SHAIRI: HIVI KWA NINI TWAVAA? - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: HIVI KWA NINI TWAVAA? (/showthread.php?tid=2875) |
SHAIRI: HIVI KWA NINI TWAVAA? - MwlMaeda - 12-19-2022 HIVI KWA NINI TWAVAA? Wasomi na wasomaji, tujadili hili jambo, Tusibaki waigaji, kukimbilia mikumbo, Lisilo na mfumbaji, la mavazi hili fumbo, Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Pengine twajivalia, kuona kama urembo, Vile tukishika njia, kuyaonesha maumbo, Tuanze kuwasumbua, wenzetu waende kombo, Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Wazazi wametwambia, nasaa zao ni wimbo, Hakuna wa kusikia, kuacha mambo ya ng'ambo, Viwalo twajitupia, Kwa wengine huwa fimbo, Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Fumbuka nakufumbua, mavazi hubeba nembo, Mvaaji akivaa, twajua ni mwendakombo, Vema akijivalia, tutasema hiki chombo, Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Mitindo tumeizua, kuweka wazi matumbo, Yatatoka kwenye pua, kuigaiga wa mombo, Laiti tungalijua, tungalivaa masombo, Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Mitindo ikiingia, twanata kama ulimbo, Bila ya kufikiria, thamani ya letu umbo, Hapo tunang'ang'ania, na kuleta majigambo, Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Uzungu watuzuzua, kwa mitumba yenye shombo, Jambo ninaloshangaa, hivi tumelewa tembo? Maungo kujiachia, wanzuki ama zarambo? Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Mtu aliyetimia, kichwa, mabega na tumbo, Akili akatumia, kung'amua haya mambo, Hawezi kuangukia, pasipo kuramba bambo, Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Siwezi kuendelea, nanga nakitia chombo, Jambo hilo shikilia, acha kuiga wamombo, Mbona wewe twakujua, umezaliwa Matombo? Dhima ya kwanza mwilini, yatusitiri mavazi. Mtunzi Filieda Sanga Mama B Mabibo Dsm 0753738704 |