UCHAMBUZI WA DIWANI YA KIMBUNGA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Uhakiki wa kazi za fasihi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=78) +--- Thread: UCHAMBUZI WA DIWANI YA KIMBUNGA (/showthread.php?tid=1816) |
UCHAMBUZI WA DIWANI YA KIMBUNGA - MwlMaeda - 12-25-2021 KITABU: KIMBUNGA
MWANDISHI: HAJI GORA HAJI
WACHAPISHAJI: TUKI
MWAKA: 1995
UTANGULIZI
Kimbunga ni diwani inayozungumziwa juu ya mawaidha mbali mbali katika maisha pamoja na suala zima la ujenzi wa jamii mpya. Katika diwani hii, mwandishi ametoa maadili na maonyo mbali mbali pamoja na mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikisha suala la ujenzi wa jamii hapa nchini.
Maudhui
Dhamira Kuu- Ujenzi wa jamii mpya
Mwandishi amejadili dhamira ya ujenzi wa jamii mpya katika kazi yake. Katika diwani hii mwandishi ameonesha vikwazo mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini. Vikwazo hivyo ni kama vile uongozi mbaya, rushwa, tamaa, ukosefu wa elimu, ukoloni mamboleo, n.k.
Katika kujadili dhamira hii mwandishi ameonesha mbinu/njia mbalimbali ambazo jamii inapaswa kuzitumia katika zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
Mwandishi ameonesha kuwa Uongozi bora unahitajika kwa jamii yoyote ile ili kuleta ufanisi mzuri katika utendaji na utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwani Uongozi mbaya unasababisha kushindwa kufikia malengo. Kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana jamii hufikia kufanya mpinduzi ili kuuondoa uongozi uliopo na kusimika uongozi mpya ili kuijenga jamii kwa upya.
Katika shairi la “Kimbunga” (uk 1) mwandishi anaongelea juu ya mapinduzi yanayofanywa na tabaka la chini dhidi ya tabaka tawala.mwandishi anasema;
‘’kimbunga mji wa siyu,kilichowahi kufika,
Si kwa yule wal huyu,ilikua patashika,
Kimeing’owa mibuyu,minazi kunusurika,
Nyoyo zilifadhaika.
Ametumia mji wa Siyu kama kielelezo kizuri kwa jamii yoyote inayotaka kufanya mapinduzi ili kuondoa viongozi wabovu na kuleta viongozi bora. Katika mapinduzi hayo mwandishi amefafanua kuwa wengi ndio wanaoathirika na wachache hunusurika.
Shairi la “Madanganyo” linazungumzia jinsi uongozi mbaya unavyowadanganya wananchi, unavyowaathiri na kuwakera wananchi. Wananchi hushiriki katika shughuli za uzalishaji mali (miradi mbli mbali) lakini matunda ya jasho lao hufidiwa na wachache. Wachache hao husahau wale waliosulubika katika uzalishaji na mtokeo yake wnanchi wanaishia kuishi maisha ya taabu. Ubeti wa 6, msanii/mwandishi ansema;
“Mlitupigia mbiu, tulimeni ushirika,
Tukakatana miguu, kwa mapanga na mshoka,
Manufaa kwa wakuu, wadogo yetu mashaka,
Wezeni kutukumbuka, mjue nasi wenzenu.”
Shairi la “Wenye Vyao Watubana” (uk 8) mwandishi amejadili namna matajiri au vitu jinsi wanavyowagandamiza, kuwanyonya na kuwabana wale wasio na chochote. Mwandishi anawaomba viongozi wawatetee ili kuepukana na hali hii. Hii ni kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana hali kama hii ipo nchini lakini viongozi hawachukui tahadhari.Ubeti wa 7, mwandishi anasema;
“Maji yamezidi unga, kwa lochi wa darajani,
Kujitole mhanga, kwa bei hiwezekani,
Mvao wake wa kanga, ni shilingi elifeni,
Wakubwa tuteteeni, wenye vyao watubana.”
Shairi la “Kibwangai” linajadili dhana ya usaliti wa viongozi wetu kwa wananchi wanaowaongoza. Mwandishi ameonesha jinsi wananchi wanavyowachagua viongozi wao lakini viongozi hao wakishapata madaraka au wakishashika nyazfa wanageuka na kuwasaliti wananchi waliowachagua. Msanii anathibitisha hayo kwenye ubeti wa 7;
“Kibwangai alipoona, ni mtu kakamilika,
Akaanza kujivuna, na dharau kuzidiya,
Wala hakujali tena, wenzake waliwambiya,
Akahisi hawi nyani, umbo lile litadumu.”
Shairi hili, limetumia taswira ya Kibwangai kuwakilisha viongozi wasaliti nanyani kuwakilisha wananchi wanaoongozwa na akina Kibwangai yaani watawaliwa.
Katika shairi la “Hili Mnatutakiya” , mwandishi anaonesha jinsi vyombo vya dola kama vile polisi ,jeshi namna vinavyoshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda raia na kuwashughulikia wahalifu..Ubeti wa 1msanii anasema;
Twasema kinaganaga,tumechoka vumiliya,
Wenzetu mkatubwaga,hasa ukiangaliya,
Hao wezi mwafuga,wazidi kutuibiya,
Msanii ameonesha kuwa vyombo hivyo ndivyo vinavyowalinda wezi,majambazi na matapeli.Kwa ujumla msanii wa diwani hii anaona kuwa ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi bora unaowajali wananchi wake.
Rushwa ni kikwazo kimojawapo kinachokwamisha kujenga jamii kwa upya. Kutokana na rushwa kuota mizizi katika jamii haki hupotea, wachache wanafaidi matunda ya nchi na wengine wanaendelea kuumia. Shairi la “Rushwa” mwandishi anasema;
“Rushwa kajenga kambi, na kuondoka hataki,
Afanya kila vitimbi, mkaidi hashindiki,
Tumzushieni wimbi, isiwe kutahiliki,
Tumchimbie handaki, rushwa tukamzikeni.”
Katika ubeti huu, mwandishi anatuonesha kuwa lazima jamii yetu ipinge rushwa ili haki na usawa vitawale.Kupiga vita rushwa ni njia pekee itakayoisaidia kujenga jamii mpya ambayo mwandishi ameipendekeza.
Ili tuijenge jamii mpya ni lazima watu wapate elimu na waelimike bila kujali umri. Mwandishi anawahimiza wazee kujiunga na kisomo chenye manufaa ili wafute ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Mwandishi anathibitisha haya katika shairi la “Kisomo cha Maarifa” Msanii ansema;
Kisomo chenye manufaa,tusomeni kwa haraka,
Isiwe tunakataa,kwa kuwa tumekongeka,
katika shairi hili mwandishi anawahimiza wazee wajiunge na kisomo cha elimu ya watu wazima kwa sababu wakishaelimika watakuwa na uwezo wa kupanga mipango yao ya maendeleo. mwandishi anaonesha kuwa elimu ni silaha madhubuti katika kufanikisha zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya kwani bila kuwa na wasomi katika jamii kama hii yetu zoezi la ujenzi wa jamii mpya halitaweza kufanikiwa.
Ukoloni mamboleo ni kitendo cha nchi kuwa na uhuru wa bendera lakini kimaamuzi inatawaliwa na nchi nyingine.Ukoloni mamboleo ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya uchumi hapa nchini. Na ili tuweze kufanikisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini hatuna budi kupiga vita ukoloni mamboleo . Katika shairi la “Chuwi” Mwandishi anaonesha jinsi ukoloni mamboleo unavyoathiri maendeleo ya uchumi hapa chini. Ukoloni mamboleo unawaathiri watu wa tabaka la chini wasio nachochote na kuwasetiri matajiri au tabaka la juu. Katika ubeti wa 6 mwandishi anasema:-
“Ambao ni matajiri, kwao anapowafikiya,
Huweza kujisitiri, salama kujipatiya,
Walokuwa mafakiri, huzidi kuwaoneya
Huyu ndiye Chuwi gani?
Mwandishi ameeleza kuwa ukoloni mamboleo huingia kwa njia mbali mbali katika nchi zinazoendelea. Hivyo mwandishi anatahadharisha kuwa tuepukane na mbinu (njia) hizo na tuupinge ukoloni mambo leo kwa nguvu zote ndipo tutaweza kujenga jamii mpya.
Ili tuweze kujenga jamii mpya ni lazima tujitawale katika Nyanja zote za kifikra, kisiasa, kiutamaduni pamoja na kiuchumi. Katika shairi la “Afrika “ Mwandishi anaeleza kuwa ili tuweze kujitawala ni lazima tuepukane na unafiki, vibaraka (wasaliti), tusikate tama na tudumishe amani. Katika ubeti wa 3 msanii ansema:-
“Wasaliti wazikishe, wasio wenye kuzuzuka,
Tamaa uwakalishe, yasiwe unayotaka,
Katu wasiwawezeshe, wabakie kuzuzuka,
Katu washindike mahusuda, wasiopenda bara letu.”
Katika shairi la “Kujitawala” Mwandishi anaeleza umuhimu wa kujitawala kwa jamii yoyote ile. Mwandishi anaonesha kuwa, kujitawala ni pale umma unapokuwa na mamlaka ya kuamua mambo yao wenyewe bila kuingiliwa au kuwekewa vikwazo vyovyote.Katika Ubeti wa 1 Msanii anasema:-
“Kujitawala ni kwema, kuliko kutawaliwa,
“Kujitawala ni umma, kila yao kuamua…”
Katika shairi hili la kujitawala mwandishi anonesha faida mbalimbali za kujitawala kama vile demokrasia, kuwepo umoja naushirikiano, kuwepo haki na usawa, amani hudumishwa, vile vile mila na desturiza nchi zinadumishwa. Hivyo mwandishi anatuasa kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima tujitawale kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kifikra.
Kazi ni nguzo muhimu sana ya ujenzi wa jamii mpya. Mwandishi amesisitiza umuhimu wa kazi na kuwajibika katika shairi la “Kazi” Mwandishi anatuonesha kuwa kzi ndio msingi wa maendeleo. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na tuepukane na uvivu. Ubeti wa 1, mwandishi anasema;-
“Pesa huletwa na kazi, ni njia zipitiayo….”
Katika shairi la “Uokolewe”, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano ili kuuinua uchumi wetu. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii kutumia vyema rasilimali zetu za kuinua uchumi wetu. Hivyo msanii aniasa jamii kujihusisha na ukulima, uvuvi, utalii na viwanda ili kujenga jamii kwa upya.
Katika shairi la “Dumizi” mwandishi anakemea tabia ya baadhi ya watu kukaa bila kazi (uvivu) na kuanza maisha ya kunyonya. Hivyo mwandishi anapiga vita unyonyajiwa watu waishio kwa jasho la wenzao.
Katika diwani hii, mwandishi ameonesha kuwa mapenzi yamegawanyika katika pande kuu mbili ambayo Kuna mapenzi ya kweli na udanganyifu.
Katika shairi la “Usimpige Mkeo “ mwandishi anasema kuwa haifai mwanaume kumpiga mke wake na vile vile mwanaume hatakiwi kumwekea mkewe masharti magumu.
Shairi la “Hongera” mwandishi anaendelea kujadili suala la mapenzi na ndoa katika jamii zetu. Anawaonya wanandoa(bibi na bwana) wasiwe na tabia ya kufukuzana wawapo nyumbani. Amewapa kila mmoja maadili yake kwa mwenzake. Beti za (4-5) mwandishi anasema:-
4- “Bi arusi yangu shika, uyatie akilini.
Mumeo akifika, anapotoka kazini,
Mpe mema mamlaka, aliwazike moyo,
Hongera.”
5- “Bwana arusi sikia, ukiwa kwako nyumbani,
Maneno ya kutupia, hayafai asilani,
Kauli njem tumia, na lugha iwe laini,
Hongera”
Katika shairi la “Sifa ya Mke” Msanii anaonesha kuwa sifa kubwa ya mwanamke ni tabia na wala si sura. Sifa ya tabia njema humpa mwanamke taadhima, huruma, utiifu na hata uhodari. Anaeleza kuwa mwanamke anapaswa kuwa mtulivu, asiwe kiruka njia, asiwe na ufedhuli wa aina yoyote, uovu, n.k.
Katika shairi la “Sitaki” Mwandishi anakemea mapenzi ya udanganyifu yaliyoshamiri katika jamii zetu kwa wakati huu. Anasema:-
“Rabi simpe mapenzi, hakuna wa kuamini,
Wapendwa wenye ujuzi, ni wachache duniani,
Mapenzi yamepotea, sasa ni adimu sana,”
Ni kweli mapenzi ya siku hizi hutawaliwa na pesa na yamejaa ulaghai wa kila aina pamoja na udanganyifu.
Mwandishi amekuwa mwalimu mzuri wa walimwengu kuhusiana na harakati mbali mbali za maisha. Mawaidha aliyoyatoa mwandishi ni kielelezo kizuri kinachofaa kufuatwa na kizazi hiki. Maadili na maonyo haya ni ya muhimu sana katika maisha. Maadili hayo ni kama vile:-
(a)Malezi bora katika jamii ni njia pekee ya kuiweka jamii katika msingi bora wa maisha. Katika shairi la “Vijana wa Zanzibar” Mwandishi ameonesha kuwa matendo ambayo vijana wa siku hizi wanayatenda si mazuri, ni ya kusikitisha. vijana wa siku hizi hawana utii, ni wajeuri, ni wadanganyifu, ni majambazi na pia hudharau mila na desturi zetu za asili a kukimbilia tamaduniza kigeni. Katika ubeti wa 2 msanii anasema:-
“Mwawacha yenu ya hapa, ambayo yako mazuri,
Kutii na kuogopa, mwaona haina heri,
Mwayavamia kwa pupa, kwa kedi na jeuri,
Mila zetu za fakhari, wacheni kuzipotosha.”
Kulingana na ubeti huu,mwandishi anaonesha kuwa suala la malezi bora ni muhimu sana katika jamii ili kuwaandaa vijana wetu kuendana na mazingira wanamoishi.
.
Kwa ujumla, katik suala la malezi mwandishi anaifundisha jamii kuwa, samaki mkunje angali mbichi.
b)Umuhimu wa kuwathamini wazazi
Mwandishi ameonesha kuwa kuna umuhimu wa kuwaheshimu na kuwathamini wazazi. Katika shairi l “Wazazi” ameonesha kuwa wazazi ndiyo ngao ya mtoto; mtoto hatakiwi kuwakasirikia, kuwaudhi wala kuwachikiza bali anatakiwa kuwa na mapenzi nao. Wajibu wa wazazi kwa mtoto ni kumpa chakula, mavazi, malezi mema pamoja na elimu. Katika ubeti wa 4:-
“Wakatafuta walimu, kukupatia ujuzi,
Wakakufunza elimu, pamoja na matumizi,
Sasa ni mtu timamu, waendelea na kazi,
Usiwaudhi wazazi, hiyo ndiyo yako ngao”
Katika shairi la “Ulezi Kazi” Mwandishi ameonesha jinsi mama (wazazi) wanavyohangaika kubeba mimba hatimye kuzaa na kuanza kazi ya ulezi wa mtoto hadi anapofikia umri wa kujitegemea. Anaonesha kuwa wazazi hupata taabu na shida mbalimbali katika ulezi wao. Hivyo mwandishi anashauri wazazi wathaminiwe napewe heshima zote.
c)Kuepukana na umbea
Umbea ni ile tabia ya kutoa maneno au habari bila kutumwa. Mwandishi anaona tabia hii si nzuri, kwani huweza kutenganisha marafiki au ndugu kwa njia ya uchonganishi.
Katika shairi la “Wacha Hayo” mwandishi anaishauri jamii iepukane na umbea na badala yake ijishughulishe katika shughuli za uzalishaji mali. Madhara ya umbea ni kama vile majungu, uchochezi, n.k. Umbea pia husababisha utengano. Ubeti wa 1 mwandishi anasema;
“Wacha kupika majungu, na kuleta uchochezi,
Kuwajaza walimwengu, kasumba zile na hizi,
Hicho kimoja kifungu, huletesha ubaguzi,
Tuacheni ubaguzi, huvunja mafanikio.”
Katika shairi la “Hayafai Mitaani” mwandishi anaionya jamii kuwa si jambo la busara au zuri kusambaza au kupeleka taarifa ya jambo fulani sehemu ambayo haihusiki. Anaona kuwa ni busara sana endapo jambo fulani limefanyikia sehemu fulani liishie huko huko lilikotokea na haifai kulipeleka sehemu isiyohusika. Si tabia nzuri kupeleka mitaani kwa watu wasiohusika. Ubeti wa 2 unasema:-
“Yanayosemwa kunini, huko huwa yamekisha,
Haifai asilani, mitaani kufikisha,
Kwani siri ya mwituni, si vyema kuelewesha,
Ya kunini huishia kunini.”
Hivyo mwandishi anatushauri kuwa jambo mojalikitendeka sehemu moja ni bora liishie katika sehemu hiyo na hakuna haja ya kulipeleka sehemu nyingine.
(d)Kuepukana na udokozi (tabia ya wizi)
Udokozi ni ile hali ya kunyemelea vitu visivyo vyako kwa lengo la kuiba au kunyang’anya. Mwandishi anakemea tabii hii kwani si nzuri. Tabia hii ipo miongoni mwa wanajamii. Mwandishi anaonya kuwa tabia hii huhatarisha maisha ya wahusika yaani wenye tabia hii. Mwandishi amemtumia pakakuwakilisha watu wenye tabia hiyo. Aidha mwandishi anaendelea anaelezea kuwa tabia hii husababisha uchokozi, ugomvi pamoja na chuki katika maisha.
(e)Umuhimu wa shukrani katika maisha
Mwandishi anaieleza jamii umuhimu wa kutoa shukrani pale mtu anapofanyiwa hisani na mtu mwingine. Katika shiri la “Punda” mwandishi ameonesha jinsi baadhi ya watu wasivyo na shukrani katika maisha . Ameonesha kuwa mwandamu asiye na shukrani hata umfanyie wema kiasi gani hawezi kutoa shukrani. Ameelezea kuwa mtu asiye na shukrani ni kuachana naye au kumtenga (kutengana naye) kabisa. Anasema;
“Punda hakumbuki wema, hta kwa mchunga wake,
Humpa mwingi mtama, na majianufaike,
Katu hawi salama, shukrani zake mateke,
Ndiyo tabia ya punda, kurusha rusha matee,
Kuchunga akikushinda, mwacheaende zake.”
Katika ubeti huu, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kutoa shukrani pale tunapofanyiwa fadhila.
UJUMBE
Ø Dhana potofu ya kudhani bila ya kuwa na uhakika wa mambo haifai katika jamii kwa sababu hupotosha ukweli wa mambo.
Ø Mapenzi na ndoa ya dhati ni muhimu katika jamii zetu
Ø Ukoloni mamboleo, uongozi, mbaya, rushwa na ukosefu wa elimu ni baadhi ya vikwazo vya ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
Ø Maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika misingi ya haki na usawa.
FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika msimamo na mwendo bora wa maisha na anatetea misingi ya haki na utu katika jamii.
MSIMAMO
Msimamo wa mwandishi una hali ya udhanifu kwani amejadili baadhi ya mambo katika jamii kwa kudhani tu bila kuwa na misingi ya kisayansi.
FANI
a)Muundo
Mwandisha ametumia miundo tofauti katika diwani hii kma vile;Tarbia (mistari 4), Tathlitha (mistari 3) katika shairi la “Kujitawala” (uk 7-8).
Pia ametumia muundo wa takhimisa (sabilia) – mistari 5 na kuendelea katika shairi la “Punda” (uk 21-22), shairi la “Bahati” (uk 36).
b)Mtindo
Mtindo uliotumika ni ule unaofuata kanuni za mapokeo za urari wa vina na mizani pamoja na mpangilio wa beti. Karibu mashairi yote yana vina vya kati na mwisho isipokuwa katika mashairi ya “Kimbunga” (uk 1), “Dumuzi” (uk 41), “Madereva” (uk 43), “Chuwi” (uk 42) yana nusu mstari katika kituo.
c)Matumizi ya Lugha
Mwandishi ametumia lugha rahisi iliyoshehenezwa lahaja ya Kiunguja yenye mafumbo na taswira mbali mbali na tamathali za semi kidogo na misemo kwa kiasi.
d)TAMATHALI ZA SEMI
Tashibiha
-Kwenye shairi la “Sifa ya Mke” (uk 40)
-Ufedhuli na uovu kama yake mazoea.
-Awe kama malaika mzuri kupindukiya
Tafsida
Mwandishi ametumia mbinu ya kufumba kwa kusema maneno makali, machafu, matusi kw kutumia tafsida. Mfano shairi la “Nyang’au” (uk 44) linahusu tamaa, “Paka” (uk 22) linahusu wizi, shairi la “Dumuzi” (uk 41) linakemea uvivu, n.k.
Mbinu Nyingine za Kisanaa
Takriri
Mwandishi ametumia takriri ili kuweka msisitizo mfano shairi la “Kujitawala” (uk 7-8) neno kujitawala limerudiwarudiwa.
Matumizi ya Taswira
Mwandishi ametumia taswira nyingi kama vile;
Mfano: Kimbunga …(uk 1)…..Kuashiria mapinduzi
Kibwangai…(uk 9)….Kuashiria viongozi wasaliti
Nyani…..(uk 9)…….Kuashiria wananchi waliosalitiwa
Chuwi…..(uk 42)…..Kuashiria ukoloni mamboleo, n.k.
Jina la Kitabu
Jina la Kitabu Kimbunga halisadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu kwa sababu hatuyaoni mageuzi yoyote ambayo anayajadili katika kitabu hiki zaidi ya mashairi ya maadili mema na maonyo ya kimaisha. Asilimia kubwa ya mashairi katika diwani hii yamejadili juu ya maonyo na maadili katika maisha.
Kufaulu kwa Mwandishi
Kimaudhui
Mwandishi amefaulu ;
Ø Kutoa maadili mema na maonyo katika jamii
Ø Kujadili dhamira ya ujenzi wa jamii mpya
Ø Ameonesha mbinu mbalimbali za kufuata ili tufanikiwe katika ujenzi wa jamii mpya
Kifani
Ø Ametumia lugha rahisi, mafumbo, taswira, n.k.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
Ø Baadhi ya maadili aliyoyajadili katika kitabu hiki ameyajadili kidhanifu, ni sawa na yale tunayoyapata makanisani, ambayo yana nafasi ndogo sana katika ujenzi wa jamii mpya
Ø Vile vile amejadili masuala mbalimbali kidhanifu hasa anapomhusisha Mungu. Kama vile maswala ya kipaji (uk 38-39), bahati (uk 36), umaskini (uk 35).
Kifani
v Mwandishi ametumia lahaja ya Unguja badala ya Kiswahili sanifu ivyo ni vigumu kueleweka kwa watu wote.
v Diwani hii ni ya hali ya chini sana katika muundo, mtindo na baadhi ya vipengele vingine vya kisanaa.
|