Utungaji Wa Kazi Za Kifasihi - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Uandishi/Utungaji (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=12) +--- Thread: Utungaji Wa Kazi Za Kifasihi (/showthread.php?tid=579) |
Utungaji Wa Kazi Za Kifasihi - MwlMaeda - 07-16-2021 Kazi za fasihi simulizi hazikutokea tu, zilitungwa. Mtu fulani alikaa na akatunga kazi fulani ambayo inajulikana katika jamii. Katika mada hii utajifunza kanuni mbalimbli zinazohusika na utunzi wa kazi za fasihi simulizi. Pia utapata fursa ya kujifunza jinsi ya kutunga kazi mbalimbali za fasihi simulizi kama vile ngonjera, methali , nahau, vitendawili na kazi nyingine. Utajifunza pia kanuni zinazoongoza utunzi wa kila kazi ya fasihi simulizi.
Mashairi Kanuni za Utungaji wa Mashairi
Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi atumie milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya fahamu mitano ambayo ni pamoja na: kuona, kunusa, kusikia, kuhisi, na kuonja.
Uzoefu wa Mwandishi
Uzoefu ni hali ya kukaa au kujishughulisha na jambo au kitu kwa muda mrefu. Mwandishi ana uzoefu (uzoevu) wa kukabiliana na maisha kwa kiasi gani? Je, ni matatizo gani ambayo umekutana nayo katika maisha yako? Je, ni mafanikio gani umekutana nayo katika maisha yako? Kwa mfano, katika ajali ya MV Spice (2011) kuna baadhi ya watu waliokolewa na magodoro ya Tanzania? Magodoro haya yana nailoni na je kama yasingekuwa na nailoni? Uzoevu/uzoefu wako ukoje?
Uchunguzi/utafiti
Uchunguzi unapaswa ufanywe na mwandishi ili aweze kuandika jambo au tukio bila kuongopa. Kwa kufanya udanganyifu, mwandishi atapoteza imani yake kwa wasomaji wa kazi zake.
Uchunguzi ili ufahamu au ujue mtu, mnyama, mdudu na kadhalika – anatembeaje, anakulaje, analalaje, anaishije, anachekaje, analiaje, anazaaje, anahusianaje na wenzane na mazingira yake? Haya ni maswali muhimu katika kumwezesha mtunzi kufanya utafiti wa kina ili ajue kitu anachotaka kukiandika akiandikaje na akiwasilishaje ili aweze kuikamata hadhira(walengwa) yake.
Mwandishi baada ya kuzingatia mambo haya sasa anaweza kuanza kutunga kazi yake. Hapa sisi tutajikita zaidi katika utunzi wa mashairi. Kabala hatujaenda katika hatua ya utunzi ni muhimu kujua dhana ya shairi kwa ujumla wake, na baada ya hapo tutakuwa tumekwisha pata maarifa yakutosha juu ya mashairi ambayo yatatuwezesha kutunga mashairi.
Dhana ya shairi
Shairi ni kipande cha maandishi kilichopangwa kwa utaratibu katika mistari. Sauti za silabi hufanana zikiwa kati au mwisho mwa mstari. Maandishi hayo yakisomwa huleta ujumbe na hisia fulani ya kimaisha.
Mpango wa maneno ya shairi, ambao huweza kuimbwa hutoa picha wazi, maana halisi na burudani ya kimuziki. Nyimbo nyingi za makabila zimepangiliwa kishairi ijapokuwa hazikuandikwa.
Mashairi yana umbo ambalo huonekana kwa mpangilio wa sauti na idadi ya maneno katika mistari. Umbo hili hutofautisha shairi na tenzi. Kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufahamika kuhusu shairi, nayo ni:
Beti – Kifungu kimoja cha shairi ambacho kina uzani sawa.
Vina – Ni mwisho wa mistari ambayo huwa na silabi zenye sauti ileile mwishoni mwa sentensi.
Mizani – Ni idadi zilizo sawa za silabi katika kila mstari, ubeti hadi ubeti.
Kituo – Huu ni mstari wa mwisho wa ubeti. Kuna vituo za aina tatu:Kituo cha bahari – ni mstari unaotoka mwanzo hadi mwisho bila kubadilika katika kila ubeti;Kituo cha kimalizio – ni kituo ambacho mstari wa mwisho maneno yake hubadilika ubeti hadi ubeti;Kituo nusu bahari – ni mstari wa mwisho ambao maneno yake nusu hubadilika na nusu hubaki kama ulivyo ubeti hadi ubeti.
Katika mashairi (ya kimapokeo), kila mstari lazima uwe umekamilika na ubeti uwe na maana kamili.
Vipengele za fani katika mashairi Vipengele za fani katika shairi ni pamoja na:
Jina / anwani
Mandhari
Wahusika
Muundo –tathnia, tathlitha, tarbia, tathamisa, sabilia n.k
Mtindo – pindu, msisitizo, beti kubadilishana vina, kurudiwa kipande kizima cha mstari wa mwisho kikiwa ni chanzo cha ubeti unaofuatia.
Vipengele za Maudhui kati mashairi Vipengele za maudhui ni pamoja na: migogoro, ujumbe, falsafa, msimamo, mtazamo, na dhamira za mwandishi.Matumizi ya ushairi ni pamoja na: kuomboleza, kubembeleza, kuliwaza, kufundisha, kuburudisha, kukosoa, na kadharika.
Baada ya hapa sasa unaweza kuanza kutunga shairi lako la kwanza.
Kuigiza Ngonjera
Katika kuigiza ngonjera muigizaji hana budi kuzingatia fani yenye kanuni zifuatazo; mtindo wa mashairi ya kimapokeo, muundo wa mashairi ya kimapokeo wenye mizani, vina, vipande, mishororo na beti, kuteua mandhari kutegemeana na mada, kuwepo kwa wahusika wawili au zaidi au makundi mawili au zaidi na matumizi ya lugha ya kishairi.
Maigizo ni tendo la kuiga sura, tabia, matendo na mazungumzo ya watu au viumbe wengine yaani kuiga jinsi walivyoumbwa, wanavyotembea, wanavyovaa, wanavyosema n.
Hatua za kutunga maigizo Kuchagua wazo, tendo, visa au tukio la kuigizwa:Ni lazima jambo hilo liwe na uzito, umuhimu au athari fulani katika jamii. Matukio hubainika kutokana na utafiti. Matukio yanayoweza kuwa kiini cha kutungiwa maigizo ni kama vile matumizi mabaya ya simu za mkononi, mitindo ya mavazi, madhara ya uganga wa kienyeji, madhara ya UKIMWI n.k.
Kutunga maelezo kuhusu mandhari:Maumbile ya wahusika na vitendo zao, ni muhimu kuelezwa katika mabano.
Kuandika maigizo na kuhariri:Ni muhimu kutumia lugha ya kimazungumzo inayovutia, yenye kuleta taharuki na yenye utamu unaoeleza maadili kwa mnato.
|