ETIMOLOJIA YA MANENO 'AKARABU/AKRABU' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO 'AKARABU/AKRABU' (/showthread.php?tid=2387) |
ETIMOLOJIA YA MANENO 'AKARABU/AKRABU' - MwlMaeda - 02-04-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'AKARABU/AKRABU' Neno akarabu hutamkwa pia akrabu katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. Nomino [Ngeli: i-/zi-] mshale katika uso wa saa unaoonyesha ama saa, dakika au sekunde. 2. Nomino [Ngeli: i-/zi-] mshale unaoonyesha uzito katika mizani. 3. Nomino [Ngeli: i-/zi-] mshale unaoonyesha upande fulani katika uso wa dira. Msemo: Akarabu/Akrabu Kaskazini: Upande wa Kaskazini. 4. Nomino [Ngeli: i-/i-] mkusanyiko wa nyota unaofanya umbo la nge angani. 5. Nomino [Ngeli: i-/i-] alama ya nge katika mfumo wa unajimu wa kutumia nyota. Katika lugha ya Kiarabu, neno akarabu/akrabu limekopwa kutoka nomino ya Kiarabu aqarabun/aqaraban/aqarabin عقرب yenye maana zifuatazo: 1. Mdudu mdogo mwenye sumu nyingi anayechoma kwa mwiba wa sumu ulio katika ncha ya mkia wake. 2. Moja ya nyota zilizo angani iliyo kati ya nyota za Mizani na Mshale na wakati wake unaanzia tarehe 24 Oktoba hadi tarehe 21 Novemba. 3. Aina ya samaki mwenye kichwa kikubwa ambaye hupatikana katika Bahari ya Kati (Bahari ya Mediteranea). 4. Mikanda ya viatu aina ya Kandambili. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili aqarabun/aqaraban/aqarabin عقرب ) lilipokopwa na kutoholewa kuwa neno akarabu/akrabu lilichukua baadhi ya maana za lugha ya asili - Kiarabu na kuacha maana zingine na pia lilipata maana mpya ya upande Akarabu/Akrabu Kaskazini: Upande wa Kaskazini. Shukran sana. Khamis S.M. Mataka. |