ISTILAHI ZA SARUFI YA LUGHA YA KISWAHILI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Sarufi na Utumizi wa lugha (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=9) +--- Thread: ISTILAHI ZA SARUFI YA LUGHA YA KISWAHILI (/showthread.php?tid=1605) |
ISTILAHI ZA SARUFI YA LUGHA YA KISWAHILI - MwlMaeda - 11-28-2021 ISTILAHI ZA SARUFI YA LUGHA YA KISWAHILI.
Ø Alomofu
Mojawapo ya viwakilishi viwili au zaidi vya mofimu moja ambavyo hujitokeza katika mazingira tofauti ya mtoano. Haya ni mazingira ambamo kiwakilishi kimoja tu hujitokeza na si kingine cha dhana hiyo. Mathalani katika lugha ya Kiswahili mofimu
–MU- huwa inajitokeza katika maumbo ya maneno kamainavyoonekana hapa chini:
Vipashio M, MW, na MU vyote ni viwakilishi vya MU katika mazingira tofauti. Hii ina maana kwamba m,mw na mu ndizo alomofu au viwakilishi vya mofimu mu katika mazingira ya maumbo yanayoanza na konsonanti na yale yanayoanza na irabu. Hakuna mifano katika lugha hii ambako viwakilishi hivyo vinabadilishana nafasi katika mazingira hayo. Hii ndiyo hufanya mazingira hayo yaitwe mtoano.
Ø Irabu
Ni aina ya sauti ya lugha inayotamkwa bila kuwepo na kizuizi chochote kwenye mkondo wa hewa kutoka mapafuni kupitia kinywani na/au puani.
Mfano wa irabu ni. a,e,i, o,u.
Ø Mofimu
–Ni kipashio kidogo kabisa chenye uamilifu katika umbo la neno. Tunapozungumzia uamilifu tuna maana ya jukumu/wajibu/kazi/dhima. Mfano. mofimu “li, na, ta” katika maneno, alikuwepo, anaongea, ataingia zinaonesha dhima ya kutaja wakati/ njeo.
Ø Mofu
_Kipashio cha kimaumbo kinachowakilisha mofimu. Katika Kiswahili mfano wa mofu yenye viwakilishi vya kimatamshi na kimaandishi ni kama huo uliooneshwa katika (4) hapa chini ambapo mofu moja inawakilisha mofimu mbili (2)
4 (a) taa-chombo kinachowashwa ili kutoa mwanga
(b) taa-aina ya samaki.
Katika (4), tunaona mfano wa mofu yenye fonimu tatu za kimaandishi, yaani herufi t-a-a. Mofu hii inawakilisha mofimu mbili kama ilivyooneshwa katika 4 (a) na (b).
Ø Mzizi
Umbo-msingi la neno ambalo haliwezi kuchanganuliwa tena katika sehemu nyingine ndogo bila kupoteza uamilifu na utambulisho wake wa kisemantiki. Mfano. -l-, -chez-, -og- ni mizizi katika. maneno kula/mlo, mchezo, wanaoga. Zipo aina kuu nne za mzizi ambazo ni mzizi asilia, mzizi wa mnyambuliko,mzizi huru na mzizi funge. (Kuhusu mzizi asilia na mzizi wa mnyambuliko, rejea maelezo ya awali)
Mzizi huru:
Ni mzizi ambao unajitegemea, yaani unaweza kusimama peke yake na ukaleta maana ya wazi. Nomino nyingi ni za namna hii, kama meza, kabati, giza n.k. lakini kuna aina nyingine za maneno ambazo pia zina mzizi huru kamasahau, saini, keti, hiari, tahadhari n.k.
Mzizi funge:
Ni mzizi ambao hauwezi kusimama peke yake na ukaleta maana ya wazi . kama. –pig-, -kat-, -som- (n.k).
Ø Silabi
Ni sehemu ya neno ambayo huweza kutamkwa mara moja na kwa pamoja kama fungu moja la sauti. Ifuatayo ni mifano ya silabi katika maneno. A-gha-la-bu, we-nda-wa-zi-mu, u-si-ni-fu-a-ti-li-e, u-m-fya-tu-li-e., m-zu-ri, si-ta-ku-a-cha. Ukiona kipande chochote ambacho hakitamkiki kwa sauti moja, jua hakina sifa ya kuitwa silabi. Kuna aina kuu mbili za silabi:
Ni silabi ambayo huishia na konsonanti na ambayo haina kilele cha msikiko au mvumo mfano: m, n (mtu, nta) .
Ni silabi ambayo huishia na irabu au kama ni konsonanti peke yake basi yenyewe itakuwa pia ni kilele cha msikiko au mvumo wa sauti.( Ikumbukwe kuwa silabi zina sifa ya kifonolojia hivyo hutambulika zaidi kwa kuzitamka na kuzingatia mafungu ya sauti)
Ø Sarufi Maumbo/mofolojia
– Ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchanganuzi wa kanuni na mifumo inayohusu upangaji wa mofimu mbalimbali kuunda maneno katika lugha.
Ø Sarufi Miundo/sintaksia
Ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchanganuzi wa taratibu na kanuni zilizopo baina ya maneno katika lugha.. Sintaksia huangalia zaidi mpangilio na mfuatano wa maumbo ya maneno katika kutoa taarifa iliyokusudiwa.
Ø Sarufi maana /umbo maana/semantiki
Ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchanganuzi wa taratibu na kanuni za maana ya maneno na tungo katika lugha. Umbo la neno hukubalika kisarufi iwapo lina maana, hivyo ni kazi ya semantiki kuhakiki maana za maneno.
Ø Sarufi matamshi/umbo sauti/fonolojia
Ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchanganuzi wa sauti za lugha.
Ø Unyambulishaji/unyumbulishaji
Upachikaji wa viambishi kwenye mzizi ili kujenga neno. Mfano. mzizi.-pend- unakuwa.-pendo, upendo, pendana, wapendanao.
Ø Shina
Ni sehemu ya neno lenye mzizi na viambishi tamati. Mfano: nitamfungashia =fung-mzizi; fungash-shina.
Ø Isimu
Ni sayansi ya lugha/taaluma ambayo hujishughulisha na uchambuzi wa vipengele mbalimbali vya lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi.
Ø Chagizo
Ni nafasi inayojazwa na maneno yanayoeleza zaidi kuhusu tendo.Hivyo chagizo ni kikundi (kirai) kielezi kinachopatikana katika kiarifu na ambacho huweza kudondoshwa na bado sentensi ikabakia na maana ya msingi.
Ø Kijalizo
Ni maneno yote ambayo hutokea katika sentensi ili kutoa taarifa ya ziada. Maneno hayo huweza kufutwa na sentensi ikabaki na maana ya msingi.
Ø Kiambishi
Ni kipashio cha neno ambacho hupachikwa kabla, au baada ya mzizi wa neno.( Lugha ya Kiswahili haina kiambishi ambacho huchopekwa ndani ya mzizi, viambishi hivi vipo katika lugha ya Kiebrania, Kiingereza, n.k)
Ø Kiarifu
Ni sehemu ya sentensi ambayo kiini chake ni tendo linalotendwa; mojawapo ya sehemu kuu mbili katika sentensi, nyingine ikiwa ni Kiima. Katika usemaji wa kawaida wa Kiswahili kiarifu huja baada ya kiima.
Ø Kiima Kiarifu
Ni aina ya uhusiano katika muundo baina ya mtendaji wa tendo na tendo lililotendwa.
Ø Kiimbo
Ni umbo la sauti linalotokana na jinsi sauti inavyopanda na kushuka katika usemaji.
Ø Shada
Ni mkazo unaowekwa silabi ya pili toka mwisho katika lugha ya Kiswahili.
Ø Kirai
Ni mpangilio wa neno au maneno wenye neno kuu moja.Mahusiano kati ya neno kuu na maneno mengine ndiyo hutupatia aina ya kirai. Yaani kama neno kuu ni nomino basi tunapata kirai nomino,(n.k)
Ø Kishazi
Ni tungo yenye kitenzi kinachojitosheleza kitaarifa au kisichojitosheleza kitaarifa. Kitenzi kinachotoa taarifa kamili hutoa kishazi huru na kile kilichoshushwa hadhi hutoa kishazi tegemezi.
Ø Konsonanti
Kitamkwa ambacho utamkaji wake huathiriwa na kuzuiwa kwa hewa ambayo ama inatoka mapafuni au inaingia ndani, kama /g / , /m/ ,/k/, /b/, /s/, / f/
Ø Nadharia
Taratibu, kanuni na misingi iliyojengwa kwa mawazo kwa madhumuni ya kuwa kigezo cha kuelezea jambo au mambo kadhaa.
Ø Krioli
Mchanganyiko wa maneno na vipengele vya lugha mbili (au zaidi) tofauti ambao umekomaa na kuunda lugha ya mawasiliano kati ya wazungumzaji ambao hapo awali walikuwa na lugha zao tofauti. Kwa kawaida krioli hutokana na pijini. Tofauti ya krioli na pijini ni kwamba wakati hiyo iliyotajwa mwanzo huwa ina sarufi kamilifu na msamiati mahsusi, hiyo ya pili huwa haina kitu kama hicho.
Ø Lahaja
Mojawapo kati ya lugha ambazo kusema kweli huhesabika kama lugha moja isipokuwa zinatofautiana katika baadhi ya vipengele fulani fulani, kama vile lafudhi, fonolojia, msamiati usiokuwa wa msingi au miundo, (Ni tofauti ya usemaji miongoni mwa jamii ya watu wanaosema lugha yenye asili moja). Lugha ya Kiswahili ina lahaja nyingi , na Kiswahili sanifu ni mojawapo ya lahaja hizo. Kuna
Lahaja Rasmi=lahaja ambayo imekubaliwa kutumiwa katika mazingira au muktadha rasmi.
Lahaja Sanifu=lahaja ambayo imesanifiwa ili iweza kutumika katika mawanda mapana zaidi na kwa shughuli mbalimbali zilizo rasmi na zinazoihusu jamii ambyo lugha yake ina lahaja nyingi.
Ø Lugha chotara
Ni lugha ambayo imetokana na mchanganyiko wa lugha mbili au zaidi.
Ø Lugha sanifu
Ni lugha ambayo imekubaliwa kutumika katika shughuli za kielimu na ambayo inakubaliwa kimatumizi na wasemaji wengi zaidi.
Ø Lugha za kibantu
Ni baadhi ya lugha za kiafrika ambazo zasemekana zilitokana na lugha mama moja. Lugha hizi zilipewa jina la lugha za kibantu na W. BLEEK, mwanaisimu mmoja wa Kijerumani aliyefanya utafiti wa muda mrefu kusini mwa jangwa la Sahara. Alizipa lugha hizo jina hilobaada ya kugundua kwamba zote zilikuwa zinatumia neno Bantu (au pengine wantu, vantu, Batu, antu,watu, anhu, Banhu n.k.) kwa maana ya watu. Lugha za kibantu hujibainisha kwa kuwa na utaratibu wa kuziweka nomino zake katika ngeli mbalimbali na kila ngeli kuwa na viambishi vyake.
Ø Prediketa
Katika sarufi ya kimapokeo hii ni sehemu mojawapo kati ya sehemu kuu mbili zinazojenga sentensi.Kwa mujibu wa mtazamo huu sentensi ina kiima, kwa upande mmoja na prediketa kwa upande mwingine.Kiima huhusu mtendaji wa tendo na maneno mengine yanayoambatana nacho, na prediketa huhusu tendo na maneno mengine yanayoandamana nalo.
Ø Sentensi
Kipashio kikubwa kabisa cha kimuundo chenye kuleta maana kamili. Ni tungo yenye muundo wa kiima na kiarifu inayotoa taarifa kamili. Aina zake ni sentensi sahili, sentensi changamano, sentensi ambatano, sentensi shurutia.
Ø Tungo
Ni kipashio cha kimiundo ambacho ni matokeo ya uwekaji pamoja vipashio sahili ili kujenga kipashio kikubwa zaidi. Aina zake ni: tungo neno, tungo kirai, tungo kishazi, tungo sentensi,
Ø Yambwa
Ni nomino inayodokeza mtendwa upande wa kiarifu.
Ø Yambiwa
Ni nomino inayodokeza mtendewa katika sentensi upande wa kiarifu.
Ø Upatanisho wa kisarufi
Ni kuwiana kwa viambajengo vinavyounda sentensi kama kitenzi, kivumishi, kielezi na maneno yanayohusiana nayo katika sentensi au tungo.
Ø Othografia
Ni mfumo wa maandishi unaotumiwa katika lugha fulani; unaweza kuwa wa alama au michoro.
Ø Radidi
-enye kurudiwa rudiwa
Ø Lafudhi
Sifa ya msikiko wa sauti ya msemaji ambayo humpa utambulisho fulani katika jamii au eneo la kijiografia analotoka.
Ø Alasauti
Sehemu ya viungo katika kinywa cha binadamu vitumikavyo katika utoaji wa sauti za lugha. Mfano: ulimi, kaakaa gumu, kaakaa laini, meno, fizi, midomo (n.k.)
Ø Alofoni
Umbo lingine la fonimu ileile moja/ maumbo tofauti ya fonimu moja. Mf. Shahani badala ya Sahani, suri badala ya zuri, fiatu badala ya viatu.
Ø Fonimu
Vitamkwa vinavyoweza kujenga maneno yenye maana tofauti au vinavyoweza kubadili maana za maneno. Mfano wa fonimu ni: /m/, /z/, /u/, /ng/ /u/ katika neno mzungu.
|