ETIMOLOJIA YA NENO 'HEKIMA' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO 'HEKIMA' (/showthread.php?tid=1748) |
ETIMOLOJIA YA NENO 'HEKIMA' - MwlMaeda - 12-15-2021 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO ' HEKIMA' Neno *hekima* katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana zifuatazo: 1. Maarifa, uwezo wa akili alionao mtu unaomuwezesha kufikiri kwa kina na kutoa uamuzi unaokubalika; busara. 2. Uwezo wa akili katika kutoa maamuzi kutokana na tajiriba na uzoefu wa muda mrefu. 3. Akili inayomuwezesha mtu kufikiri na kuweza kutoa uamuzi unaofaa. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *hekima* ( soma: *hikmatun/hikmatan/hikmatin* *حكمة* ) lina maana zifuatazo: 1. Uamuzi, *masdar* *مصدر* *tendo-jina* kutokana na *kitenzi* cha Kiarabu *hakama* *حكم* (ameamua/ametoa uamuzi). 2. Maarifa ya kujua kilicho bora zaidi kwa kutumia njia bora za kielimu; falsafa. 3. Taaluma ya kujua uhalisia wa mambo. 4. Uwezo wa kudhibiti nafsi na mihemko wakati wa kupandwa na ghadhabu/hasira. 5. Haki, uadilifu. 6. Sababu ya kutokea jambo fulani. 7. Maneno machache yenye maana kubwa na pana. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *hikmatun* *حكمة* ) lilipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa likawa *hekima* maana yake katika lugha yake ya asili - Kiarabu - haikubadilika ingawa imejifunga katika uwezo wa akili wa kufikiri na kutoa uamuzi unaofaa. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |