SHAIRI: MCHUMBA HANA TALAKA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: MCHUMBA HANA TALAKA (/showthread.php?tid=1414) |
SHAIRI: MCHUMBA HANA TALAKA - MwlMaeda - 11-04-2021 *MCHUMBA HANA TALAKA* 1.Ya Karimu Ya Jalia, nakuomba Ya Rabuka, Hekima kunijalia, kalamu ninaposhika, Niweze kusimulia, gazeti kuyaweka, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 2.Ukishindwa unakacha, Mchumba hana Talaka, Uchumba kama Pakacha, rahisi chini kuweka, Ni rahisi kumuacha, bila kwa Kadhi kufika, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 3.Uchumba si kama ndoa, kuachwa si kuachika Unapoingia doa, ndiyo mwisho umefika, Atabaki kukodoa, maji yameshamwagika, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 4.Ndoa niseme jamani, ni ahadi imeshika, Waraka utasaini, ni Mkataba hakika, Ukileta kisirani, sheria zinakushika, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 5.Uwe ‘mepeleka posa, nyumbani kwao kufika, Ya nguo pamwe na pesa, na vyote walivyotaka, Kamwe halijawa kosa, uchumba ukifutika, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 6.Mchumba wamtazama, usije kukurupuka, Je atamjali Mama, nyumbani akishafika?, Au taleta zahama, watu kuparaganyika?, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 7.Walii hutamuona, mkono wako kushika, Kukuozesha kimwana, kwa maneno kutamka, Mshenga ndo utaona, barua ameishika, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 8.Mchumba ni kama koti, kirahisi linavuka, Hata palipo kikoti, waweza kulipachika, Ubanakia na shati, hakuna wa kukucheka, ,Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 9.Uchumba kiti cha basi, popote waweze shuka, Wamwambia mie basi, kwa meseji kuandika, Nikutoe wasiwasi, korti hamtafika, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 10.Uchumba kama Bokingi, nyingine tunazoweka, Ukiviona vigingi, visoweza kukwepeka, Hakuna maneno mengi, uchumba unafutika, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* 11.Kalamu naweka chini, nimesema nilotaka, Nashukuru Manani, *WIGO* hapa nimefika, Angalia kwa makini, usije kukasirika, *Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.* Kailima Ramadhani [WIGO – I.C.B.M] Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mtumba – Mji wa Serikali *DODOMA* |