SHAIRI : ETI SIYE TULIKUWA, WASHENZI HAPO ZAMANI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : ETI SIYE TULIKUWA, WASHENZI HAPO ZAMANI (/showthread.php?tid=1947) |
SHAIRI : ETI SIYE TULIKUWA, WASHENZI HAPO ZAMANI - MwlMaeda - 01-03-2022 SHAIRI : ETI SIYE TULIKUWA, WASHENZI HAPO ZAMANI ************** Jameni ninaumia, sana ninahangaika, mno nikifikiria, imepita mingi miaka, tangu zama n’kisikia, n’kisoma wanoandika, eti siye tulikuwa, washenzi hapo zamani. **** Vitabu waliandika, Waasia na Wazungu, hata ndugu Wafirika, waliofundwa kizungu, ‘ti hatukuthamanika, mbele ya kuja Wazungu, eti siye tulikuwa , washenzi hapo zamani. ***** “Babu zetu walikuwa, wapo totoro gizani”, haya nilifundishiwa, karibu miaka sitini, ‘mi bado sijaelewa, na staki kwelewa hini, eti siye tulikuwa, washenzi hapo zamani !!? ***** Huku yote waliponda, eti ya kishenzi yetu, vyema tulivyoviunda, hawakuthamini katu, vya chuma tulipounda, waka’amba vina kutu, eti siye tulikuwa, washenzi hapo zamani. ***** Wajameni fikiria, tafakari n’nayowaza, Ziwa la Vikitoria, si li’kuwa Ziwa Nyanza? kila walichopitia, walikibatiza kwanza, eti siye tulikuwa, washenzi hapo zamani. ***** Mlima wa Eligoni, hauna la jadi jina? Wakenya nipulikeni, mnambie na maana, Babu wana jina gani, la mlima walinena? eti siye tulikuwa, washenzi hapo zamani. ***** Leo napata simanzi, kasumba walotutia, tukakubali ushenzi, hadi leo nawambia, tunalo soko mshenzi, na la kizungu sikia, eti siye tulikuwa, washenzi hapo zamani. ****^ Haya ya Nyerere mambo, kuusaili uzungu, kauliza hili jambo,la kasumba ya kizungu, vitu vyenye kubwa umbo, mwaviita vya kizungu, nzi mwenye kubwa umbo, hamusemi wa kizungu? ***** Ushenzi haswa yakini, na ma’na ye halisia, siye huo wa zamani, waliotupakazia, ni uno wa enzi hini, kasumba kukumbatia, yetu kutoyathamini, tukaona ya kishenzi, ********* Rwaka rwa Kagarama,,( Mshairi Mnyarwanda) Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare, R W A N D A.. |