SHAIRI: MAFANIKIO - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: MAFANIKIO (/showthread.php?tid=1455) |
SHAIRI: MAFANIKIO - MwlMaeda - 11-11-2021 SHAIRI: Mafanikio
BETI: 11
MTUNZI: Mary Marcus
1. Nashika yangu kalamu, nilonge yalo moyoni, nikiyaandika humu, tasomeka kwa makini, hata kwa baragumu, ndugu zangu sikieni, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
2. Wewe ulie kazini, Fanya kwa ufanisi, sibebe ya mitaani, kidhani yanaakisi, Tena hayafungamani utajikosesha pasi, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
3. Uifanye kwa nidhamu, ulivuje lako jasho, na kwa akili timamu, ukumbuke kuna kesho, Usije kujihukumu ukidhani ndiyo mwisho, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
4. Wasema amejaliwa, kiona yake neema, anayafanya makubwa, wanamjua hakusoma, bidii inatakiwa, kama kupanda mlima, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
5. Na hili ninawajuza, siriye mafanikio, usipange kuibeza, nitegee lako sikio, bidii kuikimbiza, shika kwa matamanio, *Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
6. Bidii imtupi mtu, Walahi nakuapia, bidii kwa kila kitu, Rabana anajalia, Uaminifu na utu, uwe wa uhalisia, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
7. ‘tuishi kulalamika, maisha haya magumu, hatutaki kutumika, kukicha tunalaumu, Hakuna tunachoshika, moto kila sehemu, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
_8. Jipangie na malengo, ‘kikisha wayarejea, upanue wako wigo, ushauri kupokea, Sijibane kwenye kingo, kufanya kwa mazoea, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
9. Tafiti zabainisha, bidii kama mtaji, na inachangamotisha, waangalie magwiji, Bidii yawafikisha, wamshukuru mpaji, *Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
10. Jibidishe uyaone, haya mafanikio, ushirikishe wengine, kwa hayo yako mapito, Tuache zile karne, kuletewa andalio, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
11. Kama si jana ni Leo, tuitumie vizuri, tuachane na vileo, tusijesoma nambari, Sidanganyike na cheo, maisha siyo kamari, Mafanikio bidii, jibidiishe uyaone.
© Mary Marcus
Mbezi Louis,
Dar es Salaam
Email: marymarcusg@gmail.com
|