japo macho natazama, Na kitandani sishuki, Na muhu yanisakama, Bado haiteremki, Mapenzi niliyofuma, Mwambie hayafumuki, Maana yaniandama, Kunondoka hayataki. Sina haja mahakama, Kumuaili sitaki, Anionee huruma, Ajue nitafariki. Basi mwanzoni mwa juma, MIkiwa leo hafiki, Kama tena atagoma, Ndio siku nafariki. Hapa sinipe lawama, Nikifa ndo sizinduki, Takumbuka wangu wema, Hilo ninalisadiki. Neno halirudi nyuma, Ya wavyele hakumbuki? Na tayari nimesema, Ajue halifutiki. Nivyotanguza kusema, Kitandani sibanduki, Au penzi amepima, Akaona haridhiki? Mimi bado niko wima, Mahaba hayanyauki, Si kama ua kuchuma, Kwangu halifananiki. Lakini mimi si kama, Mzigo haubebeki, Mahabani najituma, Nitoe yanostahiki. Kamwambie aje hima, Mlango haufungiki, Tena apitie nyuma, Mbele kuna mamluki. Beti kadha nasimama, Sijitwezi sijinaki, Shairi nimelichuma, Kulisoma hamtaki? Mtunzi Filieda Sanga Mama B Mabibo Dsm 0753738704 |