SHAIRI: NILETEENI TAULO - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: NILETEENI TAULO (/showthread.php?tid=1736) |
SHAIRI: NILETEENI TAULO - MwlMaeda - 12-12-2021 NILETEENI TAULO Inanikuta izara, dawatini nikiketi, Duara inanichora, katika yangu sketi, Hapo naificha sura, naaibika banati, Nileteeni taulo! Hunikosesha jubuni, wenzangu wananicheka, Hapo nakosa amani, kando nao kujiweka, Ninapokuwa hedhini, kweli ninaaibika, Nileteeni taulo! Haiachi kumwagika, nikisimama upesi, Vile inatiririka, ni damu sio kamasi, Kila mwezi ukifika, nahisi mwenye mkosi, Nileteeni taulo! Hunandama wavulana, na nyimbo kuniimbia, Huruma nao hawana, hawawezi kutulia, Kusoma jambo la mana, hedhi inanikosea, Nileteeni taulo! Nashindwa vema kusoma, yanifikavyo madhila, Masomoni ninakwama, nenda bwenini kulala, Kweli hedhi na kusoma, ni Kama lila na fila, Nileteeni taulo! Walimu huniadhibu, hudhania makusudi, Hali inanipa tabu, mie siye mkaidi, Hedhi inaniadhibu, masomo nyuma narudi, Nileteeni taulo! Enyi wafadhili wema, macho mnitupieni, Ninachoka kuwa wima, inijapo darasani, Nahofia kuchutama, sije toka hadharani, Nileteeni taulo! Serikali nanyi pia, hebu mnichinhuzeni, Hedhi yanitia doa, hasa niwapo shuleni, Kwenu leo ninalia, taulo nileteeni, Nileteeni taulo! Nimefika kaditama, ombi langu nalitua, Nami nibaki salama, nisome bila udhia, Mkinipa nitasoma, darasani tatulia, Niliteeni taulo! Mtunzi Filieda Sanga Mama B Mabibo Dsm 0753738704 |