MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
VIKOA VYA MAANA: UMUHIMU NA CHANGAMOTO ZAKE KATIKA KUELEZA MAANA YA MAANA - Printable Version
JIFUNZE KISWAHILI
VIKOA VYA MAANA: UMUHIMU NA CHANGAMOTO ZAKE KATIKA KUELEZA MAANA YA MAANA - Printable Version

+- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz)
+-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1)
+--- Forum: Sarufi na Utumizi wa lugha (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=9)
+--- Thread: VIKOA VYA MAANA: UMUHIMU NA CHANGAMOTO ZAKE KATIKA KUELEZA MAANA YA MAANA (/showthread.php?tid=1656)



VIKOA VYA MAANA: UMUHIMU NA CHANGAMOTO ZAKE KATIKA KUELEZA MAANA YA MAANA - MwlMaeda - 12-03-2021

Katika makala hii tujadili umuhimu wa vikoa vya maana katika semantiki, yaani kuonesha ni kwa namna gani vikoa vya maana vinaweza kufanikisha suala la kuendeleza taaluma ya semantiki ambayo hujihusisha zaidi na uchunguzi wa maana ya lugha ya binadamu. Pia tutaonyesha changamoto mbalimbali ambazo zinatokea wakati wa kuelezea maana ya maana. Kabla ya kujadili yote hayo ni vyema kwanza kujadili kwa ufupi maana ya vikoa vya maana pamoja na semantiki kutoka kwa wataalamu mbalimbali kusudi uhusiano na utofauti uliopo kati ya semantiki na vikoa vya maana.
Briton (2000) anaihusisha dhana ya vikoa vya maana na dhana ya hiponimia ambapo hiponimia ni uhusiano wa kiuwima ambapo fahiwa ya neno moja hujumuishwa katika fahiwa ya neno jingine  mfano fahiwa ya mgomba, mahindi, maharage zimejumuishwa katika mimea. Anahitimisha kwa kusema kuwa maneno katika vikoa vya maana huwa na sifa sawa zinazohusiana.
Wikipedia,  wanaeleza kuwa kikoa cha maana ni msamiati wa kiufundi katika taaluma ya isimu ambao unaelezea kikundi cha maneno yanayohusiana kimaana.
Dirk (2010) anaeleza kuwa vikoa vya maana ni jozi za maneno yenye maana zinazohusiana ambazo maana zake zinategemeana, na kwa pamoja zinatoa dhana ya kimuundo yenye uhalisia ndani yake.
Hivyo kikoa cha maana kinaweza kufasiriwa kuwa ni seti yeyote ile ya misamiati ambayo memba wake wanahusiana kiwima na kimlalo. Uhusiano kiwima tunaweza kusema kuwa ni namna maneno yanavyohusiana kiwima, na mlalo ni namna maneno  yanavyoweza kuvutana na maneno mengine yanayoelekeana nayo na kuleta maana.
Mifano ya vikoa vya maana nikama vile;  “Uandishi  wa kubuni” ambapo hujumuisha hadithi fupi, tamthiliya, ushairi na riwaya.
“Michezo”: ambapo hujumuisha; mpira wa miguu, mpira wa kikapu, kuruka kamba, mpira wa pete, mpira wa meza, mpira wa mikono.
“Nguo”: ambapo hujumuisha nguo za wanawake na nguo za wanaume. Nguo za wanawake: sketi, kanga, gauni, sidiria, blauzi.
Baada ya kujadili maana ya vikoa vya maana, ni vema pia kuangalia maana ya semantiki kabla ya kujadili umuhimu wa vikoa vya maana.
Kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2004) semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha ya binadamu, wanaendelea kusema kuwa maana hushughulikiwa katika viwango vyote vya lugha kama vile sauti, maneno na sentensi.
Hivyo tunaona kuwa vipengele muhimu katika lugha ya binadamu ni maana kwa sababu huweza kufanikisha suala la mawasiliano na upashanaji wa habari(ujumbe).
Umuhimu wa vikoa vya maana katika semantiki ni kama ufuatao.
Huonesha uhusiano wa maneno yenye sifa sawa au zinazoelekeana kimaana. Vikoa vya maana humsaidia mwanaisimu kutambua sifa za maana mbalimbali zinazohusiana kimaana kwani huwezi kuweka neno fulani katika kikoa fulani bila kujua sifa zinazotawala neno hilo. Mfano lazima ujue ndege na sifa zake ndipo utaje ndege wanaojenga hicho kikoa kama vile Kanga, Kuku, Njiwa, Bata, Mbuni na Kware.
Hurahisisha mchakato wa ujifunzaji lugha, husaidia kumueleza mtu anayejifunza lugha fulani husika ili kujua vitu mbalimbali vilivyowekwa katika makundi husika. Mfano  mtoto au mgeni wa lugha fulani huweza kujifunza dhana mbalimbali kupitia vikoa vya maana. Mfano watoto huweza kujifunza rangi mbalimbali hasa nyeusi na nyeupe kwa kupitia vikoa hivyo.
 Hurahisisha mawasiliano, yaani huokoa muda baina ya wazungumzaji, kwa mfano badala ya kutaja kitu kimoja kimoja basi unataja kwa ujumla wake endapo vinahusiana mfano, ukienda sokoni utauliza “una mboga za majani” utajibiwa kuwa kuna, mchicha, chainizi, spinachi, figili na matembele. Ilhali ilitakiwa mnunuaji amuulize muhudumu kwa kutaja jina mojamoja lakini yeye ametaja kwa ujumla na jibu limepatikana na ndipo huweza kutaja kikoa kimoja alichokitarajia.
Hufanya kazi ya kustawisha maana katika tungo au sentensi, utungo huwa na maana iliyojitosheleza kisemantiki(kimaana). Vikoa vya maana vinapotumika katika utungo huo hauwezi kustawisha maana  hata kama vitabadilishana nafasi na muda mwingine hupelekea hata maana ya awali kupotea lakini bado utungo utakuwa na maana. Vikoa hivyo vinaweza kujitokeza katika mfumo wa kiwima au kiulalo.
Mfano :
               (a)  paka amekula nyama yote.
               (b)  chui amekula nyama yote.
               ©  simba amekula nyama yote.
Maneno yaliyopigiwa mstari yamebadilishana nafasi kiwima lakini maana yake imebaki kama ilivyo na sentensi zimejitosheleza.
Hufanikisha shughuli za utunzi wa leksikografia, Mdee (2010), akimnukuu Wiegand anaeleza kuwa leksikografia ni shughuli au kazi ya kisanaa  inayojishughulisha na utunzi wa kamusi. Leksikografia hiyo hujishughulisha na ukusanyajin wa misamiati mbalimbali ya lugha na ndiyo inayosaidia kutungiwa kamusi. Na kamusi ni  kipengele cha kisemantiki kwa kuwa hutoa maneno yenye maana kwa watumiaji wa lugha na maneno hayo ndiyo vikoa vyenyewe vya maneno vyenye maana ambazo muda mwingine maana zake zaweza kuwa tofauti hatakama vikoa hivyo vinakuwa na maumbo sawa ya maneno. Mifano ya kamusi zenye vikoa vya maana ni kama vile;
              -kamusi ya wanyama
              -Kamusi ya mavazi
              -Kamusi ya tiba ya magonjwa
              -Kamusi za misuko ya nywele
              -Kamusi za vyakula
Kikoa kimoja husaidia kujua na kufafanua vikoa vidogo vilivyomo ndani ya vikoa vikubwa mfano kikoa cha vyakula: ugali, ndizi, viazi, ambapo kisemantiki humsaidia mtumiaji wa lugha kuteua kikoa mahususi kwa ajili ya matumizi yake kwa wakati huo.
Husaidia kuonesha umbo la wingi ambalo lina umuhimu kisemantiki hasahasa katika upatanisho wa kisarufi kwa mfano badala ya kusema ‘kikoa cha tunda” tunasema “kikoa cha matunda” “mnyama- wanyama” “mmea- mimea” hivyo basi vikoa hivyo vikitumika kwenye sentensi huwa matunda yameiva badala ya kusema Tunda yameiva, wanyamawanakimbia badala ya kusema wanyama anakimbia.
Vikoa vya maana vina sifa ya kuwa na maana ya kileksimu na kufanya kikoa kimoja kichanuze zaidi na kuweza kupata maneno mengine yenye maana kisemantiki. Mfano kuna kikoa cha masomo ya sayansi, biolojia, fizikia, kemia, kilimo. Kikoa cha biolojia huweza  hufasiliwa kuwa ni somo la kisayansi linalohusiana na viumbe hai na visivyo hai. Hivyo tunaona kuwa kikoa cha biolojia kimechanuza zaidi na kuleta maana ya kikoa hicho.
Changamoto ya vikoa vya maana katika kuelezea maana ya maana.
 Kuna baadhi ya vikoa havina idadi maalumu na vingine vina idadi maalumu, hii ni kutokana na ukweli kwamba vikoa kama vile vya siku za wiki , idadi ya miezi ya mwaka na siku katika mwezi huwa na idadi maalumu lakini vikoa vya maana vingine havina idadi maalumu mfano vikoa vya matunda, wanyama, mimea. Vikoa vya matunda,wanyama mimea na vinginevyo haviewezi kuwa na idadi maalum kwa kuwa vikoa vyake huweza kujitokeza kutegemeana na mazingira. Wanajamii watatoa majina ya vikoa hivyo baada ya aina fulani kutokea katika jamii yake na hivyo kuacha vionekani kutokuwa na idadi maalumu.
 Kuna baadhi ya vikoa ni changamani, hii ni kutokana na kwamba baadhi ya vikoa vya maana vinawakilisha dhana zaidi ya moja na hivyo kumfanya mtumiaji wa lugha apate utata wakati wa uainishaji wake.
Mfano: ndege kama mnyama, na ndege kama kifaa cha usafiri, pia mbuzi kama mnyama na mbuzi kama kifaa. Nyanya kama kiungo na nyanya kama mboga.
Hivyo basi vikoa hivi vya maana huweza kumchanganya mwanasemantiki na kushindwa kupata maana halisi.
Baadhi ya vikoa vya maana vinauhusiano wa karibu kiasi kwamba vinaweza kumchanganya mtu katika kutofautisha dhana mbili mfano Chui na Duma, Mbwa na Mbwa mwitu, Kuku na Kware.
Hakuna nadharia ya jumla inayohusika na upangaji wa vikoa hivi, hii inatokana na ukweli kwamba dhana hizi zipo vichwani mwa watu na kuandikwa kutokana na matumizi yake kimaana
Vilevile uainishaji unahitaji umakini zaidi katika upangaji wa vikoa kwani kuna uchomozi wa vikoa vingine, hii hutokea pale ambapo dhana moja mahususi huwa na dhana ndogondogo  ndani yake ambazo nazo huweza kusimama peke yake mfano kikoa cha binadamu tunapata wanaume na wanawake, ambapo ndani ya kikoa cha wanawake tunapata bibi kizee, shangazi, mama, msichana. Pia kikoa cha mwanaume tunapata babu, mjomba, Mvulana.
Vikoa vya maana hutofautiana kutokana na eneo na utamaduni, hii inamaana kuwa kila utamaduni fulani huweza kuwa na vikoa vitumikavyo katika mazungumzo yao ambavyo vinaweza kutofautiana na utamaduni wa jamii nyingine kutokana na aina na idadi ya vitu hivyo katika jamii fulani. Mfano kikoa cha ndizi katika utamaduni wa Wanyakyusa Tukuyu Mbeya kuna vikoa vya majina ya ndizi kama vile; malinda, matoki, mkono wa tembo, haradoni, kaambani na ndyali lakini katika jamii ya Wahaya huko Bukoba  kuna vikoa vya majina ya ndizi kama vile; shubili, majivu. Hivyo tunaona kuwa vikoa vya maana katika jamii ya wanyakyusa na wahaya hutofautiana.
Hivyo tunaweza kusema kuwa japokuwa kunachangamoto zinazokabili vikoa vya maana lakini vikoa hivyo vina umuhimu au mchango mkubwa katika kuendeleza taaluma ya semantiki kwa sababu wanasemantiki hufanya uteuzi mzuri wa maneno yenye maana kutoka akilini na kuyatumia katika mazungumzo na hivyo kufanya suala la mawasiliano liendelee kufanikiwa zaidi.
      MAREJEO
Brinton L. J (2000) The Structure of Modern English. A Linguistic intro Illustrated Edition. John  Benjamini Publishing company.
Dirk, G (2010) Theories of Lexico Semantics. Oxford University Press: New York.
Habwe, J na Karanja, P (2004) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Phoenix Publishers: Nairobi.
Mdee,J.S, (2010) Nadharia na Historia ya Leksikografia.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili: Dar es Salaam.