CHIMBUKO LA VINA NA MIZANI KATIKA USHAIRI WA KISWAHILI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Chuo (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=3) +---- Forum: Shahada (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=20) +----- Forum: Maswali na majibu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=24) +----- Thread: CHIMBUKO LA VINA NA MIZANI KATIKA USHAIRI WA KISWAHILI (/showthread.php?tid=1986) |
CHIMBUKO LA VINA NA MIZANI KATIKA USHAIRI WA KISWAHILI - MwlMaeda - 01-04-2022 CHIMBUKO LA VINA NA MIZANI KATIKA USHAIRI WA KISWAHILI
Mazrui na Syambo (1992:43) wanadai kuwa utafiti katika fasihi ya Kiswahili unadhirisha ya kwamba ushairi umeanza na zile nyimbo za kale.…….. nyimbo hizi ni zile zilizokuwa zikiimbwa katika hafla mbalimbali: harusini, unyagoni, mavunoni, pungwani na kadhalika na inaonekana hazikuwa na utaratibu wa vina na mizani.
Sitaki kuchimba sana kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili kwani lengo ni kuchunguza na kubaini vina viliibukaje au vilitokea wapi mpaka kuwepo katika ushairi wa Kiswahili.
VINA NA MIZANI.
TUKI (2003:94) wanadai mizani ni jumla ya silabi zilizomo katika kila msitari wa ubeti. Wanaendelea kwa kusema, hizi ndizo zileatazo urari wa mapigo, kwani kila msitari watakiwa uwe na mizani sawa na mistari mingine (au wakati mwingine ule msitari uwe nusu ya mizani ya msitari mmoja).
Nao Mazrui na Syambo (1992:40) wanasema mizani ni hesabu au idadi ya silabi katika neno au katika kifungu cha maneno (kama mshororo wa ubeti).
Kabla ya kuchambua fasili hizo za mizani, ni vema tukaitizama pia dhana ya vina kisha tuvitazame kwa pamoja.
Mazrui na Syambo (1992:40) wanafasili vina kama sauti au silabi za aina moja zinazopatikana mwisho wa kipande au mwisho wa mshororo wa kila ubeti.
Aidha, kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TUKI (2004), kwa kuegemea katika nyanja ya fasihi, mizani ni idadi ya silabi katika msitari wa shairi na utenzi.
Kwa ujumla, vina ni ufanano wa silabi za sauti za mwisho wa kila msitari (mshororo) wa ubeti wa shairi au utenzi (utendi). Ufanano huu waweza kujitokeza katikati kwa maana katika kila kipande kwa shairi lenye vipande viwili au mwishoni au vyote kwa pamoja (yaani kati na mwisho).
Kwa mfano:
Kijana sina maisha, magenge yanishawishi,
Ukata taniuisha, tuibe ili kuishi,
Arobaini zikisha, kipigo mwisho kuishi,
Maisha haya ni kifo, kifo si kukata roho.
Katika ubeti huo, kina cha kati ni –sha na kina cha mwisho ni “-shi”; lakini kuna uwezekano shairi la vipande viwili likawa na vina mwishoni lakini lisiwe na vina katikati.
Mizani ni idadi ya silabi katika mshororo (msitari) wa shairi au utenzi. Idadi hiyo inaweza kuwa na ulinganifu au isiwe na ulinganifu kwa kila mshororo au ubeti kutegemeana na bahari husika.
Kwa mfano:
Alibino kauwawa,
Mwuwaji ana kiganja,
Maswali kaelemewa,
Adai kweli kachinja,
Uchunguzi wendelea.
Katika ubeti huo, kila mshororo (msitari) una mizani nane.
CHIMBUKO LA VINA NA MIZANI KATIKA USHAIRI
Mazrui na Syambo (1992:43), wakiitetea hoja yao kuwa ushairi umetokana na nyimbo, wanataja mambo makuu matatu yaliyopelekea kuibuka kwa mbinu ya vina na mizani katika ushairi wa Kiswahili; nayo ni: mdundo katika nyimbo, methali za Kiswahili na athari za kigeni. Baada ya kuyachambua mawazo yao nimebaini kuwa, mambo wanayoyataja kama sababu za kuzuka kwa vina na mizani ni mitazamo mitatu tofauti katika kujadili na kuchunguza chimbuko la mbinu hizi za utunzi, kwa kuwa wao hawathibitishi moja kwa moja kuwa zote zilipelekea, tuzitazame hoja hizo.
Mazrui na Syambo (1992:43) wanasema kuwa pole pole, manju wa Kiswahili, katika kujaribu kuongeza ladha katika nyimbo zao walianza kutumia mbinu za vina na baadaye mizani. Huo ukawa mwanzo wa elimu arudhi, (elimu ya kanuni na kawaida za ushairi zilianza kuwa na nguvu).
Nakubaliana na wataalamu hawa kwa kuwa ili wimbo usisimue ni sharti uwe na mdundo mzuri, kwa hivyo, katika uboreshaji wa mdundo, kuna uwezekano mkubwa kwamba manju walizidi kutia vionjo katika nyimbo kiasi cha kufikia kuweka vina na mizani, nyimbo zikanoga na msisimko ukashamiri na kwa hivyo ndio kikawa chanzo hasa cha vina na mizani katika ushairi wa Kiswahil.
Utanzu wa methali unaaminika kuwa ni mkongwe na yawezekana ndio ulioasisi matumizi ya mbinu za vina na mizani. Mazrui na Syambo (1992:43) wanatoa mifano mitatu ya methali ambazo zimezingatia mbinu hizi zote.
(1) Haraka haraka
Haina baraka.
(2) Haba na haba
Hujaza kibaba
Methali zote mbili zimezingatia mbinu ya vina kwa kuwa silabi za mwisho katika methali (1) zinafanana, zote ni “ka” na katika methali (2) kuna ufanano wa silabi “ba” inayojitokeza katika kila msitari.
Hali kadhalika, katika methali (1) kuna ulinganifu wa idadi ya silabi katika kila msitari (mizani) kama inavyodhihirika hapa chini.
(1) Ha-ra-ka ha-ra-ka (mizani sita)
Ha-i-na ba-ra-ka. (mizani sita).
Kutokana na uhalisia wa baadhi ya methali kutumia mbinu hizi, na kwa ukweli kwamba methali zimekuwepo siku nyingi; kuna uwezekano mkubwa kwamba washairi walioanza kutumia vina na mizani waliathiriwa na tabia ya baadhi ya methali kwa kuwa methali pia zina mchango mkubwa katika suala la maudhui na na kuchopekwa kama zilivyo katika mashairi mbalimbali.
Hii inaelezwa kuwa sababu nyingine iliyoleta vina na mizani katika ushairi wa Kiswahili. Wageni hawa hasa Waajemi na Waarabu walipokuja (kuhamia) mwambao wa Afrika ya Mashariki waliathiri utunzi wa ushairi wa Kiswahili kwa kuwa wao walianza kutunga mashairi yaliyokuwa na arudhi na miundo yao waliyokuja nayo. Mazrui na Syambo (1992) wao wanawataja baadhi ya watunzi waliotunga mashairi yaliyokuwa na vina na mizani hapo zamani. Nao ni Fumo Liyongo ambaye mashairi yake yaliimbwa katika ngoma za “gungu” na ‘kisarambe”. Kadhalika alitunga mashairinmengine mengi tu ya tumbuizo na ukawafi.
Mwingine ni Aidarusi, huyu alipata kuishi karne ya 17; Aidarus alitafsiri wasifu wa Mtume Muhammad uliokuwa umeandikwa kwa lugha ya Kiarabu (yeye aliutafsiri kwa mfumo wa ushairi). Inadaiwa kuwa tafsiri hii ilitumia Kiswahili cha kale sana, nayo iliitwa, Hamziya.
Mnamo karne ya 18, uliibuka utenzi au utendi, utenzi huu ulikuwa na vina na mizani; miongoni mwa tenzi (tendi) za kale ni Chuo cha Utendi au Utendi wa Tambuka, au Utendi wa Herekali uliotungwa na Bwana Mwengo wa Athumani; utenzi huu unasimulia vita vilivyotokea baina ya majeshi ya Mtume Muhammad na yale ya mfalme Herakliosi wa Wayunani.
Utenzi mwingine ni ule uliotungwa na mtoto na mrithi wa Bwana Mwengo wa Athumani, huyu aliitwa Bakari wa Mwengo, nazo ni Utenzi wa Katirifu na Utenzi wa Mwana Fatuma.
Utenzi wa Inkishafi wa Sayyid Abdalla ni utenzi mwingine uliopata kutungwa ukizingatia vina na mizani.
Washairi waliotajwa wote ni wakazi wa sehemu ya Pate na ushairi wao ulikuwa na vina na mizani.
Nako Lamu kulikuwa na watunzi kama Zahindi Mgumi, Muhammad al- Lami, Mwenye Shehe Ali na Mtunzi wa Kike Saada (kwa uchache). Hawa, utunzi wao ulichochewa na na vita baina ya Mombasa na Lamu na Oman hali iliyopelekea kutungwa kwa mashairi ya Kisiasa.
Inasemekana kuwa Lamu iliathiri maeneo mengine jirani ikiwemo Pemba, Unguja, Mombasa, Tanga na kusambaa zaidi katika maeneo mengine.
Watunzi wote wa wakati huo waliathiriwa na utunzi wa Kiarabu ulioenea hasa kupitia dini ya Uislamu na hivyo washairi wa ushairi wa Kiswahili wakaanza kutumia kawaida za wageni hawa ikiwemo vina na mizani.
Athari nyingine ni ile ya ujio wa wakoloni wa Kiingereza ambao waliathiri utamaduni wetu, miongoni mwa athari zake kuhama kwa hati ya maandishi kutoka hati ya Kiarabu kwenda hati ya Kilatini. “Cheche” za ukoloni ziliposhamiri, washairi wa Kiswahili kama Shaaban Robert na wengine kama Kaluta Amri Abeid, na Mathias Mnyampala (kwa uchache), walianza kutunga wakiutetea Uafrika huku wakiulaani ubaya wa ukoloni na mkoloni mwenyewe na wakati huu kulishakuwa na mwamko wa kujua kusoma na kuandika kwa mwafrika.
HITIMISHO
Kwa ushahidi wa wazi kabisa, chanzo cha ushairi ni mahitaji ya jamii kutumia lugha kwa ajili ya mawasiliano, kwa hivyo ni sahihi kuwa kwa vyovyote vile ushairi wa awali haukuwa na vina wala mizani bali maendeleo ndiyo yaliyoleta kaida hizi. Kwa hivyo, ushairi wa mwanzo haukuwa na vina na mizani bali kawaida hizo ziliibuka mbele ya safari ndefu ya ushairi wa Kiswahili kama ilivyoelezwa katika hoja za utetezi.
Bibliografia
Mazrui, A. M. na Syambo, B. K. (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers.
Mulokozi, M. M. na Sengo, T. S. Y. (2005). History of Kiswahili Poetry: A.D. 1000 – 2000. Dar es Salaam: Institute of Kiswahili Research, University of Dar es Salaam.
TUKI. (2003). Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili (III): Fasihi. Dar es Salaam: TUKI.
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
|