SHAIRI: NITARUDI MLIMANI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: SHAIRI: NITARUDI MLIMANI (/showthread.php?tid=2420) |
SHAIRI: NITARUDI MLIMANI - MwlMaeda - 03-02-2022 NITARUDI MLIMANI Haka kaelimu kangu, mwenyewe ninajicheka, Nikitazama wenzangu, vyeti wamevitundika, Kilivyochoka Cha kwangu, kacheti kamoja haka, Nitarudi Mlimani, nikaongeze elimu. Niwe kama Mutembei, Kahigi na Mulokozi, Na niwe chini sikai, kila siku nina kazi, Jama nasema walai,nami nitaanza kozi, Nitarudi Mlimani, nikaongeze elimu. Hata nitokwe kipara, utosi nywele hakuna, Nizeeke yangu sura, Kitabu kunitafuna, Sitabadili fikira, niseme shule hapana, Nitarudi Mlimani, nikaongeze elimu. Nikifika Mlimani, nisipelekwe Coet, TATAKI nirudisheni, sizitaki Hisabati, Isimu nambari wani, niivae kama koti, Nitarudi Mlimani, nikaongeze elimu. Na siku nikifariki, ukawachoshe wasifu, Kisomwe kile na hiki, nichofanya mtawafu, Akishamaliza hiki, aseme tena halafu, Nitarudi Mlimani, nikaongeze elimu. Sikubali kuridhika, hata nitokwe mkia, Wenzangu wakanicheka, 'jione una mkia', Haitoshi kuridhika, shule nikaikimbia, Nitarudi Mlimani, nikaongeze elimu. Kutangaza ninasita, msije mkaniroga, Nianze kiwa zezeta, akili kunikoroga, Yakanikuta matata, kichwa kigeuke boga, Nitarudi Mlimani, nikaongeze elimu. Sanga Sasa nanyamaza, nitaonesha vitendo, Moyo unanikataza, kusema maneno lundo, Haya nilowaeleza, sitabadili mkondo, Nitarudi Mlimani, nikaongeze elimu. Mtunzi Filieda Sanga Mama B Mabibo Dsm 0753738704 |