YA KALE YA KUKUMBUKWA! UPAMBAUKAO HUTWA (KWAHERINI) - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi andishi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=7) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=54) +---- Thread: YA KALE YA KUKUMBUKWA! UPAMBAUKAO HUTWA (KWAHERINI) (/showthread.php?tid=2565) |
YA KALE YA KUKUMBUKWA! UPAMBAUKAO HUTWA (KWAHERINI) - MwlMaeda - 05-13-2022 YA KALE YA KUKUMBUKWA! UPAMBAUKAO HUTWA (KWAHERINI) 1. Upambaukao hutwa, na kutwapo huwa giza, Mtana hupetwa petwa, ukanyang'anywa mwangaza, *Yaliza haya yaliza!* 2. Na sisi ule mtana, uliotupambauza, Ulotupa kujuana, na mengi kuyafanyiza, Leo waanza kununa, mitima kuiumiza, *Laliza hili laliza!* 3. Hikumbuka tangamano, vyema tulivyolikuza, Mi nanyi 'kawa mfano, wa lulu katika chaza, Kisha leo saa hino, hiona twalikatiza, *Laniliza! Laniliza!* 4. Hikumbuka ukarimu, na wema wenu nduguza, Jinsi mulivyonikimu, myaka saba hatimiza, Nahisi najidhulumu, Tanzania kuipeza, *Ndipo hamba laniliza* 5. Ingawa menilazimu, na nyinyi kujiambaza, Yondokayo ni sehemu, sehemu najibakiza, Moyo wangu umo humu, Tanzania 'tausaza, *Japo hivyo laniliza!* 6. Ni yangu matumaini, kwenu nayapendekeza, Kwamba hwenda si jioni, nuru ingajipunguza, Pengine wingu angani, ndilo lilojitandaza, *Litakoma kutuliza?* 7. Na iwapo si hakika, hili nilowaambiza, Jambo moja liso shaka, tusoweza lipuuza, Utwao hupambauka, hauwezi ukaiza, *Hapo halitatuliza.* *ABDILATIF ABDALLA,* *S.L.P. 35110,* *DAR ES SALAAM.* *SEPTEMBA 8, 1979.* *NA KUCHAPO LITAKUCHWA* ( *KWA HERI YA KUONANA* ) 1. Na kuchapo litakuchwa, likafungamana giza, Na mchana ukaachwa, usiku ukajikweza, Asubuhi ikafichwa, jioni ikatokeza, *Yasikulize nyamaza.* 2. Nyamaza yasikulize, tuombeane Muweza, Mitima aitulize, mapenzi kutujaliza, Kwako kwetu atujaze, ya heri kutueneza, *Usijilize nyamaza.* 3. Pia nasi kwa mfano, kwako tukielekeza, Tuwazapo kongamano, kwenye yale mabaraza, Kwenye mbinu kwenye ngano, machozi watwambukiza, *Ndipo nasema nyamaza.* 4. Sisahau umuhimu, mengi umeniongoza, Hasa kwa ile sehemu, diwani nilimaliza, Ya mwenzetu marehemu, *Nyamaume* kuikuza, *Nyamaza bwana nyamaza.* 5. Kilio hiki si chako, ni changu unaniliza, Na giza hili si lako, ni langu lanikwamiza, Mayonzi haya si yako, ni yangu yaniumiza, *Ukilia waniliza.* 6. Kwa heri sisemi nenda, na siwezi kukataza, Wendapo naona inda, nagubikizwa na kiza, Nina nyang'anywa uwanda, uga gani nitacheza, *Hapo kulia nyamaza.* 7. Wendako usisahau, nyuma kututumbuiza, Kwa salamu angalau, heba ukatuliwaza, Wemao hatusahau, buriani nanyamaza, *Wacha kulia nyamaza.* *SHAABAN C. GONGA,* *S.L.P. 9031,* *DAR ES SALAAM.* *09 - 09 - 1979.* *USHAIRI HARIJOJO?* 1. Kwa isimuye Rabana, Muumba na Muumbule, Aliyeumba mchana, usiku uufatile, Naomba kwake auna, nudhumu niipangile, *Wapi ushairi ule, umekwenda harijojo?* 2. Ushairi wa maana, tulorithi kwa wakale, Wenye mizani na vina, maudhui yatimile, Urari, lugha mwanana, Kiswahili kiso ndwele, *Wapi ushairi ule, umekwenda harijojo?* 3. Ushairi wenye taji, walotufunza wavyele, Ulosheheni umbuji, na hekima teletele, Si leo wa mfa maji, anayepiga kelele, *Wapi ushairi ule, umekwenda harijojo?* 4. Beti nne kaditama, ukomo niufikile, Mtima unaniuma, pingiti nizionile, Zimetanda zinavuma, ni shangwe vigelegele! *Wapi ushairi ule, umekwenda harijojo?* *KHAMIS S.M. MATAKA,* *S.L.P 70249,* *DAR ES SALAAM.* *18 - 09 - 2003.* |