MATUMIZI YA NAFSI KATIKA USHAIRI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: MATUMIZI YA NAFSI KATIKA USHAIRI (/showthread.php?tid=1468) |
MATUMIZI YA NAFSI KATIKA USHAIRI - MwlMaeda - 11-11-2021 Washairi wengi sana tuchanganya nafsi katika kazi zetu za ushairi katika namna ya kumvuruga msomaji. Nafsi ziko tatu, Ya kwanza, mimi na wingi wake sisi Ya pili,Wewe na wingi wake nyinyi Ya tatu, yeye na wingi wake wao. Sasa wengi wetu hujikuta tunachanganya, na matokeo yake wakati mwingine tunamvuruga msomaji. Mfano. Ndugu yenu nikilala, ati ninawachunia, Nikiamka ni ila, vurugu namfanyia, Kwangu hakuna aula, la kuweza wavutia? Mshororo wa kwanza. Neno “Yenu” na “ninawachunia” Huashiria msemaji katumia nafsi ya pili wingi kusema hisia zake. Hii humaanisha walengwa wa ujumbe wake wako na yeye sehemu moja na anaweza kuwaelekezea macho au kidole, na hao walengwa wake wanamsikia na kumuona. Mshororo wa pili. Neno “Namfanyia” Huashiria msemaji katumia nafsi ya tatu umoja kusema hisia zake. Hii humaanisha mlengwa wa ujumbe wake hayuko naye sehemu hiyo wakati akiweka wazi tuhuma zake. Kwahivyo hapa utaona ubeti mmoja jinsi matumizi ya nafsi yalivyotumika vibaya, na matokeo yake, msomaji hubaki na viulizi ambavyo si vya msingi na visivyokuwa na natija yoyote. Kwa mfano, hatujuwi kama msemaji lawama zake anazielekeza kwa mtu mmoja au kundi la watu, na hatujuwi kama mlengwa wake yuko naye sehemu moja au hayuko naye sehemu moja. Kwa maoni yangu, nadhani shairi moja kutumilia nafsi zaidi ya moja si tatizo, ila tatizo ni mchanganyiko huo wa nafsi kukosa mantiki, kama tulivyooona katika ubeti huo wa mfano. Nadhani hii ni kasoro tusiyoijuwa au twaijuwa lakini twaipuuza kwa kudhani haithiri kazi zetu. Kwa maoni yangu hii ni kasoro na yafaa kuepukwa na washairi, ingawa wapo baadhi ya washairi wanaona huu ni ufundi. Nimeona mashairi mengi, tena mengine ya watunzi wazuri kabisa yakiwa na kasoro hii. Hayo ni maoni yangu na yanaweza kuwa si sahihi, ila kama lipo la kujifunza basi na tujifunze sote. Nawaacha na shairi langu hili nililolitunga tarehe 01 Aprili 2017 Jumamosi 03:37am SHAIRI Nianze wataka radhi, Kwa huu wangu waadhi, Huenda ukawaudhi, Ingawa si yangu nia. Wako wenzetu baadhi, Wamejivisha kubadhi, Zilizo na kubwa hadhi, Kwenye hii tasnia. Wanajiita malenga, Na hawajuwi kulenga, Leo wajijuwe chenga, Si mchele nawambia. Uchao wanapotunga, Vina huviungaunga, Pasi mizani kuchunga, Tungo hutuandikia. Makosa yanakithiri, Tungo zao sio nzuri, Waambiwapo ni shari, Nzi wanakujazia. Haya yetu mashairi, Yawapo sio mazuri, Lazima tutafakari, Wapi tulipokosea. Kwa kuitazama fani, Vina na yake mizani, Tuone namna gani, Yataweza kuvutia. Aula kila fanani, Aweke kando utani, Anapokuwa ugani, Kwa kufuata sheria. Tuyachunge maudhui, Kama maziwa na tui, Kama haya hatujui, Tungo hazitatimia. Sivyo katu hatukui, Na tija hatuambui, Kabisa hatuchanui, Haya sipozingatia. Lipo la muhimu hasa, Mtiririko wa visa, Siviweke kwa makosa, Pindi ukijipangia. Na hoja za kibubusa, Mithili yake garasa, Wachana nazo kabisa, Tungo kuziandikia. Tungo ziwe za mfano, Zisilete farakano, Bali zikuze usono, Pamwe na udugu pia. Kama kingali cha mno, Ni kuchezesha maneno, Pasi na kumwaga wino, Na maguvu kutumia. Kwani hakutaki nguvu, Kuwa mtunzi angavu, Tungo nyingi huwa mbovu, Nguvu tunapotumia. Zinataka utulivu, Pamoja na uzamivu, Kusoma siwe mvivu, Sivyo hazitavutia. Ili tungo ziwe tamu, Mithili yake ya jamu, Basi inatulazimu, Kutunga kwa kutulia. Hawi mtunga nudhumu, Kuinuka alaumu, Karatasi na kalamu, Ambazo azitumia. Na pia haiwi kwake, Afure aghadhibike, Kisa kiwe tungo zake, Hadhira kumsusia. Hata watu wamcheke, Wamwite mwana mteke, Hainuwi kinywa chake, Mawi kuwarudishia. Bali atakaa chini, Tena akiwa makini, Apate kuyabaini, Ya ganda na kokwa pia. Atazama vitabuni, Kuzirejea kanuni, Ili asitunge guni, Na kuiudhi jamia. Atatunga za maana, Zenye mizani na vina, Asifike kila kona, Kwa tungo za kuvutia. Katu hawezi tukana, Watu wanao mguna, Ila atawaza sana, Wapi alipokosea. Na hata wakimgomba, Ujuzi atawaomba, Na kwao atajikomba, Yake yapate timia Yashike ninayoamba, Uende nayo sambamba, Sikio sitiye pamba, Upate kuyasikia. Mithili ya asumini, Mwenye ujuzi rasini, Mpigiye goti chini, Kama wataka nukia. Hapa sasa tamatini, Naweka kalamu tini, Nawaaga kwaherini, Kikomo changu natia. MISAMIATI Kibubusa….mtu anayekubali jambo pasina kulitafakari Usoni……….usuhuba 13 Agosti 2018 Jumatatu 21:58 Jina la Mtunzi Dotto Rangimoto Jina La Utunzi Jini Kinyonga Simu +255762845394 Morogoro. |