MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
Lugha ya mazungumzo haina muundo rasmi? - Printable Version
JIFUNZE KISWAHILI
Lugha ya mazungumzo haina muundo rasmi? - Printable Version

+- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz)
+-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1)
+--- Forum: Sarufi na Utumizi wa lugha (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=9)
+--- Thread: Lugha ya mazungumzo haina muundo rasmi? (/showthread.php?tid=1549)



Lugha ya mazungumzo haina muundo rasmi? - MwlMaeda - 11-23-2021

Lugha ya mazungumzo haina muundo rasmi?. Huku ukijikita katika nduni za lugha ya mazungumzo, jadili kauli hii.


Katika kujadili swali hili, tutaanza kujadili nini maana ya lugha kwa mujibu wa wataalam mbalimbali, pia tutatoa maana ya lugha ya mazungumzo, maana ya muundo rasmi na hatimaye tutaingia katika kiini cha swali ambapo tutakubaliana na swali kwa kutumia uthibitisho wa nduni (sifa) za lugha ya mazungumzo jinsi zinavyofanya lugha ya mazungumzo isiwe na muundo rasmi. Yaani tutaangalia ni kwa vipi sifa za lugha ya mazungumzo zinavyopelekea lugha ya mazungumzo kukosa sifa ya kuwa na muundo rasmi. Na mwisho tutatoa hitimisho.
Massamba (2009) anaeleza kuwa, lugha ni mfumo wa sauti nasibu ambazo zimekubaliwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano yao.
Mgullu (1999) kama alivyomnukuu Trudgil (1974) anafafanua kuwa, lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani wenye utamaduni wake.
Kwa ujumla tunaweza kusema kwamba, lugha ni mfumo wa sauti nasibu ambazo zimebuniwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano miongoni mwao.
Dhana yingine tuliyoiangalia kulingana na swali hili ni lugha ya mazungumzo. Kwa mujibu wa Wikipedia, wanasema lugha ya mazungumzo ni utaratibu wa kuongea baina ya pande mbili, kwa kawaida wahusika ni watu. Lugha ya mazungumzo huwa na mitindo mbalimbali kama vile rejesta, misimu, jagoni na agoti.
Kisha tukaangalia dhana ya muundo, kwa mujibu wa Concise Oxford Dictionary (2001) (toleo la 10) muundo ni mpangilio na uhusiano wa vitu katika kuunda kitu kizima;
Katika muktadha wa mazungumzo, muundo rasmi ni ule mpangilio unaohusisha kanuni na taratibu zilizowekwa katika uzungumzaji ambapo kila mzungumzaji hana budi kuzingatia wakati wa mazungumzo.
Vilevile tunapozungumzia muundo rasmi katika lugha huangalia mpangilio wa maneno na muundo wa sentensi na namna maneno na sentensi hizo zinavyopangiliwa na kuleta mtiririko wenye maana na uliokamilika na unaoweza kueleweka na watu wote.
Kutokana na fasili hii lugha ya mazungumzo haina muundo rasmi, hii ni kwa sababu haizingatii vigezo hivyo wakati wa uzungumzaji na hivyo kuonekana kutokuwa na muundo rasmi na hii ndiyo sifa mojawapo kati ya sifa zinazojidhihirisha katika lugha ya mazungumzo.
Hivyo basi tunaweza kuthibitisha kauli hii kwamba, lugha ya mazungumzo haina muundo rasmi kwa kujikita katika sifa au nduni za lugha ya mazungumzo kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa King’ei (2010), anaorodhesha sifa zinazojitokeza katika lugha ya mazungumzo ambazo ni kama ifuatavyo;
Ubadilikaji wa kila mara wa maudhui, na uteuzi usiotabirika wa maneno, kauli au usemi. Hivyo katika sifa hii tunaona kwamba hakuna muundo rasmi kutokana na kwamba mzungumzaji ana uteuzi wa maneno na kauli zisizotabirika, hivyo anaamua mwenyewe nini cha kusema bila kufuata muundo au kanuni zozote. Mfano anaweza kuanza na aina yoyote ya neno katika sentensi.
Utokezaji wa makosa wa aina tofauti katika mazungumzo, mfano kukosea matamshi, kusitasita, kusahau baadhi ya maneno, kuchanganya hoja, wazungumzaji kusema kwa pamoja na hivyo kupoteza uzi au mtiririko sahihi wa mazungumzo. Jambo hili hutokea kutokana na kukosekana kwa muundo rasmi unaowaongoza wazungumzaji. Kimsingi muundo rasmi hufuata kanuni madhubuti na utokeaji wa makosa haupo kwa sababu ya urasmi wake.
Pia kuwepo kwa uradidi / marudio na msisitizo kwa wingi katika mazungumzo na pia mazungumzo kukatishwa kwa vichekesho, miguno ama matumizi ya lugha ya ishara, hali hii hutokana na kutokuwepo na muundo maalum unaomwongoza mzungumzaji, ndiyo maana wazungumzaji hujikuta wakirudia rudia maneno wakati wa mazungumzo.
Masahihisho ya kila namna na pia ufafanuzi na maelezo hutolewa mara kwa mara pale utata unapotokea. Hii ni kwa sababu ya kutokuwepo kwa muundo maalum kama vile mpangilio wa mawazo, sentensi na mtiririko wa mawazo katika mada ndivyo vinapelekea kutokea kwa utata na kusababisha masahihisho ya mara kwa mara.
Matumizi ya sentensi fupi fupi, sentensi za neno moja moja au maneno yasiyokamilika hutokea kwa wingi katika mazungumzo pindi mzungumzaji anapozungumza kwa huweza kutumia sentensi fupi fupi, au kutumia maneno yasiyokamilika. Yote hii hutokana na kutokuwepo kwa muundo rasmi wa lugha ya mazungumzo. Katika hali ya muundo rasmi hauruhusu udondoshaji wa maneno au tungo au matumizi ya sentensi fupifupi ambazo hazijajitosheleza.
Msamiati mwepesi na unaofahamika kwa urahisi, pindi mzungumzaji wa lugha anapoongelea mada fulani mbele ya hadhira yake huangalia mandhari pamoja na uhusiano baina yake na wasikilizaji wake, hivyo anaweza kubadilika kulingana na hali halisi anayokutana nayo. Hii haijidhihirishi katika muundo rasmi kama vile lugha ya maandishi, mwandishi hazingatii muktadha au uhusiano baina yake na wasomaji wake, yeye huandika kazi yake bila kujua watakaosoma ni akina nani. Hivyo basi ubadilikaji huu wa msamiati kulingana na hadhira ya mzungumzaji unatuthibitishia kwamba lugha ya mazungumzo haina muundo rasmi.
Vilevile kuna uvunjaji wa kanuni za sarufi na matumizi sanifu kutegemeana na uhusiano wa wazungumzaji, katika lugha ya mazungumzo hakuna kanuni ambazo zinamfanya/kumbana mzungumzaji, hivyo basi kwa sababu ya kutokuwepo kwa kanuni hizo ni wazi kwamba lugha hii haitakuwa na muundo rasmi unaomuongoza mzungumzaji ndiyo maana mzungumzaji hujikuta akivunja kanuni. Mfano; mtu anaweka viambishi sehemu ambayo haihitajiki kiambishi kama vile neno nilikuwepo – nilikuwepogi, alimpaga au hakunaga. Pia wapare husema thatha ni thaa thaba kamili wakimaanisha kuwa sasa ni saa saba kamili. Vilevile Wahaya husema ngombe badala ya ng’ombe.
Pia katika lugha ya mazungumzo hakuna muda au nafasi ya kufikiria jambo lakuzungumza, hapa mzungumzaji hana muda wa andalio la anachotaka kusema, hutamka tu bila kufikiria jambo analotamka. Jambo hili la kutokuwa na muda wa kujiandaa ndilo hupelekea kutokea kwa miguno na makosa ya kimantiki. Lakini katika muundo rasmi mambo haya huwa hayajitokezi kwa sababu kuna maandalizi ya kutosha.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, muundo wa lugha ya mazungumzo hauwezi kujidhihirisha moja kwa moja kwa watumia lugha isipokuwa huweza kuhusisha utaratibu fulani unaozingatia mada, muktadha na mahusiano ya wazungumzaji. Aidha hoja inasisitiza kuwa hakuna mada rasmi zilizozoeleka na zinazotumika na watu wote, vivyo hivyo kwa muktadha na mahusiano. Pia lugha hiyo haiwezi kuwa na mpangilio maalum wa kile kinachozungumzwa na maelezo yake kwa wazungumzaji baina yao.
MAREJEO:
Smith, T. (2001). Concise Oxford English Dictionary. (10th Edt). Oxford University Press. UK.
King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimujamii. Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Chuo Kikuu                                       cha Dar es salaam.
Massamba, D.P.B. (2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha.TUKI, Dar es Salaam.
Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Longhornpublishers. Ltd. Nairobi