ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABIRI' na 'ABIRIA' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABIRI' na 'ABIRIA' (/showthread.php?tid=1766) |
ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABIRI' na 'ABIRIA' - MwlMaeda - 12-18-2021 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABIRI' na 'ABIRIA' Neno abiri katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino* : Harufu nzuri inayonukia; manukato ya kupendeza. 2. *Kitenzi elekezi:* (i) fafanua jambo kwa vizuri, (ii) eleza jambo litakavyojiri; tabiri. 3. *Kitenzi si elekezi:* (i) safiri kutoka eneo moja kwenda jingine kwa kutumia chombo chochote cha usafiri. (ii) fanya safari kwa chombo cha majini. 4. *Kitenzi si elekezi:* elimika na jambo kwa kutumia mfano uliokwishatokea. (Visawe: tahadhari; jihadhari; kuwa mwangalifu.) 5. *Kitenzi si elekezi:* ingia katika chombo cha kusafiri, kwa mfano, meli, basi, mashua na kadhalika. Neno *abiria* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino* yenye maana ya: mtu anayetoka mahali fulani na kwenda pengine kwa kutumia chombo kwa mfano, basi, treni na kadhalika na ambaye si mfanyakazi wa chombo hicho. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *abiri* limetokana na vitenzi vya Kiarabu *abara* *عبر* na pia *abbara* *عبر* vyenye maana zifuatazo: 1. Amevuka (barabara au mto). 2. Amesafiri na chombo cha majini. 3. Amekufa/Amefariki/Ametawafu. 4. Amepita/Yamepita. 5. Ameieleza vyema habari fulani. 6. Amefasiri ndoto. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *abara* *عبر*) lilipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *abiri* , maana yake katika lugha ya asili - Kiarabu haikubadilika ingawa lilichukua baadhi za maana na kuacha maana zingine. Ama neno *abiria* , hili si neno halisi la Kiarabu bali ni matokeo ya usanifishaji na unyambulishaji wa neno *abiri* kutoka neno la Kiarabu *abara/abbara.* *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |