ETIMOLOJIA YA NENO ' JAALA', 'JALIA' 'JALI.A/JAALI.A' na 'MAJALIWA' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO ' JAALA', 'JALIA' 'JALI.A/JAALI.A' na 'MAJALIWA' (/showthread.php?tid=1916) |
ETIMOLOJIA YA NENO ' JAALA', 'JALIA' 'JALI.A/JAALI.A' na 'MAJALIWA' - MwlMaeda - 01-01-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO ' JAALA', 'JALIA' 'JALI.A/JAALI.A' na 'MAJALIWA' Neno *jaala*[ *Ngeli: i-/i-]* katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana ya' mambo yafanyikayo kwa mapenzi/uwezo wa Mwenyezi Mungu'. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *jaala* (soma: *ja-a-la جعل)* ni kitenzi cha Kiarabu chenye maana zifuatazo: 1. Amefanya kitu fulani kiwepo. 2. Ametoa kitu kumpa mtu mwengine. 3. Ameanza jambo fulani. 4. (Kwa Mwenyeezi Mungu tu) Ameumba. 5. Ametengeneza. Neno *jalia*[ *Ngeli: a-]* katika lugha ya Kiswahili ni kisawe cha neno *jalali* [ *Ngeli: a-]* lenye maana ya 'jina la kumtaja Mwenyeezi Mungu kwa sifa yake ya kuwa utukufu mwingi'. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *jalali* (soma: *jalaalun/jalaalan/jalaalin جلال)* ni nomino ya Kiarabu yenye maana zifuatazo: 1. Utukufu. Mwenyeezi Mungu hutajwa kuwa *Dhul Jalaali* *ذو* *الجلال* mwenye utukufu. 2. -enye cheo/hadhi kubwa. 3. Kilicho kikubwa zaidi. Maneno *jali.a/jaali.a*[ *Vitenzi Elekezi* ] katika lugha ya Kiswahili vina maana ya 'fanya uwezekano, saidia, wezesha: Mwenyeezi Mungu *akitujalia/akitujaalia* uhai tutaonana. Neno hili linaponyambuliwa tunapata vitenzi: *jaalika, jaalisha na jaaliwa.* Neno *majaliwa*[ *Ngeli: ya-/ya-]* katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana ya' mambo yafanyikayo kwa uwezo/mapenzi ya Mwenyezi Mungu'. Maneno ' *jaala* ' na ' *majaliwa* ' ni visawe. Neno ' *majaliwa* ' halina mfano wake kimatamshi katika lugha ya Kiarabu bali yumkini limebuniwa kutokana na nomino ' *jaala* ' au kitenzi ' *jaalia/jaaliwa*'. Kitenzi ' *jali.a/jaali.a'* kinamhusu Mwenyeezi Mungu tu kwa maana ya kumpa mtu uwezo wa kupata au kuweza kufanya jambo fulani. Kinachodhihiri ni kuwa neno *jaala* ( *soma: ja-a-la جعل*) ambalo ni kitenzi katika lugha ya Kiarabu lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *jaala* limekuwa nomino kwa maana ya 'mambo yafanyikayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu'. Kiujumla, maneno yote haya hayakuepukana na maana zake katika lugha ya asili - Kiarabu. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |