ETIMOLOJIA YA MANENO ' AFYA' 'AFUA' NA 'AFUWA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO ' AFYA' 'AFUA' NA 'AFUWA (/showthread.php?tid=1970) |
ETIMOLOJIA YA MANENO ' AFYA' 'AFUA' NA 'AFUWA - MwlMaeda - 01-03-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' AFYA' 'AFUA' NA 'AFUWA' Neno afya katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. Nomino: [Ngeli: -i/-zi] ukamilifu na usahihi wa utendaji wa viungo vyote vya mwili na akili na ustahifu wa kijamii sawa. Kuna methali: Afya ni bora kuliko mali. Kuna msemo : Buheri wa afya: Afya nzuri. 2. Kihisishi: Neno linaloonesha utayari wa watu katika kufanya jambo aghalabu hutumiwa na watoto. Mfano: Afya! Twendeni tukaangue mapera! 3. Neno linalotumiwa kumuombea uzima mtu aghalabu mtoto baada ya kupiga chafya. Kuna msemo: Kua mwanangu kama mgomba, mnazi unachelewa (unakawia). Katika lugha ya Kiarabu, neno hili afya (soma: aafiyatun/aafiyatan/aafiyatin عافية) ni nomino yenye maana zifuatazo: 1. Kinga; Tiba, Masdar (Tendo-Jina) kwa kitenzi cha Kiarabu aafaa عافى (amemkinga na shari/ubaya, amemtibia maradhi yake). 2. Siha/Swiha timilifu. 3. Wageni. 4. Watafutaji riziki (wanaadamu na wanyama). 5. Wafanyao wema, hisani. Neno afuwa[ Ngeli: i-/i-] katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana ya: 'hali ya kumsamehe mtu au kumwia radhi kutokana na kosa alilolitenda. Na neno afua katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. Nomino : [ Ngeli: i-/zi-] uamuzi unaoweza kufanywa; chaguo. 2. Kitenzi elekezi : Afu.a hali aghalabu ya Mwenyeezi Mungu kumwepusha mtu na madhara ambayo yangeweza kumpata. Mfano: Usihofu, Mwenyeezi Mungu atakupa afua. 3. Nomino: [ Ngeli: i-/i-] hiari au kudra ya Mwenyeezi Mungu aliyonayo kwa mja wake anapokabiliwa na hatari. Kuna msemo: Afua ni mbili, kufa au kupona. Katika lugha ya Kiarabu maneno ' afua ' na ' afuwa ' yametokana na neno la Kiarabu afwu عفو ( soma: afwun/afwan/afwin عفو) lenye maana zifuatazo: 1. Nomino : Msamaha/Kusamehe, Masdar Tendo-Jina la kitenzi cha Kiarabu afaa عفا (amesamehe). 2. Nomino : Msamaha; kuacha kuadhibu. 3. Nomino : Wema, tendo jema. 4. Nomino : Ziada, kilichozidi. 5. Nomino/Kivumishi: -enye ubora. 6. Nomino: Ardhi ambayo haijakanyagwa na wayo wowote. 7. Mtoto wa punda. Kinachodhihiri ni kuwa wakati maneno haya afya , afuwa na afua yalipoingia katika Kiswahili na kutoholewa mbali ya kuchukua sehemu ya maana za lugha asili - Kiarabu, yalibeba dhana nyingine katika Kiswahili. Shukran sana. Khamis S.M. Mataka. |