ETIMOLOJIA YA MANENO ' BAHATI' NA 'HADHI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO ' BAHATI' NA 'HADHI (/showthread.php?tid=1920) |
ETIMOLOJIA YA MANENO ' BAHATI' NA 'HADHI - MwlMaeda - 01-02-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' BAHATI' NA 'HADHI' Neno *bahati*[ *Ngeli: i-/zi-]* katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana ya' mafanikio yanayotokea kwa mtu bila ya kutarajia. *Kuna methali:* *Asiye na bahati habahatiki*: mtu ambaye hajapangiwa kupata bahati, hawezi kuipata. *Kuna msemo: Maisha ni bahati ifumbate*: jitahidi kufanya mambo ya maana maishani unapokuwa hai. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *bahati* (soma: *bakhtun/bakhtan/bakhtin بخت)* lina maana ya 'fursa anayoipata mtu bila ya kutarajia'. Kisawe cha neno ' *bahati* *(bakht)* katika lugha ya Kiarabu ni neno ' *hadhi* ' ( *soma: hadh-dhwun/hadh-dhwan/hadh-dhwin حظ*). Neno *hadhi*[ *Ngeli: i-/zi-]* katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana zifuatazo: 1. Ngazi au nafasi ya heshima aliyonayo mtu katika jamii, shirika au kazi. 2. Sifa ya kumfanya mtu aheshimike na ajiheshimu. 3. Hali ya maisha ya kiwango cha juu anayoishi mtu; maisha bora. Katika lugha ya Kiarabu neno 'hadhi' ( *soma: hadh-dhwun/hadh-dhwan/hadh-dhwin حظ)* lina maana zifuatazo: 1. Fursa, fungu. 2. Bahati. 3. Utukufu, ubora, hali njema. 4. Mwenye bahati/fursa *dhuu hadh-dhwi ذو حظ* Kinachodhihiri ni kuwa wakati neno *bahati* ( *soma: bakhtun/bakhtan/bakhtin بخت*) lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *bahati* maana yake katika lugha yake ya asili - Kiarabu haikubadilika, neno ' *hadhi* ' ( *soma: hadh-dhwun/hadh-dhwan/hadh-dhwin حظ)* ambalo ni kisawe cha neno ' *bahati* ' ( *soma: bakhtun/bakhtan/bakhtin بخت*) lilichukua dhana mpya. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |