ETIMOLOJIA YA MANENO ' ABYADHI' na 'AHAMARU/AHAMARI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO ' ABYADHI' na 'AHAMARU/AHAMARI' (/showthread.php?tid=1789) |
ETIMOLOJIA YA MANENO ' ABYADHI' na 'AHAMARU/AHAMARI' - MwlMaeda - 12-21-2021 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' ABYADHI' na 'AHAMARU/AHAMARI' Neno *abyadhi* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino* : Kete/karata isiyo na alama yoyote inayotumika katika mchezo wa dhumna (dominos). 2. *Kivumishi:* - enye rangi nyeupe. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *abyadhi* (soma: *abyadhwu/abyadhwa* ) ni nomino yenye maana zifuatazo: 1. - enye rangi nyeupe, rangi ya maziwa au rangi ya barafu. (Silaha nyeupe *al-Silaahu al-Abyadhwu السلاح الأبيض* silaha nyeupe; visu na mapanga, usiku wa mbalamwezi *laylatun baydhwaa ليلة بيضاء* .) 2. Jambo lililotokea ghafla *mautun abyadhwu موت ابيض* kifo cha ghafla. 3. Weupe wa Alfajiri na miale yake *al-Khaytwu al-Abyadhwu الخيط الابيض.* 4. Mkono mweupe; neema, wema *al-Yadu al-Baydhwaa اليد البيضاء* (Katika Kiarabu nomino/kivumishi huzingatia jinsia. Hivyo neno *abyadhwu* linatumika kwa jinsia ya kiume na neno *baydhwaa* linatumika kwa jinsia ya kike.) 5. Mtu safi aliyeepukana na aibu *abyadhwul Wajhi أبيض الوجه* mwenye sura nyeupe/wajihi mweupe. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *abyadhwu ابيض*) llipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *abyadhi* maana yake inayohusu rangi katika Kiarabu haikubadilika na lilichukua dhana mpya ya Kete/karata isiyokuwa na alama yoyote inayotumika kwenye mchezo wa dhumna. Neno *ahamaru/ahamari* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino* : Rangi nyekundu. 2. *Kivumishi:* - enye rangi nyekundu; -ekundu, iliyo ya rangi nyekundu; -enye wekundu mwingi. 3. Kifo cha ghafla na cha kikatili. Kuna msemo: *mauaji ahmari* : kifo cha kikatili chenye kusababisha damu nyingi kumwagika. Neno hili *ahamaru/ahamari* (soma: *ahmaru/ahmara احمر* ) katika lugha ya Kiarabu lina maana ya: 1. Nomino: -enye rangi nyekundu; rangi ya damu. (Neno hili *ahmaru/ahmara احمر* lipo katika jinsia ya kiume. Neno la jinsia ya kike ni *hamraau حمراء* (soma: hamraa.) 2. Madini ya dhahabu. 3. Zafarani (ungaunga wa majani wenye rangi ya manjano au nyekundu ambao hutiwa kwenye chakula kuwa kiungo na pia kutengeneza wino, rangi ya manjano isiyo kali). 4. Mauaji/kifo cha kinyama *al-mautu al-ahmaru الموت الاحمر* (soma: *al-mautul* *ahmaru* ) kifo chekundu. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili *ahmaru/ahmara* lilipoingia katika Kiswahili maana zinazohusu rangi na kifo hazikubadilika. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |