NYANYA SHUKA BEI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: NYANYA SHUKA BEI (/showthread.php?tid=586) |
NYANYA SHUKA BEI - MwlMaeda - 07-17-2021 ”NYANYA SHUKA BEI” Nyanya umeleta shida, kipi tulichokukwaza Kila soko we ndo mada, watu wakuzungumza Umetoweka kwa muda, na bei ukajikweza Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei. Nyanya moja hadi jero, utadhani Coca-Cola Unasakwa ngarenaro, bongo hadi ilemela Waumiza wapogoro, chaga na kila kabila Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei. Nakumbuka enzi zako, nyanya kumi mia mbili Tukaangua vicheko, ukioza hatujali Leo sasa zamu yako, umetupiga kabali Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei. Kweli tulikudharau, tukakutupa jaani Kumbe we hukusahau, ukayaweka moyoni Leo umepanda dau, ndio tunakuthamini Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei. Hatuli tena michuzi, tumebaki kulumanga Zimekosa bei nazi, hunogi tena mpunga Metunyima usingizi,vitambi vinatuchenga Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei. Kukukata kachumbari, hakuna wa kuthubutu Walala kwa matajiri, hutaki kurudi kwetu Umekuwa mashuhuri, na hutukumbuki katu Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei. Rafikizo bilinganya, kitunguu na karoti Hawajui Cha kufanya, mbona umewasaliti Na adui yako panya, kakumisi Sana eti Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei. Lile chuzi shatashata, tulilomezea mate Limekuwa pwatapwata, mradi tonge lipite Kwa manji tunakukuta, na nyumbani kwa dangote Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei. Ewe nyanya shuka bei, ili tuheme wanyonge Kwa michuzi tujidai, yasitukwame matonge Mama lishe wapo hoi, yanadorora magenge Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka beiii…! Dada D. Malenga wa Uhehe |