FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi kwa ujumla (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=73) +--- Thread: FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI (/showthread.php?tid=1423) |
FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI - MwlMaeda - 11-10-2021 FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI
FANI: huu ni ufundi wa kisanaa autumiao msanii katika kutoa ujumbe wake kwa hadhira iliyokusudiwa. Katika fani kumegawanyika vipengele mbalimbali kama vile wahusika, mitindo, muundo, mandhari, matumizi ya lugha, kufaulu na kutokufaulu kifani. Vipengele muhimu vinavyoangaliwa ni hivi vifuatavyo:
Mtindo; hii ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui, zinazotofautisha msanii mmoja na mwingine. Kwa mfano, katika riwaya ya “Barua Ndefu kama hii” iliyoandikwa na Mariama Ba ametumia mtindo wa kirafiki kuanzia mwanzo hadi mwisho. Kwa mfano, barua ya Ramatulayi kwa Dauda Dieng na barua kwa Aisatu.
Vilevile katika tamthilia ya “Nguzo Mama” na Penina Muhando, ametumia mitindo mbalimbali kwa lengo la kuipendezesha kazi yake na kuifanya iwe na mvuto zaidi kwa hadhira yake. Kwa mfano, ametumia mtindo wa kimonolojia (uk.3, 5, 13), vilevile ametumia mtindo wa majibizano mfano katika uk. (36, 37) Pia ametumia nyimbo (uk.2, 3).
Muundo; huu ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia mwandishi katika kupangilia kazi yake. Mwandisha katika tamthilia ya “Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe” na tamthilia ya “Nguzo Mama” zimetumia muundo wa moja kwa moja. Kwa mfano, katika “Nguzo Mama” mwandishi ameanza kuonesha jitihada za akina mama katika kusimamisha nguzo mama na anaonesha udhaifu uliojitokeza na jinsi walivyoshindwa kuisimamisha nguzo. Yote hii ilitokana na kukosa umoja, ushirikiano na kutothaminiana. Tamthilia hii imegawanywa katika sehemu nne ambazo zimeoneshwa kama onesho la kwanza hadi la nne.
Vilevile Mariama Ba katika riwaya ya “Barua Ndefu kama hii” ametumia muundo rejeshi kwani amechanganya matukio lakini yenye mtiririko mzuri. Alianza na kifo cha Modu halafu akaelezea jinsi Modu na Ramatulayi walivyokutana na kupendana na hatimaye kuoana.
Pia muundo waweza kufasiliwa kama mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi, kwa upande wa visa na mtukio. Katika riwaya ya “Pesa zako zinanuka” mwandishi ametumia muundo changamano. Hii ni kwa sababu ndani ya muundo huu kuna masimulizi ya moja kwa moja na kuna urejeshi ndani yake.
Wahusika; hawa ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi ya fasihi mwandishi huwagawa wahusika katika makundi mawili yaani wahusika wakuu na wahusika wadogo.
Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa kazi ya fasihi. Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza sehemu mbalimbali katika kazi ya fasihi kwa mfano, mwanzoni mwa kitabu hadi mwishoni mwa kitabu.
Mandhari; hii ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza kuwa halisi au ya kufikirika.
Maudhui; Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe na msimamo.
Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Senkoro anataadharisha maana hii isichanganywe na maudhui kwani dhamira ni sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo. Kwa mfano, katika riwaya ya “Pesa zako zinanuka” na Ben Mtobwa dhamira kuu ni uhujumu uchumi, magendo, ulanguzi na rushwa ambapo mwandishi ameonesha kuwa hiki ni kikwazo kikubwa kinachochangia kutokuwa na maendeleo katika jamii.
Zipo pia dhamira ndogondogo kama vile mapenzi, nafasi ya mwanamke, uteteaji wa haki za binadamu, matabaka, nafasi ya mwanamume katika jamii na dhamira hizi ndogondogo zimebebwa na ile dhamira kuu.
Migogoro; ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali.
Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
Riwaya ya “Pesa Zako Zinanuka” na Ben Mtubwa imeonesha migogoro mbalimbali iliyojitokeza. Kwa mfano, kuna mgogoro wa kijamii, huu unajitokeza baina ya watu au kikundi cha watu katika jamii. Katika riwaya hii mgogoro huu unajitokeza kati ya Kandili na Dora. Suluhisho la mgogoro ni kuwa Dora aliamua kuishi yeye peke yake na mtoto wake wakipambana na maisha ya kila siku.
Pia kuna mgogoro wa nafsi, huu unajitokeza kati ya mtu na nafsi yake. Katika riwaya ya “Pesa Zako Zinanuka” mgogoro huu unajitokeza kwa Dora na nafsi yake katika uk.81.
Kwa ujumla suluhisho la migogoro yote ni jamii kuwa na haki na usawa kuondoa chuki, kuondokana na uvivu, kushirikiana katika kuwafichua wale wanaotumia mali ya umma kwa kujinufaisha wenyewe.
Ujumbe; mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi.
Msimamo; katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Kwa mfano, katika tamthilia ya “Pesa zako zinanuka” mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani amejadili matatizo yanayochangia kukwama kwa ujenzi wa jamii mpya.
Pia anaonesha njia au suluhisho la matatizo hayo. Matatizo hayo ni kama vile: uhujumu uchumi, wivu, magendo, usaliti na mmomonyoko wa maadili.
UHUSIANO WA FANI NA MAUDHUI
Fani na maudhui ni dhana mbili ambazo hazitenganiki. Kuna mitazamo miwili ambayo inajaribu kutazama uhusiano wa fani na maudhui katika kazi za fasihi andishi. Mitazamo hiyo ni ya kidhanifu na kiyakinifu.
Katika mtazamo wa kidhanifu wapo wataalam mbalimbali ambao wametoa maelezo yao kuhusu uhusiano wa fani na maudhui katika kazi za fasihi andishi.
Tukianza na Bi. Materu, yeye anasema fani na maudhui ni kama mwili na nguo hivyo anatoa maoni kuwa fani na maudhui ni dhana ambazo zinaweza kutenganishwa kama vile mwili unavyoweza kutenganishwa na nguo. Bi. Materu anasema maudhui ni mwili ambao ndilo umbo la ndani la kazi ya fasihi, wakati nguo ndio fani ambayo ni umbo la nje la kazi ya fasihi.
Fauka ya hayo Mtaalam mwingine ni Penina Muhando (Mlama), anasema kuwa fani na maudhui ni kama sahani na chakula. Sahani yaweza kutengwa na chakula pale ambapo chakula hicho kitaondolewa. Penina Muhando anasema, chakula ndio maudhui yaani umbo la ndani la kazi ya fasihi na sahani ndio fani ambayo ni umbo la nje la kazi ya fasihi. Hivyo yeye anaona kuwa fani na maudhui ni dhana mbili ambazo zinaweza kutenganishwa na bila athari yoyote.
Naye T. Sengho anasema kuwa fani na maudhui ni kama chungwa na ganda, akiwa na maana kuwa chungwa ndio maudhui na ganda ndio fani. Hapa T. Sengho anatoa msimamo kuwa fani na maudhui vinaweza kutenganishwa bila ya athari, kwani chungwa linaweza kutengwa na ganda lake.
Mtaalam mwingine anayeegemea mtazamo wa kidhanifu anasema kuwa fani na maudhui ni kama kikombe na chai. Huyu ni Mtaalam F. Nkwera ambaye anasema kuwa chai ndio maudhui na fani ndio kikombe. Hapa F. Nkwera anataadharisha kuwa chai inaweza kunywewa kwenye kikombe na kikombe kubakia kitupu, hivyo fani yaweza kutengwa na maudhui kama vile chai inavyoweza kutengwa na kikombe.
Katika mtazamo wa kiyakinifu, Senkoro anasema kuwa fani na maudhui ni sawa na sarafu. Hapa anamaanisha kuwa fani na maudhui ni dhana mbili zisizoweza kutenganishwa kama vile pande mbili za sarafu moja.
Senkoro F. E. M. K. anasisitiza kuwa fani na maudhui havitenganishiki bali hutegemeana ili kazi ya fasihi iweze kuwa bora zaidi. Kazi ya fasihi ambayo maudhui yamezidi fani huwa chapwa au fani ikizidi maudhui, kazi hiyo ya fasihi huwa chapwa, hivyo maudhui na fani ni dhana ambazo hutemeana. Fani na maudhui lazima vilingane na kushabihiana ili kazi yenyewe iweze kuwa bora na yenye mvuto zaidi.
Mtazamo mwingine unadai kuwa fani na maudhui hulinganishwa na roho na mwili ambapo haiwezi kutenganishwa na mwili kwani kwa kufanya hivyo athari itakayotokea ni kwamba mwili hautaweza kufanyakazi ipasavyo pasipo roho.
Vilevile tunaweza kufananisha fani na maudhui kama gari na injini. Hii ni dhana ambayo inajidhihirisha kuwa gari haliwezi kutenda bila injini, hivyo ni kuweza kuthibitisha kuwa fani na maudhui ni dhana mbili zisizotenganishwa kwani huleta athari zinapotenganishwa na vilevile fani na maudhui hutenda kazi pamoja.
|