SHAIRI : TANZANIA, MAMA’NGU WA KAMBO MWEMA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : TANZANIA, MAMA’NGU WA KAMBO MWEMA (/showthread.php?tid=1942) |
SHAIRI : TANZANIA, MAMA’NGU WA KAMBO MWEMA - MwlMaeda - 01-03-2022 TANZANIA, MAMA’NGU WA KAMBO MWEMA ————————————————————– 1. Ipo dhana kwao wengi, ‘ti mama wa kambo mbaya, yananenwa mara nyingi, Ila si wote wabaya. Si dhana yenye msingi, kuwa ni kanuni haya, mama’ngu wa kambo mwema, anaitwa Tanzania. 2. Ni wasaa maalum, Qarima ‘menipatia, n’kiitumia nudhumu, nina kumsalimia. Asalaam aleikumu, heshima nakupatia, mama’ngu wa kambo mwema, Tanzania nipulike. 3. Nalipofunua mato, na akili kufungua, wa Kinyarwanda mtoto, nchi hini nalikua, n’kicheza nao watoto, mu vichaka vya maua, mama’ngu wa kambo mwema, alikuwa Tanzania. 4. N’kumbuka shule n’kienda, kalamu kwanza kushika, mchangani tukiunda, vimichoro kadhalika. Nyimbo somo tulipenda, na mistari kwandika, mama’ngu wa kambo mwema, si’sahau Tanzania. 5. Wendani nawakumbuka, huko darasa la kwanza, madogo wa Ubendeni, na Wakikuyu n’kiwaza, Pili wa Unyamwezini, na Nyagah ninawawaza, mama’ngu wa kambo mwema, jinale ni Tanzania. 6. Huko yali masikani, Warwanda yalihifadhi, wa MAUMAU yakini, Wakenya yakihifadhi. Eneo la Ubendeni, haja zetu yalikidhi, mama’ngu wa kambo mwema, Tanzania mkarimu. 7. “Binadamu wote sawa, Wafirika ndugu zangu” ni somo tulipatiwa, tuli makinda wenzangu. ni ya utu tuligewa, na tukifundwa undugu, mama’ngu wa kambo mwema, ni mlezi Tanzania. 8. Nchi mama n’kamkuta, nikiwa mtu mzima, kwa malezi nilopata, sasa natenda mazima, yangu nchi mama hata, yatambua yako mema, mama’ngu wa kambo mwema, ni jirani Tanzania. 9. Toka ndani ya mtima, nakutakia kwa dhati, fanaka na usalama, amani kulla wakati. Nina namuenzi jama, n’sema pasi masharti, mama’ngu wa kambo mwema, ni wa kheri Tanzania. 10. Jameni Watanzania, Mola awajalieni, ya umoja kuwania, undugu twendelezeni. Tuikuze njema nia, mikono tushikaneni, mama’ngu wa kambo mwema, Tanzania laazizi. 11. Tungo nimeshalijenga, kalamu chini naweka, n’shukuru kun’gea mwanga, Maulana Mtajika. Hisia zangu kutunga, mno nimefarijika, n’kikumbuka Tanzania, Mama’ngu wa kambo mwema. *** Rwaka rwa Kagarama, Mshairi Mnyarwanda. Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare, RWANDA. |