SHAIRI: FUKARA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: FUKARA (/showthread.php?tid=610) |
SHAIRI: FUKARA - MwlMaeda - 07-21-2021 Fukara Fukara hapati konde, jembele likatumika Mazao humo apande, kwa wingi yakapatika Lake kuzoga umande, na nguvuze kumtoka Mwishowe kwenda upande, mgongo ukakatika. Fukara yake faraja, ni mate kumdondoka Watu wakikidhi haja, kwa minofu ya kuoka Harufu kwake zikaja, na pua ikatanuka Hata roho ikataja, lini kwake itafika. Jirani akifurahi, siku ya pili kufika Yeye hana masilahi, amekosa chakupika Ishafika asubuhi, na macho yashamtoka Ni lipi kwake sahihi, kama mja kutumika? Fukara hana rafiki, moyoni alomuweka Wakwasi hawamtaki, kuombwa wameshachoka Anofaidi ni dhiki, na mazonge kuzongeka Mwishowe hufanya chuki, na hasadi kujengeka. Ufukara ukizidi, nchi itasawajika Sababu ya uhasidi, na mali zitageleka Nyoyo zikataradadi, furaha itafutika Zitadamiri biladi, thamaniye itashuka. Enyi wenye karatasi, ambazo zahesabika Fanyeni haraka basi, mambo yasije chafuka Ufukara ni utesi, heshima utatupoka Nawaita wangu mbasi, tutoweni pasi shaka. Ali Ben Othman Zanzibar 21/7/2021 3:50 |