ETIMOLOJIA YA NENO 'BERKANE' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'BERKANE' (/showthread.php?tid=2457) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'BERKANE' - MwlMaeda - 03-15-2022 MAKALA MAALUMU KWA HISANI YA DKT. ATHUMANI S. PONERA. HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'BERKANE' Neno *berkane* ni zao la kuandika kwa herufi za Kilatini neno la Kiarabu *burkaanu بركان* lenye maana ya *volkano.* Hakuna katika makamusi ya zamani ya Kiarabu asili ya neno *burkaanu* kwa maana iliyo mashuhuri hivi sasa bali neno *burkaanu* lilijulikana kwa maana ya moto kama vile ' *burkaanu Al-Madinatu Al-Munawwarah*, moto uliotokea katika mji wa Madina (Saudi Arabia) mnamo Karne ya 7 AD. Baadhi ya Watafiti wa Historia ya Lugha ya Kiarabu wanadai kuwa neno hili liliingia katika Kiarabu zaidi ya miaka 1000 iliyopita. Watafiti wengine wanadai kuwa neno *burkaanu* ( *volkano*) limetoholewa kutoka neno la Kitaliano *vulcano* ambalo lina maana ya *mlima unaowaka moto* au kutoka neno la Kilatini *Vulcanus* ambalo ni jina la mungu wa moto wa Warumi. *Tanbihi:* Mlipuko wa volcano ni matokeo ya fukuto la joto kali katika matabaka ya miamba kwenye kina kirefu sana cha ardhi. Fukuto hilo la joto husababisha matabaka ya miamba kuyeyuka na kuwa katika hali ya uji-uji. Kutokana na nguvu za mgandamizo zinazosababishwa na kina cha miamba tabaka hilo la uji-uji (magma) husukumwa na kuelekea juu ambapo hurushwa juu ya uso wa ardhi *na hiyo ndiyo volkano (berkane)*. Tabaka hilo la uji-uji huwa lina mchanganyiko wa vitu vingi kutegemeana na kiasili cha miamba iliyohusika katika kuzalisha tabaka hilo. Hali kadhalika, linaweza likasababisha kutiririka kwa lava, au kurushwa hewani kwa majivu ya miamba iliyoungua, na vipande vya miamba ambapo huambatana na gesi zenye sumu au kutokea vyote kwa pamoja. *Muhimu:* Ni ukweli kuwa utokeaji wa *volkano (berkane)* hutegemea mazingira kuntu wezeshi si mazingira ya Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, nchini Tanzania. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |