ETIMOLOJIA YA NENO 'UBANI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'UBANI' (/showthread.php?tid=1863) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'UBANI' - MwlMaeda - 12-28-2021 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'UBANI' Neno ubani [Ngeli: u-/u-] katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana zifuatazo: 1. Utomvu mkavu wa mti wa mbani ambao unapochomwa hutoa moshi na harufu maalumu unaotumiwa kufukiza. Kuna methali : la kuvunda halina ubani; jambo linapokwenda kombo, huwa limekosa mwongozaji. Kuna msemo : wangu wa ubani; umpendaye kwa dhati. Kuna nahau : tia ubani; ombea dua. 2. Kiasi fulani cha pesa anachopewa mfiwa kusaidia shughuli za mazishi au kuwa msaada. Kuna msemo : toa ubani. 3. Utomvu wa mti fulani unaonatanata ambao unatumiwa kutengeneza vitu vitamu vya kuvutika kama mpira kama vile peremende. 4. Ada anayopewa mwalimu (wa madrasa) au Sheikh ukiwa ushuru wa kazi aliyofanya. Ada hii hulipwa mwanzoni au mwishoni mwa mafunzo. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili ubani (soma: lubanun/lubanan/lubanin لبان) ni nomino yenye maana zifuatazo: 1. Mmea wa familia ya uvumba ambao hutoa utomvu (gundi). 2. Utomvu (gundi) wa mti wa miiba ambao majani yake ni kama mihadasi. Mhadasi (wingi: mihadasi ) ni aina ya mmea wenye majani mabichi majira yote wenye matunda yenye mchanganyiko wa rangi ya bluu na nyeusi. 3. Maziwa ya mwanamke anayomnyonyesha mtoto; kwa Kiarabu huitwa hasa libanun/libanan/libanin لبان) 4. Kamba nzito ya mkonge ambayo hutumika kuvuta meli wakati wa shwari. Kwa Kiarabu huitwa hasa (libanun/libanan/libanin لبان). Katika Kiarabu kisawe cha lubaanun لبان ni kandar كندر neno lenye asili ya kiYunani. Kinachodhihiri ni kuwa neno ubani ( soma: lubanun/lubanan/lubanin لبان) lilipoingia katika Kiswahili maana yake ya msingi katika lugha yake ya asili - Kiarabu haikubadilika bali lilibeba dhana mpya ya kile kinachotolewa kumuhani mfiwa na ile ada anayopewa mwalimu wa madrasa au sheikh mwanzoni au mwishoni mwa mafunzo. Shukran sana. Khamis S.M. Mataka. |