ETIMOLOJIA YA NENO 'AKIDI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'AKIDI' (/showthread.php?tid=2405) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'AKIDI' - MwlMaeda - 02-20-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'AKIDI' Neno akidi katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. Nomino [Ngeli: i-/zi-] makubaliano rasmi ya kuishi pamoja kama mume na mke; akdi; tendo la kufunga ndoa. Nahau : Funga akidi: kamilisha ndoa. 2. Nomino [Ngeli: i-/zi-] idadi maalumu ya wajumbe inayoruhusu mkutano kufanyika na uamuzi kuweza kutolewa katika vikao. 3. Nomino [Ngeli: i-/i-] uchache wa watu au vitu. 4. Kitenzi elekezi chenye maana ya: (i) fikia kiwango kinachohitajika; tosha. (ii) hitimisha jambo au shughuli fulani; kamilisha jambo. Kisawe: maliza. Minyumbuliko: akidia, akidika, akidiwa, akidiana, akidisha. 5. Kitenzi elekezi: akid.i nakili andiko la mtu au saini kwa lengo la kufanya udanganyifu; ghushi. Visawe: ghilibu, iga, zuga. Minyumbuliko: akidia, akidika, akidiwa, akidiana, akidisha. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili akidi( soma: aqdun/aqdan/aqdin عقد ) ni nomino ya Kiarabu yenye maana zifuatazo: 1. Tendo-jina masw-dar مصدر linalotokana na kitenzi cha Kiarabu aqada عقد chenye maana ya: (i) amefunga mfano kamba au fundo (ii) ameingia katika makubaliano fulani.(iii) amedhamini (iv) amefanya mahesabu. (v) ameyafunga maua pamoja. (vi) amemkwamisha kwa kumuuliza maswali magumu. (vii) ameghadhibika na kuwa tayari kwa shari yoyote. (viii) amemkalifisha mwengine majukumu fulani. 2. Makubaliano ya pande mbili yanayoulazimisha kwa muktadha wake kila upande kutekeleza walichokubaliana, kama vile makubaliano ya biashara, ndoa na kadhalika. 3. Mkataba wa kazi. Kwa mujibu wa Uchumi wa Kisiasa ni makubaliano yanayomlazimisha mtu, kwa mujibu wake, kumtumikia mwajiri wake kwa kulipwa malipo maalumu. 4. Makumi: hesabu ya kumi, ishirini, thelathini....hadi tisini. 5. Tamko linaloashiria kufanya jambo fulani, mathalani: zawwajtuka زوجتك nimekuozesha, bi-ituka بعتك nimekuuzia. Kinachodhihiri ni kuwa neno aqdun/aqdan/aqdin عقد lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno akidi/akdi maana yake katika lugha ya asili - Kiarabu haikubadilika bali Waswahili walichukua baadhi ya maana zake katika Kiarabu na kuziacha nyingine, kama ambavyo walilipa neno hili maana mpya ya idadi maalumu ya wajumbe inayoruhusu mkutano kufanyika na uamuzi kuweza kutolewa katika vikao na zile maana za vitenzi elekezi. Shukran sana. Khamis S.M. Mataka. |