Tunajifunza nini vita dhidi ya Kiswahili shuleni? - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: Tunajifunza nini vita dhidi ya Kiswahili shuleni? (/showthread.php?tid=1524) |
Tunajifunza nini vita dhidi ya Kiswahili shuleni? - MwlMaeda - 11-20-2021 MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Tunajifunza nini vita dhidi ya Kiswahili shuleni?
Kwa ufupi
Na. Erasto Duwe
Kiswahili ni lugha ya Taifa na lugha rasmi nchini Tanzania; hutumika kama chombo cha kuelezea, kubeba na kuutangaza utamaduni wetu kitaifa na kimataifa.
Kwa upande mwingine, Kiingereza ni lugha itumikayo kufundishia katika shule za msingi zitumiazo mfumo wa Kiingereza, sekondari na vyuo nchini Tanzania.
Ni wazi kwamba, wanafunzi hawana budi kuzifahamu ipasavyo lugha hizi. Kwa sababu ya nafasi yake, Kiswahili hakina budi kufundishwa kwa umahiri mkubwa ili wanafunzi wakifahamu ipasavyo. Kiingereza pia kifundishwe kwa ustadi na maarifa kwa kuwa ndiyo lugha itumikayo kufundishia masomo yote katika viwango hivyo vya elimu.
Ikiwa lugha hiyo haifundishwi ipasavyo, ni dhahiri kuwa uelewa wa watoto katika masomo yao utakuwa finyu.
Ukibahatika kutembelea shule za msingi zitumiazo mfumo wa Kiingereza, na sekondari, utakutana na mabango yaliyotundikwa sehemu mbalimbali yakiwa na maneno haya: ‘Speak English only’ (zungumza Kiingereza tu), “No English, no service” (usipotumia Kiingereza, huhudumiwi).
Yawezekana lengo la kuwa na kaulimbiu hizi katika mazingira hayo ni kusisitiza matumizi ya Kiingereza kwa wanafunzi, kwa kuwa ndiyo lugha itumikayo kufundishia. Kinachosikitisha ni namna Kiswahili kinavyobezwa katika muktadha wa usisitizaji wa matumizi ya Kiingereza kwa wanafunzi.
Katika shule moja, niliwahi kushuhudia mwalimu wa Kiingereza Mtanzania akisema kwa kejeli, “What is Swahili? It’s the language of uncivilized people in the street…” (akimaanisha Kiswahili ni lugha ya watu wasiostaarabika…). Nilishikwa na bumbuazi kwani huyo aliyesema hivyo akiwa darasani; nje alitumia Kiswahili muda wote.
Ofisa mmoja wa taaluma, alishuhudia kioja katika shule fulani ya sekondari. Alipoingia katika geti la shule hiyo, aliona bango kubwa linalosisitiza matumizi ya Kiingereza. Baadaye alibahatika kuingia katika darasa fulani.
Mbele darasani humo, mlikuwa na bango kubwa lililokuwa na maneno, ‘Speak English only’ ilhali nyuma ya darasa hilo hilo mlikuwa na ubao wenye maneno yaliyoandikwa kwa chaki na wanafunzi, ‘Speak Kiswahili only’
Mwalimu wa somo la Kemia alipoingia darasani, alianza kufundisha kwa Kiingereza kwa mbwembwe nyingi. Wanafunzi walitulia tuli wakimkodolea macho. Baada ya dakika 10 alibadili lugha, akaanza kufundisha kwa Kiswahili hapa na pale akiingiza istilahi za Kiingereza. Darasa lilichangamka, maswali yaliulizwa na kujibiwa, ikawa hivyo mpaka mwisho.Baada ya kipindi, mwanafunzi mmoja alimtanabahishia kuwa, wao huelewa zaidi wanapofundishwa kwa Kiswahili kuliko Kiingereza kwa kuwa hawana msingi mzuri katika lugha hiyo.
Lengo la makala haya, ni kuangalia ‘vita’ dhidi ya Kiswahili katika muktadha wa kitaaluma, wanafunzi wanaposisitizwa kutumia Kiingereza. Mtazamo wetu ni kwamba, pamoja na kusisitiza wanafunzi kutumia Kiingereza, heshima ya Kiswahili ilindwe.
Kaulimbiu za kukibeza Kiswahili hazina tija. Nafasi ya Kiswahili ipo palepale na itabaki hivyo siku zote: ndiyo lugha ya Taifa letu, lugha rasmi na ndicho chombo kitumikacho kuubeba na kuutangaza utamaduni wetu.
Kwa kuwa Kiingereza ndiyo lugha ya kufundishia katika shule tajwa, msisitizo uwekwe kiutendaji zaidi ili wanafunzi wajengewe msingi imara, wakielewe na kiwawezeshe kuyaelewa masomo yao.
Kisibaki tu katika mabango yanayokipa hadhi na kukibeza Kiswahili, huku wanafunzi wenyewe wakibebeshwa mzigo mzito kimawasiliano na kitaaluma kwa kulazimishwa kukitumia huku wakiwa wanapata shida kuyaelewa masomo yao.
|