MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
SARUFI YA KISWAHILI NA SINTAKSIA - Printable Version
JIFUNZE KISWAHILI
SARUFI YA KISWAHILI NA SINTAKSIA - Printable Version

+- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz)
+-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1)
+--- Forum: Sarufi na Utumizi wa lugha (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=9)
+--- Thread: SARUFI YA KISWAHILI NA SINTAKSIA (/showthread.php?tid=1632)



SARUFI YA KISWAHILI NA SINTAKSIA - MwlMaeda - 12-01-2021

SARUFI YA KISWAHILI NA SINTAKSIA
Utangulizi wa kozi
Sarufi ya Kiswahili na sintaksia ni kozi inayochambua sarufi ya Kiswahili kwa kuzingatia nadharia za kisintaksia kama zilivyoasisiwa na wanazuoni wa isimu. Sintaksia ni tawi la isimu linalohusu mpangilio na mfuatano wa vipashio vya lugha katika kuunda tungo za darajia mbalimbali, huchunguza mathalan namna maneno yanavyounda virai na sentensi za Kiswahili. Sintaksia inahusu tungo za lugha ambazo zaweza kuwa ni maneno, virai, vishazi na sentensi. Japokuwa neno ni kipashio cha kiumbo, linasadifu kuingia katika sintaksia ya lugha kwani lenyewe lina muundo wake unaotokana na viambajengo vinavyoliunda ambavyo ni mzizi na viambishi.
Baada ya ufafanuzi huo kwa kifupi sasa unakaribishwa kwenye somo lenyewe. Ni imani yangu kuwa utalifurahia na kulipenda na hatimaye kulifaulu vizuri somo hili.
MAANA YA LUGHA NA SARUFI
Lugha ni nini?
Dhanna ya lugha ni pana sana, hata hivyo kimuundo lugha inafafanuliwa kama “Mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa na watu ili kupashana habari.”
Hammerley, 1982:26 anasema; Lugha ni mfumo wa mawasiliano wenye ishara za kinasibu, mfumo ambao ni tata, kamilifu na unaobadilika. Mfumo huo humudiwa na hutumiwa na wanajamii wenye utamaduni maalumu.
Kutokana na fasili hiyo tunapata mambo saba ya msingi kuhusu lugha:
  1. Lugha ni kamilifu; Lugha ni kamilifu kwa kuwa inahimili matakwa ya jamii kimawasiliano. Kila jamii hutosheka inapotumia lugha yake kuelezea hisia zake kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi pamoja na matakwa mengine ya kijamii. Panapotokea dhanna mpya lugha hujiongezea msamiati kwa njia mbalimbali.
Mfano:
(a)    Antena, kompyuta, jokofu.
(b)    Mofolojia, hisabati, elimu
©    Demokrasia, vyama vingi, mgombea
  1. Lugha ni tata; Kisintaksia lugha ni tata kwa sababu inaundwa na vipashio vidogo ambavyo huweza kubainishwa katika viwango mbalimbali kama vile; fonimu ambazo huunda mofimu, mofimu huunda maneno, maneno huunda virai, virai huunda vishazi na vishazi huunda sentensi.
Mfano:
(a)    Sentensi 1: Mtoto anaomba maziwa
(b)    Maneno:  3: Mtoto + anaomba + maziwa
©    Mofimu   7: M + toto + a + na + omb + a + maziwa
(d)    Fonimu  18: M + t + o + t + o + a + n + a + o + m +
           b + a +m + a + z + i + w + a
 Vipashio vyote hapo juu hushonana kwa kanuni maalumu
 ambazo hutofautiana kati ya lugha na lugha.
  1. Lugha hubadilika; Lugha hupokea mabadiliko kulingana na mahitaji ya jamii kwa wakati husika. Baadhi ya maneno hutoweka katika matumizi na misamiati mipya huibuka na mingine hubadili maana ya awali.
Mfano:
(a)    Kichele
(b)    Kutesa kwa zamu
©    Buzi
(d)    Nyambizi, nk
Mabadiliko ya lugha pia huweza kujitokeza kisarufi ingawa si kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa msamiati.
Mfano:
(a)    Mambo iko huku (yako)
(b)    Khabari (habari)
©    Sawabu (thawabu)
(d)    Zambi (dhambi)
  1. Lugha ina mfumo; Lugha ni matokeo ya mfumo ambao hujibainisha katika kiwango cha muundo na pia maana.
(i)         Kiwango cha muundo (sintaksia); Lugha ina utaratibu maalumu wa mfuatano wa maneno (mofolojia) na mshonano wa sauti (fonolojia). Katika kiwango hiki mpangilio wa vipashio husimamiwa katika namna inayokubalika ili vilete maana inayokubalika au iliyokusudiwa.
Mfano: – Mdogo baba analima shamba (sio
 sahihi)
–   Baba mdogo analima shamba (sahihi)
(ii)       Kiwango cha maana; Kiswahili kwa mfano kina namna ya kupambanua maana za maneno kwa njia mbalimbali. Mathalan Upambanuzi wa maneno kwa njia ya kutoa maana iliyo kinyume cha maneno ya awali.
Mfano:
(a)    Refu – fupi
(b)    Funga – fungua
©    Nene – embamba
(d)    Zito – epesi
  1. Lugha hasa ni ya mazungumzo; Uasilia wa lugha ni mazungumzo tangu mwanadamu alipoanza kutumia lugha kuwasiliana. Lugha hutegemea sauti za kutamkwa toka kinywani mwa mwanadamu kwa kutumia ala za sauti. Lugha ya mazungumzo maneno yake hubeba maana nyingi na pana sana kuliko yakiwa katika maandishi. Ni dhahiri kuwa maandishi ni namna tu ya kuwasilisha yale yote yaliyo katika mazungumzo. Wapo watu wengi ambao humudu lugha ya mazungumzo lakini hawawezi kuandika lugha hizo.
  2. Lugha humudiwa/hufunzwa; Pamoja na ukweli kwamba kila mtu anapozaliwa huzaliwa na uwezo wa kumudu lugha, uwezo huo ni sawa na uwezo mwingine tu kama kuendesha gari, kunyonya, kutambaa au kutembea. Kila mwanadamu hupaswa kutumia uwezo alionao kujifunza na kuimudu lugha yake kama ilivyo kwa mambo mengine. Juhudi hizi huanzia pale mtu anapojifunza lugha yake ya kwanza katika jamii inayomzunguka.
–   Baada ya kumudu lugha ya kwanza mtu huyo huweza kujifunza lugha ya pili akiwa shuleni au kupitia njia zozote za mawasiliano.
  1. Lugha hufungamana na utamaduni wa jamii; Kila lugha hueleza mambo yanayoihusu jamii yake kwa wakati wote wa historia ya jamii hiyo. Hivyo lugha na utamaduni ni vitu visivyoweza kutenganishwa. Kwa mantiki hii kumbe kuijua lugha kunahitaji ujuzi wa utamaduni wa wanalugha husika. Hii ni kwa sababu maneno ya lugha hubeba vionjo vya wanalugha na huambatana na ishara na maana mbalimbali zinazofungamana na utamaduni wa jamii husika.
         Kwa mfano:
–   Mchele kwa mswahili
–   Migomba kwa mchaga/mhaya
–   Samaki kwa mpare,n.k
LUGHA KAMA MFUMO BUNIFU
Uwezo wa kuimudu lugha uko katika sehemu ya ubongo na hushamirishwa na jamii ya wazungumza lugha ambao humsaidia mtu kuimarisha uwezo huo. Kuimarika uwezo wa kumudu lugha huongezeka kutokana na ujuzi anaoupata mwanadamu katika harakati za kupambana na mazingira yanayomzunguka.
Kila mtumia lugha hubuni lugha inayokidhi mazingira fulani. Hivyo lugha hubuniwa wakati wote na ubunifu huu hutofautiana kati ya lugha moja na ingine.
Kwa mfano:
(a)    Soma: somo,kisomo,usomaji,msomi,masomo
(b)    Jibu: kujibu,majibu,
©    Lima: kilimo,mkulima,mlimaji
Katika mifano hiyo msemaji ametumia mbinu gani kuunda msamiati huo?
DHANNA YA SARUFI
Sarufi ni mfumo wa taratibu na kanuni zinazomuongoza mtumiaji wa lugha ili aweze kuitumia lugha yake kwa usanifu na ufasaha.
  Ni uwezo wa wazungumzaji wa lugha kuunda na kufasili kanuni za usahihi au kutokuwa sahihi kwa maneno au sentensi za lugha yao. Sarufi kwa ujumla inajumuisha vipengele vya lugha kama vile: fonetiki, fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki.
SIFA ZA JUMLA ZA KISARUFI
  1. Lugha zote zina sarufi; kila lugha duniani inatawaliwa na sarufi ingawa sarufi za lugha hutofautiana.
     Mfano:
    Kiingereza
  • The two boys now see several dogs
  • This boy is incredible
 Kiswahili
  • Boys two see now dogs several
  • Vijana wawili sasa wanaona mbwa wengi
  • Boys two see dogs several
  • Sasa vijana wawili wanaona mbwa wengi
  • This boy is incredible
  • Huyu kijana ni mkorofi (sio sahihi)
  • Kijana huyu ni mkorofi (sahihi)
Kwa mifano hiyo ni dhahiri kuwa kila lugha ina sarufi yake na haiwezekani sarufi ya lugha fulani ikawa ndio msingi wa sarufi za lugha nyingine.
  1. Sarufi za lugha hufanana; sarufi za lugha hufanana ingawa ndani ya lugha moja jambo fulani huweza kuelezwa kwa namna tofauti. Utofauti huo haumaanishi namna fulani ni bora zaidi ya ingine. (rejelea mifano ya hapo juu).