UHAKIKI RIWAYA YA WATOTO WA MAMAN’TILIE - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Uhakiki wa kazi za fasihi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=78) +--- Thread: UHAKIKI RIWAYA YA WATOTO WA MAMAN’TILIE (/showthread.php?tid=1871) |
UHAKIKI RIWAYA YA WATOTO WA MAMAN’TILIE - MwlMaeda - 12-28-2021 UCHAMBUZI WA RIWAYA WATOTO WA MAMA NTILIE
MWANDISHI: EMMANUEL MBOGO
WACHAPISHAJI: HEKO PUBLISHERS
MWAKA: 2002
WASIFU WA MWANDISHI
Emmanuel Mbogo ni Profesa wa drama na fasihi na amehudumu katika vyuo vikuu mbalimbali ikiwemo, Chuo Kikuu cha Kenyatta Kenya na Chuo Kikuu Huria. Mbogo ni mwanafasihi mahiri sana katika Afrika ya Mashariki.
MUHTASARI WA RIWAYA
Maman’tilie, mama mwenye watoto wawili lakini wote wamefukuzwa shule kwa kukosa ada na sare. Anajitahidi hapa na pale ili apate, lakini wapi? Pesa imegeuka nyoka inateleza kwenye nyasi. Mumewe Mzee Lomolomo hana muda, yeye kila kukuchapo huelekea bunge la walevi kunywa pombe tani yake. Akiwa huko hunywa na kurudi nyumbani akiwa mbwii! Mwisho mwandishi anauliza swali gumu, ‘Nani anajali?’
UCHAMBUZI WA FANI NA MAUDHUI
MAUDHUI KATIKA RIWAYA YA WATOTO WA MAMAN’TILIE
Maudhui hujumuisha mawazo na pengine mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma mtunzi ama mwandishi wa kazi ya fasihi akaandika kazi yake.
DHAMIRA
Dhamira ni lile wazo linalomfanya mwandishi wa kazi ya fasihi aandike kazi yake. Katika riwaya hii, dhamira nyingi zimejadiliwa kama:
UMASIKINI
Dhamira hii imetawala katika riwaya. Asilimia kubwa ya wahusika ni watu wenye maisha ya dhiki na kazi za kijungujiko. Umasikini wao unadhihirishwa na mitaa wanayoishi kama: Manzese, Msufini, Tabata, Kisutu na Temeke. Maeneo haya ndiyo yaitwayo uswahilini leo hii.
Zita na Pita wanafukuzwa shule kwa sababu ya kukosa ada na sare (uk 1). Mamant’ilie naye anatumia maji ya mwarobaini kutibu homa yake kwa sababu hana pesa ya kununulia dawa za hospitali.
ULEVI
Unywaji wa pombe kupitiliza huweza kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji. Mzee Lomolomo ni mlevi mzoefu, kutokana na ulevi wake, anashindwa hata kuwalipia ada wanae ili waendelee na shule. Ni ulevi huohuo unamfanya aishi maisha ya dhiki huku akishindwa kutoa mchango kwa familia yake na taifa linalomtegemea. Mwisho Lomolomo anakufa kwa sababu ya pombe.
Mwandishi anasema, “… Lomolomo alikuwa lofa, mtu wa kazi za kijungujiko na vipesa vyake viliishia kwenye pombe…” (uk 7).
MALEZI YA WATOTO
Watoto wasipopata malezi yanayostahili kutoka kwa wazazi wote wawili huwa ni rahisi kwao kujiingiza katika mambo yasiyofaa.
Mwandishi anaonyesha aina tatu za watoto. Kwanza kuna Zita na Pita. Hawa wana wazazi wote wawili lakini baba hajishughulishi na malezi yao. Pia mama naye ametingwa na shughuli nyingi katika genge lake la uuzaji wa chakula. Zita na Pita hawana malezi ya kueleweka. Hali hii inamfanya Pita ajiingize katika biashara ya madawa ya kulevya.
Pili, kuna Dan na Musa hawa hawana baba, wanaishi na mama zao tu. Mama zao hawawajali wala kuwakemea kwa chochote kibaya wanachofanya. Dan anajiingiza katika ujambazi na kupoteza maisha. Musa anajiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya na kuishia jela.
Tatu kuna Kurwa na Doto. Hawa hawana wazazi kabisa. mwandishi anasema, “… walikuwa chokoraa namba moja, kupigana kulala na njaa, kukamatwa na polisi… yalikuwa sehemu ya maisha yao…”
Doto anajiingiza katika ujambazi, huko anauawa na mlinzi Simango.
RUSHWA
Rushwa imeota mizizi katika jamii. Kila uendako, kila upitako na kila utokako utaambiwa toa rushwa ili upate kitu fulani.
Mamant’ilie alishindwa kuyamudu maisha ya mjini kwa sababu ya rushwa aliyokuwa akiwapa askari wa jiji. Kwa kalamu yake isiyoisha wino, Mbogo anaandika, “Kodi na hongo kwa askari wa jiji, ziliikamua faida yake.” (uk 32).
MMOMONYOKO WA MAADILI NA KUKOSEKANA KWA UTU
Maadili ya siku hizi si yale ya zamani. Miaka inabadilika na vizazi navyo vinabadilika. Watu ni watu tu lakini hawana utu. Watoto wadogo sasa wanavuta sigara na kutafuna mirungi kama tumuonavyo Dan na Musa. Watu hawana moyo wa kusaidiana tena, wao wanaamini kuwa kila mwenye janga atalila peke yake. Zita anazidiwa na maradhi yaliyosababishwa na kuumwa na mbwa mwenye kichaa. Watu hawakumsaidia, badala yake walivishangilia vioja alivyovifanya. Mwandishi anatuonesha Zenabu akiwaomba msaada na kuwakalipia, “Nisaidieni, mnacheka nini? Wendawazimu wakubwa.” (uk 82).
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII
Nafasi ya mwanamke ni jumla ya matendo yote yafanywayo na mwanamke katika jamii yake. Mara nyingi huwa mabaya na yenye mtazamo hasi, lakini mara chache huwa mazuri yenye mtazamo chanya. Mwandishi wa riwaya hii, amemchora na kumjadili mwanamke kwa mawanda mapana kama inavyoelezwa:
UJUMBE
Ujumbe ni funzo litolewalo na kazi ya fasihi. Mafunzo mengi yametolewa katika riwaya hii:
MIGOGORO
Migogoro ni kukosekana kwa maelewano baina ya watu binafsi, jamii, taifa au mataifa. Migogoro iliyojitokeza ni:
Migogoro ya wahusika
Mgogoro wa nafsi
Migogoro mingine ni: migogoro ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
FALSAFA
Falsafa ni imani ya mwandishi. Emmanuel Mbogo anaamini kuwasaidia watoto kupata elimu yao kutaondoa matatizo yanayozuia ujenzi wa jamii mpya.
MTAZAMO/MSIMAMO
Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi. Anaamini kuwapatia watoto elimu na kusimamia malezi yao kutaliokoa taifa.
UCHAMBUZI WA FANI NA VIPENGELE VYAKE
Fani ni ule ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kazi yake. Fani ndiyo hutupatia kile kiitwacho maudhui. Katia riwaya hii, fani imechambuliwa kama ifuatavyo:
WAHUSIKA
Wahusika ni watu au viumbe waliokusudiwa uwakilisha tabia za watu katika kazi ya fasihi. Wahusika waliopo katika riwaya hii ni:
MATUMIZI YA LUGHA
Fasihi ni sanaa itoayo maudhui kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa au kuandiwa. Kipengele cha lugha ni muhimu kwani ndicho kinachotofautisha fasihi na sanaa zingine.
Lugha iliyotumika katika riwaya hii ni nyepesi na yenye kueleweka. Mwandishi ametumia vipengele vingi vipatikanavyo katika matumizi ya lugha kama: ucheshi na lugha ya picha, misemo na tamathali za semi.
TAMATHALI ZA SEMI
Tamathali za semi ni maneno au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi ama kusema. Wakati mwingine hutumiwa ili kupamba na kuongeza utamu wa kazi za fasihi. Mwandishi ametumia tamathali nyingi za semi kama:
“Bwee!”
“Paah!” (uk. 5)
“Masikio yamesimama wima kama anasisitiza kitu.” (uk. 2)
“Mdomo wake uliokaa kama bakuli la pombe.” (uk. 10)
“Akaenda haja ndogo.” (uk. 2)
“Akakitibu kidonda chake kwa maji ya chumvichumvi.” (uk 55)
“Yalaa! Yalaa!” (uk 2)
“Mjomba! Mjomba!”
“Shikamoo mama…” (uk 6)
“Una… una…” (uk 11)
“Maman’tilie alimtupia jicho bintie.”
“Mabega yameangalia juu.” (uk 10).
“Walikaa, wakala, wakanywa maji, wakamshukuru Mungu.”
“Naye pita aliitikia salamu hizo za ukarimu kwa kupiga chafya mbili au tatu.” (uk 19).
“Lomolomo uso wake uliopendeza kwa chang’aa…” (uk 70).
“Wakatembea mwendo wa farasi.” (uk 86).
“Kumbe wewe na mwanao mna hila kiasi hiki? Mmepatana kuondoka na kusafiri katika dau moja.” (uk 94).
“Ukienda Tabata utapata.”
“Waswahili hawana dogo.”
“Nikukonekti.” (uk 78).
“Kamba hukatikia pembamba.”
“Alikunywa funda moja, akajisikilizia kabla ya kulimeza. Alisikia pombe ikisafiri kufuata barabara ya lami hadi tumboni.” (uk 87).
MTINDO
Mtindo ni ule upekee wa mtunzi wakazi ya fasihi na mtunzi mwingine. Mfano, mwandishi anaweza kutumia, nyimbo, mashairi, nafsi zote, dayolojia, monolojia n.k. mwandishi amefanikisha mtindo wake kwa kutumia,
“Kuleni nae,
Hata bangi vuteni nae,
Lakini ni bure,
Mwenzenu nimezaa naye…”
MUUNDO
Muundo ni mpango na mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio.
Riwaya hii imetumia muundo wa kurukia. Mwandishi amemuonyesha Lomolomo akiwa katika hali ya ulevi, baadaye anatukumbusha alipokuwa anafanya kazi bandarini. Vilevile anawaonyesha Kurwa na Doto wakiishi peke yao. Lakini baadaye anatukumbusha kipindi walipokuwa wanalelewa na mama yao ambaye hata hivyo alifariki kisha wakalelewa na Jane ambaye naye anafariki.
MANDHARI
Mandhari ni sehemu ambayo kazi ya fasihi hutendeka. Riwaya hii imetumia mandhari ya jiji la Dar es Salaam na mitaa yake kama, Manzese, Msufini, Tabata, Kisutu, Urafiki na mtaa wa Ajentina.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu, Watoto wa Maman’tilie, linasadifu yaliyomo, kwani ndani ya riwaya hii kuna mhusika mkuu ambaye ndiye Maman’tilie.
Riwaya hii inamwonesha mama huyu akijaribu kujinasua yeye na watoto wake katika wimbi la umasikini, lakini wapi? Jitihada zote anazofanya zinagonga mwamba na matatizo yake yanazidi kuongezeka.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
KUFAULU KIMAUDHUI
– Mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuonyesha shida wazipatazo watoto wa mitaani.
– Mwandishi amefanikiwa kuonyesha madhara ya umasikini.
– Mwandishi ameonyesha madhara ya unywaji wa pombe kupita kiasi na ulevi.
KUFAULU KIFANI
– Amekitendea haki kipengele cha mtindo, kwani humo ametumia vipengele vingi kama nyimbo n.k.
– Kazi yake imeshibishwa kwa tamathali nyingi za semi.
– Ametumia lugha ya picha inayomwelewesha zaidi msomaji.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
– Kimaudhui. Mtazamo wa mwandishi katika suala la umasikini hauko sawa. Yeye anaamini hata ukifanya kazi kwa bidii kama ni masikini utaendelea kuwa masikini kama tumuonavyo Maman’tilie.
– Kifani wahusika wa mwandishi hawana uwiano. Wengi wao ni watu masikini.
– Pia, mandhari yote yaliyotumiwa na mwandishi ni ya mjini. Mwandishi ameutenga upande wa kijijini ambao nao kama ungetazamwa, jamii ingejifunza mengi.
|