ETIMOLOJIA YA MANENO ' ABTADI' na 'ABTALI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO ' ABTADI' na 'ABTALI' (/showthread.php?tid=1780) |
ETIMOLOJIA YA MANENO ' ABTADI' na 'ABTALI' - MwlMaeda - 12-19-2021 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' ABTADI' na 'ABTALI' Neno *abtadi* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino* : Shujaa wa vita. 2. *Kitenzi elekezi:* fanya jambo kwa mara ya kwanza ili wengine wafuate; tangulia, anza. 3. *Kitenzi elekezi:* *alika kitu au shughuli _* ninabtadi safari yangu kwa kumuomba Mola; Bismi - Llaahi n'abtadi_ *ninaanza kwa jina la Mwenyeezi Mungu.* Neno *abtali* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino* yenye maana zifuatazo: 1. Kwa mujibu wa *Kamusi Kuu ya Kiswahili* neno hili *abtali* lipo katika umoja na wingi wake ni *maabtali* . Neno hili *abtali* lina maana ya *askari au mpiganaji ambaye ni shujaa na mzoefu wa kupigana.* 2. Kwa mujibu wa *Kamusi ya Kiswahili ya Karne ya 21,* neno hili *abtali* ni nomino yenye maana ya *wapiganaji* . Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *abtadi* limetokana na kitenzi cha Kiarabu *abtadiu* *ابتدأ * kitenzi cha Kiarabu cha wakati uliopo cha nafsi ya kwanza *(ninaanza)* . Neno *abtali* , katika lugha ya Kiarabu ni wingi wa neno *batwalun بطل* lenye maana ya mshindi, shujaa. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *abtadiu أبتدأ*) llipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *abtadi* maana yake inayohusu kitenzi katika lugha ya asili - Kiarabu haikubadilika bali ikachukua dhana mpya ya *shujaa wa vita* (Kamusi Kuu ya Kiswahili). Ama neno *abtali*, ambalo katika lugha ya Kiarabu lina maana ya *washindi/mashujaa*, wakati *Kamusi Kuu ya Kiswahili* ikiliweka katika umoja ambao wingi wake ni *maabtali* wakilipa maana ya *askari au mpiganaji ambaye ni shujaa na mzoefu wa kupigana* , Kamusi ya Kiswahili ya Karne ya 21 imelitambua kuwa lipo katika wingi na imelipa maana ya *wapiganaji* badala ya ile maana yake katika lugha yake ya asili - Kiarabu ya *washindi/mashujaa.* *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |