FASIHI SIMULIZI: MUHADHARA WA SITA: AINA ZA HADITHI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Hadithi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=48) +---- Thread: FASIHI SIMULIZI: MUHADHARA WA SITA: AINA ZA HADITHI (/showthread.php?tid=763) |
FASIHI SIMULIZI: MUHADHARA WA SITA: AINA ZA HADITHI - MwlMaeda - 08-04-2021 MUHADHARA WA SITA: AINA ZA HADITHI Istiara,Mbazi na Kisa
(a) Istiara
Ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine isiyo ya wazi. Ni masimulizi ya kiishara yenye kutumia wanyama au taashira za aina mbalimbali zinazowakilisha wanyama hao.
Hadithi kama za sungura,majitu na kobe huwa zinawakusudia watu. Hadithi hizi hutumia wanyama kama vielelezo vya sifa na tabia za binadamu. Baadhi ya wataalamu wa sanaa waliotumia sana Istiara ni Shaaban Robert katika Adili na Nduguze, Kufikirika na Kusadikika.
Katika kazi hizo vitu,watu na wahusika vinasimamia mawazo na adili fulani maalumu.
(b) Mbazi
Ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama mfano wakati wa maongezi au kumwonya mtu. Mwalimu aliyevunja rekodi katika matumizi ya aina hii ya hadithi alikuwa Yesu Kristo.
Alitumia mbazi kwa kiasi kikubwa kuwaelekeza wanafunzi wake na walimwengu katika mafundisho yake.
Mfano wa mbazi ni huu:
Kiongozi mmoja wa kitaifa alikuwa akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kushiriki katika kulinda usalama na amani nchi badala ya kuona suala hilo ni la watu fulani tu hasa vyombo vya ulinzi na usalama. Katika msisitizo wake huo akatoa mbazi ifuatayo…………. siku moja katika nyumba fulani panya aligundua kuwa ametegewa mtego na kwa kuwa hakuweza kuutegua alienda kuomba msaada kwa ng’ombe lakini ng’ombe alikataa akidai kuwa huo ni mtengo wa panya yeye haumuhusu. Panya hakuchoka akapiga hodi kwa mbuzi na kumlilia shida yake, mbuzi naye akamjibu kama alivyojibu ng’ombe kuwa huo ni mtego wa panya wala haunihusu. Hatimaye panya akamwendea jogoo na kueleza yote lakini jogoo naye alimkatalia panya na kumkejeli kuwa huo mtego hamhusu yeye jogoo. Baada ya kugonga mwamba panya akakosa amani akihofia mtego ulioitwa.. “ …wa panya..” kwa kweli siku nzima ile panya hakuweza kujipatia riziki akihofia mtego. Usiku ulipofika baba mwenye nyumba alishituliwa na mkewe akiambiwa kuwa mtego umefyatuka na bila shaka panya atakuwa amenaswa. Baba yule akakurupuka na kuuendea mtego huku akipuuza hadhari ya mkewe kuwa asiende giza giza, alienda huku akijifariji kuwa panya hawezi kumdhuru chochote……alipoufikia mtego ule akapeleka mkono ili auchukue na kumsulubu panya aliyewasumbua kitambo. La haula! Kumbe hakuwa panya, mzee yule akarudi nyuma haraka huku akiagiza mkewe amletee taa haraka. Baada ya taa kuletwa ikabainika mtego ulinasa nyoka na hivyo mzee yule aliumwa na nyoka yule…..ghafla hamkani ikaingia ndani ya nyumba kutafuta dawa ya kumponya mzee mwenye nyumba. Muda si muda mzee yule alikata roho kwa kuzidiwa na sumu ya nyoka na nyumba ikawa na tanzia. Siku ya kwanza wageni wachache ikabidi achinjwe jogoo kupata kitoweo. Siku ya pili wageni ni wengi kiasi ikabidi achinjwe mbuzi ili kukidhi mahitaji. Baada ya maziko siku ya tatu na kumaliza tanga akachinjwa ng’ombe.
Funzo:
Hivi ule mtego ulikuwa wa panya,ng’ombe,mbuzi,kuku au baba mwenye nyumba? Mbazi hii inasadifu umuhimu wa kushirikiana kuokoa mambo ambayo yakiharibika yataathiri wengi.
© Kisa/kidahizo
Ni masimulizi mafupi yanayohadithia tukio moja bila ya kulifafanua kwa mfano; kidahizo cha nyani na mtoto wake.
Nyani na mtoto wake walikwenda kula mahindi katika shamba,wakala,wakala,wakala,halafu mtoto aliuliza,…… “mama tunakula tu,je mpaka uko wapi?” mamaye akamjibu …. “we kula tu mpaka wataweka wenyewe.”
Kidahizo chaweza kutokana na tukio la kweli lenye kuchekesha.
|