ETIMOLOJIA YA MANENO ' RIZIKI' na 'ARZAKI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO ' RIZIKI' na 'ARZAKI' (/showthread.php?tid=2578) |
ETIMOLOJIA YA MANENO ' RIZIKI' na 'ARZAKI' - MwlMaeda - 05-24-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' RIZIKI' na 'ARZAKI' Neno *riziki* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: i-/zi-]* yenye maana zifuatazo: 1. Mahitaji ya msingi kama vile chakula anachopata mtu aghalabu baada ya kufanya kazi; malipo, ujira. 2. Baraka anazopata mtu katika maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; neema. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *riziki* limetokana na neno la Kiarabu *rizqun* (soma: *rizqun/rizqan/rizqin رزق* ) lenye maana zifuatazo: 1. Kila kinachomnufaisha mtu kama vile chakula na mavazi. 2. Kinacholiwa kikafika tumboni; kilichoruzukiwa, marzuuq مرزوق maruzuku. 3. Mvua, sababu ya kupatikana chakula. 4. Ujira anaolipwa mtu kwa kazi aliyoifanya; mshahara. 3. Upole na huruma. 4. Moyo wa huruma. 5. Anachoruzukiwa mtu na Mwenyezi Mungu. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *rizqun/rizqan/rizqin رزق*) lilipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *riziki* maana yake katika Kiarabu haikubadilika. Neno *arzaki* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: i-/zi-]* iliyo wingi wa neno riziki. Neno hili *arzaki* (soma: *arzaaqun/arzaaqan/arzaaqin ارزاق* ) katika lugha ya Kiarabu ni wingi wa neno 'rizqun' kama lilivyofafanuliwa hapo juu. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili *arzaaqun*(soma: *arzaaqun/arzaaqan/arzaaqin ارزاق*) lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *arzaki* maana yake katika lugha asili - Kiarabu haikubadilika. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |