KATEGORIA ZA KILEKSIKA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Sarufi na Utumizi wa lugha (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=9) +--- Thread: KATEGORIA ZA KILEKSIKA (/showthread.php?tid=316) |
KATEGORIA ZA KILEKSIKA - MwlMaeda - 06-27-2021 Kategoria ya kileksika ndilo kundi la kwanza la kisemantiki ambapo vitu vyote vilivyo katika ulimwengu, vinavyoonekana na visivyoonekana hupewa majina ya kidhahania kimakundi. Makundi hayo si ya ubia bali hutegemea jamii-lugha, utamaduni wao na mazingira yao. Uainishaji wa vitu kimakundi hutokea bila kufahamu, kufikiri au kupanga. Hali ya ufahamu hutokea panapozuka utata.
Rosch (1975) anaziita kategoria hizi za kisemantiki kategoria tambuzi. Kategoria hizi hupangwa na watumiaji wa lugha kutegemea tajiriba zao, imani na mazoea ya jamii au kundi fulani la kijamii, na jinsi wanavyouona ulimwengu wao bila shaka itadhihirika kutokana na kategoria tofauti tofauti za kisemantiki. Kila kategoria huwa na kielelezo chenye sifa mahususi, na chochote kinachokiuka sifa za kundi hubainika kimaelezo na kuwekwa katika kundi lingine.
Kwa mfano, kasuku anaweza kutumika kama kielelezo cha ndege ilhali popo ambaye ana sifa za ndege vilevile hutofautishwa na ndege kwa vile baadhi ya sifa zake ni tofauti na zile za ndege wengine.
Mbinu nyingine ya uainishaji ni ile iliyotumiwa na Voegelin (2006) na inazigawa kategoria za kisemantiki kwa matapo manne. Matapo hayo ni pamoja na 1) sura ya nchi pamoja na vitu na viumbe vilivyomo, 2) tabia na shughuli za watu, 3) shughuli za kiakili pamoja na hisia, jazba na maadili na, 4) watu na mahusiano kati yao. Katika kujumlisha matapo haya ya kusemantiki, Voegelin (Aprili 2006) katika makala ya AIATSIS anayaita makundi ya kisemantiki ambayo ni pamoja na nomino, vivumishi, vitenzi, na mengineyo anuwai yanayotoa maana msingi za dhana mbalimbali. Kategoria za kisemantiki zimerejelewa kama kategoria za kisintaksia na na kisemantiki na Bennet (2000).
Mbinu nyingine inayotumiwa kuainisha kategoria za kileksika ni ile inayoyagawa maneno ya lugha kwa makundi mawili makuu. Makundi hayo ni maneno makuu na maneno ya kimatumizi. Kundi la kwanza lina maneno mengi mno, na kila neno huwa na sura mbalimbali kutegemea jinsi linavyobainika kiuamilifu katika tungo.
Sura hizo zinatokana na uambishaji wa maneno hayo. Kundi la pili lina maneno machache, na maneno hayo huwa hayabadilikibadiliki (Crystal, 2003).
Maneno katika lugha hugawanywa katika sehemu mbalimbali kutegemea matumizi yayo katika upatanisho wa kisarufi.
Migao hiyo ndiyo huitwa aina za maneno. Kila lugha ina maneno mengi yanayotumika katika mawasiliano ya kawaida na yale yanayotumika katika miktadha na taaluma maalum, na uianishaji huo hutegemea maana au semantiki, maumbo ya maneno hayo au mofolojia yao pamoja na uamilifu wa maneno hayo kwenye tungo, (Kapinga, 1983; Mgullu, 1999). Nyanja za kileksika ndizo huorodheshwa kwenye makamusi ya lugha na maana za kila neno kuelezewa. Pamoja na maana msingi ya neno, matumizi yake pia huelezwa pamoja na jinsi neno hilo hubainika kimatumizi. Kando na matumizi yake, maneno huelezwa kama ni ya umoja au wingi, miktadha yanamotumika pamoja na makundi yao. Katika ufundishaji wa sarufi, maana msingi za maneno husisitizwa pamoja na taratibu za upanganji wa maneno hayo kenye tungo ili maana ziweze kufasiriwa kwa urahisi.
Kategoria za kileskika zimeelezwa kama aina za maneno katika lugha za Kiswahili na Ekegusii (Whiteley, 1956 ; Massamba na wenzake, 1999 ; Habwe na Karanja 2004). Katika lugha ya Kiswahili maneno yameainishwa kwa makundi manane makuu ambayo ni nomino, viwakilishi, vivumishi, vitenzi, vielezi, viunganishi, vihusishi na vihisishi. Majina ya makundi hayo yanatokana na uamilifu wayo katika sintaksia. Katika lugha ya Ekegusii makundi yaliyotambuliwa na Whiteley (1956) ni pamoja na nomino, viwakilishi, vivumishi, vitenzi, vielezi, viunganishi, vihusishi na vihisishi. Taratibu hizi za uainishaji wa maneno katika lugha hizi mbili unaelekea kushabihiana kwa sababu lugha hizi zote ni za Kibantu na muundo wake wa kisintaksia unashabihiana sana.
Utafiti huu utachunguza kategoria mbili za kileksika ambazo ni nomino na vitenzi. Nomino ni maneno yanayotajia vitu, watu, hali na mahali. Kuna aina mbalimbali za nomino, (Mgullu, 1999 ; Habwe na Karanja 2004). Katika lugha za Kiswahili na Ekegusii, nomino zina mshabaha mkubwa kimaana na kiothografia, hasa ikizingatiwa kuwa hizi zote ni lugha za Kibantu.
Mifano ya nomino ni :
Kiswahili Ekegusii
Mtu Omonto
Nyumba enyomba
Utamu obwansu
Kuku engoko
Maji amache
Munyu omonyo
Maneno haya yana maana mahususi zinazoeleweka yanapoelezwa bila miktadha ya kimazungumzo. Tofauti na maana msingi za maneno haya, neno linapowekwa kwenye muktadha kimazungumzo linapata maana nyingine, kwa mfano:
3. Mainye n’achete enyomba yaye. Mainye anaipenda nyumba yake. Kando na maana msingi ya nyumba, nomino hiyo inapata maana nyingine ambayo inadhihirika kiusemi kwamba: Mainye anaipenda familia yake Mazungumzo yanaliwezesha neno ‘nyumba’ kusimba maana nyingine tofauti na uwazi na hivyo kuzua umaanisho wa familia.
Vitenzi ni maneno yanayoeleza mambo yanayotendeka. Massamba (2004) anaeleza kitenzi kama ‘Kipashio kinachotoa taarifa kuhusu tendo linalofanyika, lililofanyika au litakalofanyika.’ Lugha zote zina maneno ya kutajia vitendo. Lugha za Kiswahili na Ekegusii zina vitenzi vingi ambavyo hubainisha mlingano wa kimuundo.
Mifano ya vitenzi katika lugha hizi ni:
Kiswahili Ekegusii
Amka booka
Funga sieka
Toka sooka
Angalia rigereria
Lala raara
Maana msingi za vitenzi hivi katika lugha hizi ni mahususi. Hata hivyo, kimazungumzo vitenzi hivi huweza kupata maana nyingine tofauti na maana za kileksika, na maana hizo zinaweza kufikiwa na msikilizaji kwa kutumia mbinu ya ufaafu katika miktadha maalum, kwa mfano, mtu akisema;
4. Tom nere osieka
Tom ndiye alifunga
Uwazi wa kauli hii ni kwamba Tom ndiye alifunga (pengine mlango) lakini umaanisho wake katika mazungumzo ukawa unaelekea kwenye ile hali ya kuwa wa mwisho katika mashindano fulani. Washiriki wa mazungumzo haya ni lazima wawe katika hali sawa ya kimawazo ili kupata maana ya kile kilichomaanishwa ingawa hakikusemwa kwa kutumia mbinu za uhusiano.
|