ETIMOLOJIA YA MANENO ' ADA' na 'ADAA' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO ' ADA' na 'ADAA' (/showthread.php?tid=1791) |
ETIMOLOJIA YA MANENO ' ADA' na 'ADAA' - MwlMaeda - 12-22-2021 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' ADA' na 'ADAA' Neno *ada* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino* : Gharama au karo anayolipa mtu ili apatiwe huduma fulani kwa mfano katika elimu, burudani au kupata uanachama katika chama. 2. *Nomino:* Mila na desturi za jamii fulani. (Mfano: Kila kabila lina ada zake za maziko.) 3. Kawaida katika kufanya jambo. (Kwa mfano: Kunywa chai kila jioni ni ada yake.) Kuna methali: *Ada ya mja hunena, muungwana ni kitendo.* Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *ada* (soma: *aadatun/aadatan/aadatin عادة* ) lina maana zifuatazo: 1. *Nomino* : Jambo ambalo mtu amezoea kulifanya na kulikariri. 2. *Nomino* : Kulitekeleza jambo ipasavyo na ndani ya wakati. 3. *Nomino* : Kutimiza wajibu na kuukamisha. 4. Jambo linalokariri kutokea kila mwezi; ada ya mwezi. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *aadatun/aadatan/aadatin عادة*) lilipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *ada* maana yake katika Kiarabu haikubadilika na lilichukua dhana mpya ya *gharama au karo anayolipa mtu ili apatiwe huduma fulani a* dhana ambayo Kiarabu huitwa *rasmun/rusuumun* *رسم/رسوم* . Neno *adaa* katika lugha ya Kiswahili lina maana ya 'ulazima unaompasa mtu kuutekeleza kwa mujibu wa maamrisho ya dini kwa mfano kuswali, kufunga na kutoa Zaka. Neno hili *adaa* (soma: *adaa-un/adaa-an/adaa-in أداء* ) katika lugha ya Kiarabu lina maana ya: 1. Kulifikisha jambo na kulitimiza au kulitekeleza kwa namna inavyopasa. 2. Kuzitamka herufi za lugha kwa namna inayopasa. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili *adaa*(soma: *adaa-un/adaa-an,/adaa-in أداء*) lilipoingia katika Kiswahili maana yake katika Kiarabu haikubadilika ingawa lilijifunga katika wajibu wa kutekeleza maamrisho ya dini. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |