ETIMOLOJIA YA MANENO 'WAKALA' NA 'WAKILI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO 'WAKALA' NA 'WAKILI' (/showthread.php?tid=2502) |
ETIMOLOJIA YA MANENO 'WAKALA' NA 'WAKILI' - MwlMaeda - 04-07-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'WAKALA' NA 'WAKILI' Neno *wakala* katika lugha ya Kiswahili ni *Nomino [Ngeli: a-/wa-]* yenye maana mtu anayefanya kazi kwa niaba ya asasi, shirika au serikali katika utekelezaji wa majukumu yake; mwakilishi. Neno *wakala* limechukuliwa kutoka neno la Kiarabu *wakaalatun/wikaalatun* *(soma: wakaalatun/wakaalatan/wakaalatin وكالة)* lenye maana zifuatazo: 1. Kazi ya uwakili, ofisi ya wakili. 2. Mapatano ya mtu kufanya kazi fulani kwa niaba ya mwengine. 3. Shirika linalojishughulisha na aina mbalimbali za biashara. Neno *wakili* katika lugha ya Kiswahili ni *Nomino [Ngeli: a-/wa-]* yenye maana zifuatazo: 1. Mtaalamu wa sheria ambaye hutetea mtu, kampuni au serikali kwenye kesi mahakamani; mwanasheria, mtetezi. 2. Msimamizi wa kazi au shughuli za mtu mwengine; *dalali* . 3. Mtetezi wa wenye dhambi mbele ya Mungu. Neno hili *wakili* ( *soma: wakiilun/wakiilan/wakiilin وكيل)* ni nomino ya Kiarabu yenye maana zifuatazo: 1. Moja ya Majina Mazuri ya Mwenyeezi Mungu *ALWAKIILU الوكيل* lenye maana ya Mdhamini wa riziki za viumbe na Mlinzi wao. 2. Anayefanya kazi fulani kwa niaba ya mwengine. Kwa Waarabu neno hili hutumika kwa jinsia zote na kwa umoja na wingi, *hum wakiilun, wao ~, hiya wakiilun, yeye (mwanamke) ~.* 3. Katibu Mkuu *wakiilul wizaarati وكيل الوزارة* katibu mkuu wa wizara. 4. Mtu mwenye sifa ya ujasiri. 5. Mdhamini. 6. Naibu. *wakiilul mudiir,* naibu mudiri/mkurugenzi/ mkuu وكيل المدير. 7. Mwanasheria mkuu, *wakiilul maliki* وكيل الملك. Kinachodhihiri ni kuwa neno *wakaalatun وكالة* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *wakala* halikubadili maana ya msingi katika Kiarabu wakati neno *wakiilun وكيل* lilipotoholewa na kuwa neno *wakili* lilibeba maana ya msingi ya kufanya kazi kwa niaba ya mwengine na ikalihusishwa neno hili na mwakilishi mtetezi mahakamani ambaye Waarabu wanamuita *muhaamin محام* kwa maana ya mtetezi. Waswahili wamelipa neno *wakili* maana mpya ya mtetezi wa wenye dhambi mbele ya Mungu ambaye kwa Kiarabu ni *shafiiun شفيع* sifa ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |