ETIMOLOJIA YA NENO 'ANSARI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'ANSARI' (/showthread.php?tid=2524) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'ANSARI' - MwlMaeda - 04-22-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'ANSARI' Neno ansari katika lugha ya Kiswahili ni Nomino [Ngeli: a-/wa-] yenye maana zifuatazo: 1. Wakazi wa mji wa Yathribu (sasa Al-Madiinatu Al-Munawwarah/Madina) waliwapokea Muhajirina (Waislamu waliouhama mji wa Makkah) na Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na wakawanusuru na kumuunga mkono Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) dhidi ya maadui zake Maqureishi Washirikina wa Makkah. 2. Kundi la watu wanaoenzi na kunusuru matendo aliyoyafanya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). Ansari Sunna; Wafuasi wa matendo ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). 3. Waokoaji. Katika lugha ya Kiarabu neno ansari linatokana na neno la Kiarabu answaaru (soma: answaarun/answaaran/answaarin أنصار) lililo wingi wa neno naaswirun ناصر lenye maana zifuatazo: 1. Al-Answaaru; watu wa mji wa Yathribu (sasa: Madina) waliomhami Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kutokana na maadui zake wa mji wa Makkah na wengineo. 2. AN-NAASWIRU الناصر, Mwenye kunusuru, moja ya majina matukufu ya Mwenyeezi Mungu. 3. Naswiirun ناصر, jina la mwezi wa 6 (Juni) kwa Kalenda ya nchi ya Libya. Kinachodhihiri ni kuwa neno answaarun انصار lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno ansari maana yake katika lugha ya asili - Kiarabu inayohusu watu wa Madina na watu wenye kunusuru; waokoaji haikubalika. TANBIHI: Mambo yafuatayo ni ya kuzingatiwa: 1. Ansari ni wanaoenzi, kunusuru na kufuata Sunna (mambo yote yaliyohusishwa na Mtume Muhammad - Allaah Amrehemu na Ampe Amani - iwe kauli yake, kitendo chake au lile alilolikubali lilipofanywa mbele yake) na sio matendo yake tu. 2. Katika kujipambanua, Libya chini ya Kiongozi wake wa zamani Marehemu Muammar Gaddafi, ilibuni na kuanzisha majina ya miezi tofauti na wengine na wakati mwaka wa Kalenda ya Ulimwengu wa Kiislamu unaanzia toka kuhama kwa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kutoka Makkah na kuhamia Madina, Libya ilihesabu Kalenda yake toka kutawafu kwa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). 3. Jina Naaswirus Sunnah, mwenye kunusuru Sunnah au Answaarus Sunnah, wenye kunusuru Sunna ni jina kongwe walilojinasibisha nalo baadhi ya Wanazuoni wa Kiislamu wa Karne nyingi zilizopita. Jina hili lilipata umashuhuri zaidi lilipotumiwa na wafuasi wa Mwanazuoni Sheikh Muhammad Abdul-Wahabi (Allaah Amrehemu) katika kinachoitwa mwamko mpya wa Uislamu. Wafuasi hawa wametambulika kwa majina mengi kama vile: Mawahabi (jina linalotumiwa sana na wapinzani wao), Masalafi, Ahlus Sunnati Waljamaa, Salafi Jadiid na mengineyo. Shukran sana. Khamis S.M. Mataka. |