ETIMOLOJIA YA MANENO 'HURU' NA 'AHIRARI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO 'HURU' NA 'AHIRARI' (/showthread.php?tid=2269) |
ETIMOLOJIA YA MANENO 'HURU' NA 'AHIRARI' - MwlMaeda - 01-21-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'HURU' NA 'AHIRARI' Neno huru katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. Nomino: [Ngeli: a-/-wa] yenye maana ya: mtumwa aliyeachiwa. 2. Nomino: Mwanamke mtawa, mcha- Mungu na mwenye tabia njema. 3. Kivumishi: -sio chin ya utawala wa nchi au mtu mwengine. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili huru( soma: hurrun/hurran/hurrin حر ) ni nomino ya Kiarabu yenye maana zifuatazo 1. Mtumwa aliyeachiwa. 2. Mtu mwenye uhuru wa kufanya mambo yake bila ya kuingiliwa au kudhibitiwa na mwengine. 3. Mwanamke aliyeachika; imra-atun hurratun امرأة حرة mwanamke huru. 4. Usiku wa kwanza wa mwezi mwandamo hurratush shahri حرة الشهر. 5. Changarawe zisizochanganyiwa na udongo/mchanga ramlatun hurratun رملة حرة. 6. Mvua nyingi, sahaabatun hurratun سحابة حرة *(mawingu huru). 7. Farasi asiyechanganya damu; farasun hurrun فرس حر. 8. Asali safi isiyochanganywa na sukari guru; asalun hurrun عسل حر. Neno ahirari katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. Nomino: [Ngeli: a-/-wa, wingi: maahirari] yenye maana ya: mtu aliyeachiliwa huru kutoka kifungoni. 2. Kitenzi elekezi: ahirar.i achilia huru aghalabu watu waliokuwa kifungoni au kizuizini; weka huru. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili ahirari( soma: ahraarun/ahraaran/ahraarin احرار ) ni nomino ya Kiarabu ikiwa ni wingi wa neno huru ( soma: hurrun/hurran/hurrin حر ). Kinachodhihiri ni kuwa neno hili huru ( soma: hurrun/hurran/hurrin حر ) lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa huru lilichukua kutoka lugha ya asili - Kiarabu maana ya mtumwa aliyeachiwa n a ikabuniwa maana mpya ya mwanamke mtawa, mcha-Mungu na mwenye tabia njema , wakati neno la Kiarabu ahraaru/ahraaran/ahraarin lililo wingi wa neno la Kiarabu hurrun/hurran/hurrin lilitoholewa kuwa neno la Kiswahili ahirari likiwa nomino iliyopewa maana mpya ya mtu aliyeachiliwa huru kutoka kifungoni na kitenzi elekezi chenye maana ya achilia huru aghalabu watu waliokuwa kifungoni au kizuizini; weka huru. Shukran sana. Khamis S.M. Mataka. |