UHAKIKI WA TAMTHILIYA YA KWENYE UKINGO WA THIM - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Uhakiki wa kazi za fasihi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=78) +--- Thread: UHAKIKI WA TAMTHILIYA YA KWENYE UKINGO WA THIM (/showthread.php?tid=1813) |
UHAKIKI WA TAMTHILIYA YA KWENYE UKINGO WA THIM - MwlMaeda - 12-25-2021 KITABU: KWENYE UKINGO WA THIM
MWANDISHI: IBRAHIM HUSSEIN
MCHAPISHAJI: OXFORD UNIVERSITY PRESS
MWAKA: 1988
UTANGULIZI
Kwenye Ukingo wa Thim ni tamthiliya inayoonesha na kuibua mgogoro uliopo katika hali halisi ya maisha. Mvutano uliopo baina ya mahitaji ya mila na ya kisasa (ukale na usasa) na maonevu yaliyopo-maonevu ya mwanamke na upendeleo wa mwanaume katika sheria za taasisi za utamaduni wa Mwafrika. Aidha mwandishi amenonesha jinsi mvutano huo unavyoleta athari katika jamii.
Maudhui
Dhamira Kuu: Ukombozi wa kiutamaduni
Katika kuijadili dhamira hii mwandishi anaonesha wazi kasoro zinazojitokeza katika utamaduni wa Kiafrika, kama asmeavyo katika utangulizi wake wa kitabu …
“Katika kutumia na kufasiri kipengele cha utamaduni wa Mwafrika kama nilivyofanya mimi katika mchezo huu nimehisi kuna wlakini”.
Walakini anaouzungumzia mwandishi katika utamaduni wa Mwafrika una athari mbaya kwajamii, kwani unasababisha mvutano kati ya ukale na usasa ambao ndicho kiini cha tamthiliya hii.
Ndoa ya Herbert na Martha ambao wameoana watu wa kabila tofauti imechangia kwa kiasi kikubwa juu ya mvutano huu. Jamii nyingi za Kiafrika, mila na desturi zao haziruhusu mwanamke kuolewa au mwanaume kuoa njeya kabila lake. Kutokana na mila hizi kushikiliwa na jamii zetu za Kiafrika, inazua mvutano kati ya vijana na wazazi. Vijana hawaoni sababu inayowazuia kuoa au kuolewa na mtu asiye wa kabila lake wakati wao wanapendana. Kwa upande mwingine mvutano huu umechangiwa na mabadiliko ya jamii kiuchumi, kiasia na kiutamaduni na mabadiliko haya hayajawakumba wazee ambao hayo ndio wanaoshikilia mila hizo zilizopitwa na wakati. Vijana wanaona mabadiliko hayo ni mkombozi kwa upande wao juu ya mila na desturi hizo kama anavyosema Lydia;
“Ndiyo ukweli wenyewe siku hizi mambo ya kisasa. Kila kitu cha kisasa. Mtazame Herbert au Martha. Hii habari ya kuoana kabila moja imekwisha kila unayemuona hivyo hivyo hata Chris” (Uk. 9).
Hivyo mwandishi anaonesha kuwa ili tujikomboe kiutamaduni lazima tufutilie mbali mila kama hizo, kwani zimepitwa na wakati. Hazina nafasi katika kizazi hiki. Masuala ya ndoa yaamuliwe na wale wanaopendana na sio mila na desturi za jamii. Athari hii ya kushikilia ukale kwa upande mwingine hata kwa wasomi haifai kwa kumtumia mhusika Ben, ambaye ni Mwalimu wa Chuo Kikuu, anaamini kuwa mke wa kweli lazima awe ni wa kutoka kabila lako. Haya yanadhihirishwa wazi na mazungumzo ya Ben na Herbert juu ya ndoa ya Herbert na Martha (uk. 11).
Ben: “Toka huyo mke ameolewa na wewe mimi simjui kama dada yangu labda ni bibi yako tu”
Herbert: “Wewe huoni aibu kuwa mkabila…..wewe umesoma halafu bado mkabila kiasi hicho”
Ukabila unapoota mizizi katika jamii una athari zake kama vile kuuana hovyo kama ilivyotokea Burundi na Rwanda. Na ni kutokana na ukabila huo ndio unaosababisha kifo cha Herbert (uk. 14).
Kwa upande mwingine mwandishi anaonesha kuwa, utamaduni wa Mwafrika unamgandamiza na kumuonea mwanamke. Utamaduni huo unamnyima haki za kuamua mambo yake mwenyewe, unamnyima haki ya kurithi mali alizochuma na bwana wake anapokufa. Mwandishi katika utangulizi wake anasema kuwa mwanamke anaonewa na taasisi za utamaduni wa Mwafrika.
Vilevile mwandishi anaonesha kuwa, baadhi ya watu hasa waliosoma na kubahatika kupata kazi mijini wanasahau vijijini kwao ambako walizaliwa. Mfano halisi ni Herbert ambaye baada ya kupata kazi mjini alisahau kabisa kijijini kwao kiasi cha kushindwa hata kujenga nyumba au kibanda cha kujisetiri kama asemavyo mwandishi (uk. 17);
Mzee: “Herbert alikuwa mtu mjinga hakuwa mwerevu, si vizuri kusema maiti kwa vibaya lakini Herbert aliishi chini ya matakwa ya mkewe hata kibanda kimemshinda kujenga?”
Lydia: “Kwa nini Herbert hakujenga kibanda?”
Mzee: “Dharau….!”
Hii si tabia ya Herbert tu katika jamii yetu. Tunao watu wa namna hii ambao hawataki kurudi kwao kwa ajili ya anasa na starehe za mjini (Rejea Mtawa Mweusi na Ngugi wa Thiong’o).
Dhamira Ndogondogo
Nafasi ya mwanamke katika jamii
Katika tamthiliya hii mwanamke anaoneshwa kwa pande mbili. Kwanza kama mwanamapinduzi na pili kama kiumbe duni anayeonewa na kunyanyaswa na mwanaume.
Mwanamke kama mwanamapinduzi ameoneshwa jinsi Martha alivyoshiriki vita vya msituni vya Mau Mau huko Kenya bega kwa began a wanaume katika kuutokomeza ukoloni wa Kiingereza nchini Kenya (uk. 26). Mwanamke kama kiumbe duni ameoneshwa jinsi sheria za taasisi za utamaduni wa Mwafrika zinavyomwonea na kumgandamiza mwanamke. Sheria hizo zinamnyima haki anayotakiwa kupata kama mke. Mwandishi anaonesha wazi kuwa mwanaume anapendelewa na mwanamke anaonewa na kunyanyaswa na sheria hizo. Anasema hivi…. (uk. 30)
“Mwanamke utakuwa na pesa uliyopata kwenye kibarua na kufunga ndoa na kuanzisha familia….ukipatana na mme basi hiyo ni bahati yako……”
Hapa mwandishi anaonesha kuwa, mwanamke ananyanyashwa juu ya hata kile alichonacho mwenyewe. Hali hii ipo katika utamaduni wetu wa Kiafrika ambao mwandishi anaona una walakini. Vilevile mwandishi anaonesha kuwa, wanaume wana uhuru wa kufanya jambo lolote watakalo bila kipingamizi. Ana uwezo wa kutafuta mke mwingine kijana zaidi, anakwenda kilabuni na mwenzie bila matatizo yoyote. Lakini mwanamke kufanya hivyo hawezi kwa sababu ya sheria zilizopo. Martha anasisitiza hivi (uk. 30)….
“Kwa mwanaume mambo ni rahisi ndani ya nyumba hayamwelemei…..mwanamke kufanya hivyo ndio mwanamke kupewa talaka jina baya! Unaona?”
Hapa mwandishi anaonesha wazi jinsi wanawake wanavyonyimwa uhuru wao wa kufanya mambo watakayo wenyewe. Hili ni zao halisi la maisha ya jamii nyingi zenye mwenendo na taratibu za namna hiyo za kumwonea, kumgandamiza na kumnyanyasa mwanamke. Licha ya hiyo, mwandishi pia anaonesha jinsi mwanamke anavyonyimwa haki ya kurithi mali waliyochuma na mumewe pindi bwana wake anapoaga dunia. Hii inadhihirishwa wazi jinsi Martha alivyolazimishwa kutoa kila kitu kwa George na Umma Klan baada ya mume wake kufa. Mwandishi anasema (uk. 25)…
“Basi baba yako katuachia kichwa cha tembo. Tumewinda pamoja…..unavyotuona hapa sisi ni maskini…..unapoteza mume, maisha na kila kitu!”
Mwandishi anaonesha kuwa, mwanamke anapofiwa na mume wake anapoteza kila kitu cha mume wake. Martha alikataliwa kumzika mume wake Herbert kwa madai kuwa yeye ni mwanamke. Mila na desturi za Kiafrika zinamnyima haki mwanamke hata kama vyombo vya sheria vimeamua (uk. 23). Ili kujikomboa kiutamaduni mwandishi anaonesha kuwa jamii haina budi kutupilia mbali baadhi ya mila hizo zinazomnyanyasa, kumuonea na kumgandamiza mwanamke.
Malezi
Malezi ni dhamira mojawapo inayojitokeza katika tamthiliya hii. Mwandishi anaonesha kuwa malezi mabaya yana athari mbaya hapo baadaye kwa wanaohusika.
Malezi aliyopewa Chris na baba yake wa kumlea, Herbert, bila kumwambia baba yake halisi ni kinyume na taratibu za malezi bora kwa watoto. Martha na Herbert hawakumfahamisha Chris ukweli wa mambo ulivyo hadi anakuja kujua kuwa Herbert sio baba yake baada ya kifo cha Herbert. Hali hii ilitaka kuzua mvutano kati ya Chris na mama yake Martha (uk. 24-25).
Vilevile kitendo cha baba na mama kucheza kwa kukumbatiana mbele ya watoto wao ni kinyume na desturi za Kiafrika. Huo ni mwigo kutoka kwa wageni ambao unazidi kushamiri katika jamii yetu. Mwandishi anatutahadharisha kuwa, hali hii ina athari kubwa kwa malezi ya watoto wetu kwa sababu tunawafundisha watoto mambo ya kigeni badala ya kuwafundisha utamaduni wetu (uk. 12).
Ndoa
Katika kujadili dhamira hii mwandishi ameonesha wazi jinsi mila na desturi za Kiafrika zilivyo na athari mbaya katika suala la ndoa. Vijana wengi wanashindwa kuoa/kuolewa kutokana na sheria mbalimbali zinazowazuia vijana, ambazo zimekumbatiwa na jamii zetu nyingi.
Mfano mzuri ni ndoa ya Herbert na Martha ambao walioana kutoka kabila tofauti. Hii iliwafanya watengwe na jamii yao kwa madai kuwa wamekiuka taratibu za jamii kama anavyosema Martha (uk. 26-27);
“Jamaa zangu damu moja walinitenga siku ya ndoa. Ben peke yake ndiye aliyekuwa na mimi; jamaa za mume wangu pia walinitenga siku hiyo…..”
Katika dondoo hii, mwandishi anaonesha kuwa, baadhi ya mila zinawanyima vijana uhuru wa kuamua ni nani awe mke au mume. Na hii ina athari zake kwa jamii, kwani mara nyingi inazua mvutano kati ya ukale na usasa.
Mwandishi anapendekeza kuwa ili kujikomboa kiutamaduni lazima tutupilie mbali baadhi ya mila hizo ili kuwapa vijana uhuru wa kuchagua wenzi wao wanaowapenda wenyewe. Vijana wakipewa uhuru huo itazuia kutokea kwa mivutano baina ya wazee na vijana. Mawazo haya yanajadiliwa pia na A.J Safari katika Harusi, H. Mwakyembe katika Pepo ya Mabwege, N.Balisidya katika Shida na E. Hussein katika Wakati Ukuta, n.k.
Dhana potofu
Kuna baadhi ya watu wana dhana potofu akilini mwao kuhusu uonevu na unyanyasaji wa akina mama katika jamii. Mojawapo ya dhana hii potofu inatokana na imani kuwa uonevu na unyanyaswaji wa akina mama ni mpango wa Mungu. Hali hii inadhihirishwa wazi na mazungumzo ya Pasta na Martha (uk. 30-31).
Vilevile kuna wengine wanaamini kuwa hali zote za watu wawe matajiri au maskini ni mipango ya Mungu. Pasta anaonesha kuwa utajiri wa Martha na Herbert ni Mungu kawapa na hata baada ya Martha kupokonywa kila kitu na George pamoja na Umma Klan ni mipango ya Mungu, Pasta anasema (uk. 31);
“Unakumbuka uliponunua nyumba hii…..ulijiona umefika sasa……hii ni kazi ya Mungu ambayo haina makosa”
Mawazo kama hayo ni potofu na hayana ukweli wowote ndani yake. Mhusika anayetamka haya anaamini kuwa Mungu huwapendelea baadhi ya watu ili wawe matajiri na wengine masikini. Kwa ujumla, utajiri au umaskini hautoki kwa Mungu bali ni matokeo ya mfumo wa siasa wa jamii unaotawala jamii hiyo, ndiyo unaosababisha utajiri au umaskini wa mtu. Kwa upande mwingine. Pasta anaamini kuwa, kunyanyaswa na kuonewa kwa mwanamke ni maamuzi ya Mungu na mwanamke hawezi kutafuta suluhu bali ni kumwachia Mungu ambaye ndiye mwenye mipango yote, Pasta anasema (uk. 30);
“Wewe huwezi kujua la kufanya mwachie Mungu”.
Msanii anaitahadharisha jamii juu ya mawazo kama haya kuwa ni mawazo potofu. Vilevile anaonesha kuwa kunyanyaswa na kuonewa kwa mama kunatokana na sheria za taasisi za utamaduni wetu pamoja na mfumo wetu wa maisha unaomfunga mama kama kiumbe duni katika jamii. Msanii anaonesha kuwa ili kujikomboa kiutamaduni hatuna budi kufuta mawazo hayo, kwani hayana nafasi kwa jamii ya sasa.
Utekelezaji mbaya wa mipango ya maendeleo ya taifa
Licha ya kujadili dhamira ya ukombozi wa kiutamaduni, vilevile mwandishi anajadili juu ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa.
Katika tamthiliya hii msanii anaonesha wazi jinsi viongozi wanavyopingana wao kwa wao juu ya utekelezaji wa maamuzi yanayohusu ujenzi wa taifa. Msanii anaonesha kuwa kiongozi fulani anaagiza wananchi wafanye kitu fulani na halafu kiongozi mwingine anakataza jambo hilo lisifanyike. Wananchi wanapoacha anakuja mwingine na kuwahimiza kufanya kitu hichohicho. Kutokana na hali hii viongozi wanaleta mkanganyiko kwa wananchi wakati wa utekelezaji wa mipango hiyo ya kimaendeleo (uk. 19-20). Hapo swali la kujiuliza ni kuwa, wananchi washike la nani na kuacha la nani? Hapo ndipo unapokuja mkanganyiko wa mawazo yanayokwamisha maendeleo ya jamii kwa ujumla. Na ni kutokana na hali hii ya viongozi wetu kupingana wao kwa wao ndiyo maana wanashindwa kuinua hali ya uchumi wan chi yetu na matokeo yake ni kudidimiza zaidi uchumi.
Migogoro
Ujumbe
Falsafa ya mwandishi
Mwandishi anaamini kuwa ili kujikomboa kiutamaduni ni lazima tufutilie mbali baadhi ya mila ambazo zimepitwa na wakati kama vile kumwona mwanamke kama kiumbe duni. Suala la ndoa kuachiwa wale wanaopendana na mawazo potofu juu ya kunyonywa na kuonewa kwa mwanamke kuwa ni mpango wa Mungu. Vilevile mwandishi anaamini kuwa mipango mizuri ya maendeleo na utekelezaji wake mzuri utaleta manufaa nchini.
Msimamo wa mwandishi
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi, kwani anaonesha wazi kasoro mbalimbali zinazojitokeza katika utamaduni wetu wa Kiafrika na anashauri jamuu kuziondoa kasoro hizo kwani zinawanyanyasa na kuwaonea baadhi ya watu katika jamii hasa wanawake na vijana.
Fani
Muundo
Muundo wa tamthiliya hii ni wa moja kwa moja. Mchezo unaanza kwa kuonesha juu ya ndoa ya Herbert na Martha hadi vifo vya wote wawili na matokeo yake. Mchezo umegawanyika katika sehemu kuu nne na kila sehemu ina onyesho moja lenye kichwa cha habari. Mfano Onyesho la I Nyumba, Onyesho la II Nyumbani, Onyesho la III Chira, Onyesho la IV Msingi uliobomoka.
Mtindo
Mwandishi ametumia dayalojia (majibizano) katika tamthiliya hii, na nafsi zote tatu zimetumika katika mchezo huu.
Matumizi ya Lugha
Lugha iliyotumika ni ya kawaida yenye sentensi fupifupi na yenye mbinu mbalimbali za kisanaa.
Tamathali za semi
Tafsida
Tashihisi
Mbinu nyingine za kisanaa
Takriri
Mjalizo
Mdokezo
Lugha ya Kishairi
Vilugha
Wahusika
Herbert na Martha
Hawa ndio wahusika wakuu wa mchezo huu ambao maudhui yote yanawazunguka wao. Hawa ni mume na mke ambao kuoana kwao kumesababisha kutengwa na jamii, kwa sababu ya kuoana watu wa kabila tofauti. Herbert ni msomi ambaye ana kazi nzuri mjini na kutokana na kuathiriwa na kazi mjini anasahau kijijini kwao kiasi cha kutowatembelea ndugu zake.
Martha ni mke wake Herbert ambaye alipigana vita vya Mau Mau na baaba ya kifo cha mumewe ananyang’anywa kila kitu na Umma Klan kwa kisingizio cha kuwa yeye ni mwanamke ambaye hastahili kurithi chochote. Herbert na Martha ni mfano wa watu wanaopenda mabadiliko katika jamii nan i vielelezo vya watu wanaopinga ukabila katika jamii. Hivyo ni mfano bora wa kuigwa.
Chris
Ni mtoto wa Martha anayesoma Columbia (Amerika ya Kusini). Ni mtoto aliyetegemewa kuwa mrithi wa Herbert, lakini kutokana na kitendo cha kuwa mtoto wa nje anakosa urithi huo.
George
Huyu ni ndugu wa Herbert aliyemdhulumu Martha, shemeji yake, mali zote baada ya Herbert kufa. George ni kiwakilishi cha watu wanaoshikilia mila za kizamani zilizopitwa na wakati. Hivyo hafai kuigwa na jamii.
Lidya, Jean na Stella
Hawa ni wawakilishi wa vijana wa kike wanaoona umuhimu wa mabadiliko katika jamii hasa katika kipengele cha utamaduni. Hawa wako mstari wa mbele katika kufutilia mbali desturi zinazowagandamiza wanwake katika jamii.
Ben
Mwalimu wa Chuo Kikuu anayeshikilia ukabila katika jamii, Ben ndiye aliyesababisha kifo cha Herbert nan i mtu asiyefaa kuigwa.
Mandhari
Mandhari ya kitabu hiki ni nchini Kenya mjini na kijijini. Uthibitisho ni vita ya Mau Mau na ukabila ambao umekithiri nchini Kenya, na neno “chira” lenye asili ya Kijaluo kabila lililopo mpakani mwa Tanzania na Kenya. Vilevile kuna mandhari ya nyumbani, msituni wakati wa Mau Mau, barabarani, ofisini, mitaani, shuleni, n.k
Jina la Kitabu
Jina la kitabu Kwenye Ukingo wa Thim linasadifu yaliyomo ndani ya kitabu. Kwanza Thim kwa Kijaluo ni Msitu. Kitaswira Kwenye Ukingo wa Thim linaashiria kuwa ukingoni mwa msitu (mila na desturi zilizopitwa na wakati) kwa maana ya jitihada za jamii kutoka katika kifungo cha mila na desturi zilizopitwa na wakati. Vilevile inaashiria kuwa baadhi ya wahusika kama vile Herbert, Martha, Chris, Lydia, Jean na Stella nao wako pembeni mwa mila hizo.
Kufaulu kwa Mwandishi
Kimaudhui
Mwandishi amefaulu sana katika kuonesha kasoro mbalimbali zinazojitokeza katika jamii za Kiafrika kama vile kumwona mwanamke kama kiumbe duni katika jamii, kung’ang’ania ukabila na kupendelewa kwa wanaume katika jamii za Kiafrika.
Kifani
Mwandishi amefaulu pia kutumia lugha rahisi yenye sentensi fupifupi na yenye kueleweka. Ujenzi wa wahusika ameugawa katika pande mbili, wanaopenda mabadiliko na wasiopenda mabadiliko.
Kutofaulu kwa Mwandishi
|