MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 3 - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Watunzi wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=17) +--- Thread: MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 3 (/showthread.php?tid=1406) |
MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 3 - MwlMaeda - 10-29-2021 Baada ya miaka mitano ya ujane, Shaaban Robert akaoa mke wa pili. Ebu kwanza tujikumbushe ni nini aliyoyataja
kuhusu watu kama wajane au watawa katika Wasifu wa Siti Binti Saad. Aliwapinga kwa kusema kuwa kukaa na kutoolewa kwa ajili ya fahari ya kutoolewa tu, ni bure. Hakuna maana. Kwa hivyo yeye akaoa ‘msiba ni tokeo kwa watu wote. Maisha ya ujane yalijaa tuhuma. Heshima yake ilikuwa ndogo lakini aibu yake ilikuwa kubwa.’ Kifo kilivunja mkataba wa ndoa na akawa hutu kuoa; akaoa ‘msichana aliyekuwa na nasaba njema na aliyepata malezi mema vile vile’ Katika kuoa kila mara, Shaaban
alifuata mambo mawili. Kwanza alifuata uzuri wa mwili na wa tabia. Pili, ndoa zake hakuziharakisha-alichukua muda wa kutayarisha jambo hilo. Yule wa kwanza alichukua miaka kumi, na huyu wa pili miaka miwili. Alikuwa akimfariji ‘kama mama na dada akaziba pengo la ujane kama mke halisi.’ Inaelekea wazo la kuoa zaidi ya mara moja halikuwa la asili yake. Shaaban anaandika kuwa, ‘Wasutaji wakinidhihaki kuwa nilikuwa mume wa wake wengi na tabia mbaya wakumbushwa kuwa nilikuwa sina ahadi wala mkataba na msutaji hata mmoja kuwa sitaoa tena hali ya mambo ikilazimisha jambo hilo.’ Mauti ndiyo yaliyotangua ahadi yake. ‘Isitoshe; mke wangu wa kwanza aliishi na mimi kwa wakati fulani mbali, na wa pili alikuwa na wakati wake mbali vile vile. Hawakukusanywa pamoja katika wakati mmoja wala katika nyumba moja kama mapacha mimbani au wanyama zizini. Ningalipenda niweze kuishi na mke mmoja tu lakini bahati haikuniamuru nifanye hivyo.’ Hivi ndivyo alivyowaza na kufanya kuhusu ndoa. Je, kazini nako? Kwanza inataka
tufahamu kwamba marehemu hakukaa bure bila kazi. Yale aliyowausia wanawe ndiyo aliyoyatenda. Kwa hivyo alikuwa ni mfanya kazi. Hakuna tusomapo kwamba alikuwa na mali aliyopenda wanawe warithi kwani alikuwa ni mtu hivi hivi; si tajiri wa mali. Utajiri wake ulikuwa ni akili zake na nguvu za mwili wake pamoja na mipango yake. Elimu humwezesha mtu kupata kazi ya aina fulani tu, lakini pengine elimu pekee siyo aifanyiayo kazi mtu. Mbali na elimu, juhudi na kupenda kazi ndio mchanganyiko wa rutuba ya mbolea na maji kazini. Matokeo yake huwa ni matunda mema ya maendeleo kazini. Hii ni siri kubwa ya kazini. Ndiyo yaliyomo katika kiini cha kazi. Elimu ni mlango tu wa kuingilia kazi fulani. Katika Wasifu wa Siti Binti Saad, Shaaban anatoa mawazo yake kuhusu kazi, na
anasema kwamba kazi lazima ipendwe, ifanywe kwa bidii, isibadilishwebadilishwe. Kwa kufanya hivyo Siti binti Saad aliendelea vyema na kazi yake ya kuimba. Na hata naye Shaaban hakupenda kubadilisha kazi na, mwaka alipohamishwa kwenda idara nyingine, anasema kuwa sikuzote angependa kuwa katika idara moja. Shaaban aliingia kazi ya ukarani
forodhani ambayo aliifanya mpaka ikafikia miaka kumi bila kubadili! Kazi hiyo, siku za 1926, kianzio chake kilikuwa shilingi sitini kwa mwezi, lakini aliishikilia tu! Je, hii inaonesha uvumilivu au shida ya ukosefu wa kazi nyingine? Ni wazi jambo hili linaonesha ule moyo wa ujamaa aliokuwa nao marehemu. Kwa miaka kumi hiyo nyongeza yake ilikuwa shilingi sitini tu! ‘Lakini, anasema, ‘kila ongezo la mshahara lilizidisha uzito wa shughuli kulemea juu ya mabega yangu.’ Kama wewe msomaji ni mmojawapo wa waliofanya kazi za afisi miaka hiyo, jaribu kufikiri tena jinsi zilivyokuwa kazi nyingi, na linganisha na pato lake. Au, kama wewe ni mfanyakazi wa siku hizi, hebu angalia jinsi kazi zilivyokatwakatwa ili kuwepo wafanyakazi wengi wa kazi moja na jinsi ambavyo mshahara wa kazi hiyo haukukatwakatwa kugawanyiwa hao wanaoifanya, bali kumewekwa mishahara mbalimbali, kila mtu na wake, tena si shilingi sitini kwa mwezi! Wale ambao hawajawa wafanyakazi nawajaribu kulinganisha mshahara huo na yale matumaini yao tu. Siku hizo za marehemu kulikuwa na
ubaguzi baina ya wenyeji na wageni katika kazi. Kwa wenyeji wenzake alikuwa mfano wa kuiga. Lakini kwa wageni kazi yake nzuri ilionewa wivu, jambo ambalo anasema aliliogopa kama alivyoiogopa tauni, na akajaribu kulikimbia kama ikimbiwavyo njaa. Je, jambo hilo la wivu afisini alilifanyia nini? Hakuacha juhudi mpaka uadui ukaupisha urafiki. Mojawapo ya kazi zake ilikuwa ni
upokeaji fedha na utoaji stakabadhi-kazi yenye mtego na hatari ya kutamani kuiba, hasa kama karani huyo kima chake cha mshahara ki mbali na fedha azionazo na kuzishikanisha kila siku. Lakini Shaaban alikuwa imara. Anasema, ‘Kosa ni uanadamu.’ Siku moja, kulitokea kasoro katika kazi yake hiyo: tafauti ya upungufu wa shilingi sita! Lakini hakuwa ameziiba. Alikuwa ameziweka mahali pasipo pake tu, na kisha akasahau. Katika kazi yake ya pili alikuwa mkubwa wa watu wa kabila, dini na madhehebu mbalimbali. Hawa, anasema, alipatana na kupeana msaada nao kama walikuwa “Mti-pane” usiovunjika. Shaaban ana mengi ya kutuachia
kama kielelezo. Jinsi alivyopanda cheo ndivyo jinsi alivyoyapanua mawanda ya jina lake katika Idara, na alijishughulisha pia kuyaswagia moyoni majina ya wale alioshirikiana nao katika kazi yake. Kuwa hodari wa kazi, kuwa na uwezo wa kuchukuana vyema na wafanyakazi wote wa chini na wa juu ndio mfano aliotuachia marehemu, tuwe nao kazini. Wafanyakazi hutazamia mabadiliko
mara kwa mara. Mabadiliko ya kazi bora ni kuongezwa mshahara na cheo, na wakati mwingine uhamisho pia. Baada ya miaka kumi na minane forodhani Pangani Shaaban aliyapata yote hayo mabadiliko matatu. Alipandishwa cheo cha pili katika makarani, akapata na uhamisho wa Idara-akenda kwenye Idara ya Utunzaji wa Wanyama huko Mpwapwa ambako alikaa kwa miaka miwili. Hapa sitahakiki kazi yake huko
Mpwapwa maadamu ilikuwa nzuri kama kawaida yake. Badala yake, nimechagua kutoa maoni yangu kuhusu taabu na matukio yaliyimpata kuhusu uhamisho huo. Ingawa alisita, kama wafanyakazi wengi wafanyavyo, baadaye alitambua kuwa uhamisho huwa una sababu iliyo nzuri. Kwa kuwa alikuwa anapelekwa mahali papya kwa kazi mpya anasema, ‘Nilijiona kama mtu aliyepewa shoka na mundu kufyeka njia mpya katika pori kubwa.’ Aliukubali uhamisho huo kwa kutii amri ya wale waliomtunukia cheo: ‘Nilipewa amri sio uchaguzi.’ Kwa hivyo, hata kama ilikuwa ‘mkuku ng’ombe’, ilimbidi ahame. Na bila shaka kuondoka ilikuwa ni lazima. Ndege mwenye kutua tawini lazima aruke. Huu ndio moyo ambao marehemu angelifurahi wafanyakazi wote kuwa nao. Pia hakukosa shukrani. Alishukuru
kwa kupandishwa cheo bila ya kukiomba. Msomaji akumbuke kuwa mfanyakazi huwezi kuwa na sifa bora kazini na papo wakuu wake wasimtambue kwa kumpandisha cheo. Kupandishwa cheo si tukio la binafsi tu bali ni pamoja na cheche nzuri ziwafikiazo wakuu wa kazi. Kabla hajenda Mpwapwa, Shaaban alirudi kwao Tanga kupumzika kwa siku ishirini, na huko alishughulika na kuwarithisha warithi wa mali (mashamba ya minazi) za marehemu mkwe wake na warithi wa mali za mke wake. Ingawa kulikuwa na mzozano fulani, kama ilivyo desturi katika mambo ya urithi, Shaaban aliyatuliza yote. Baada ya mapumziko yake safari ya
uhamisho ikaanza; Shaaban akiwa abiria cheo cha pili kutoka Tanga hadi Mpwapwa kupitia Korogwe, Morogoro na Gulwe. ‘Kumbe safari kweli taabu’ ni usemi wa kweli, kama alivyoimba mwimbaji fulani. Lakini safari ya Shaaban ilikuwa ni taabu zaidi kwa vile alikuwa Mwafrika ingawa alikuwa na cheo cha pili. Korogwe ilitokea shida, aliposhuka kungoja safari ya lori. Anasema, ‘Karibu ningalilala nje Korogwe kwa ukosefu wa malazi ya abiria Waafrika.’ Lakini mtu mmoja, bila shaka ni Mwafrika mwenzake, alimchukua kwake kumpa malazi mema. Jambo la kusikitisha zaidi
lilifanyika keshoye Asubuhi alipolazimishwa na Mhindi, msimamizi wa safari, ashuke kutoka lori la abiria wa cheo cha pili apande lile la cheo cha tatu au la mizigo kuwapisha nafasi Wahindi wane waliochelewa kuja. Yeye na watoto wake tu ndio waliokuwa abiria Waafrika katika lori hilo la cheo cha pili, tena walikwisha wahi kukaa mapema. Lakini mhindi yule hakuona mtu mwingine wa kumshusha ila Shaaban na watoto wake. ‘Baridi ina mzizimo siku zote kwa kondoo mwenye manyoya haba’, ndivyo Shaaban alivyoandika. Baada ya kumjibu maneno ya haki, kwamba yeye naye alikuwa ni abiria wa cheo cha pili na mfanyakazi Serikalini, aliendelea kukaa; na, kwa vile hakuwa na haki ya kutereshwa, Mhindi aliwaamuru matarishi wamakamate na kumtupa chini kama mtumba. Mungu awaweke matarishi hao; hawakutii amri! Lakini, kwa kuwa Shaaban hakupenda kuchelewa bure Korogwe, aliita watu waje kushuhudia atendewavyo. Wengi wakampa sahihi za mikono yao na, ingawa yule Mhindi alikataa kuandika stakabadhi ya kuonesha namna Shaaban alivyosafiri kutoka Korogwe, Shaaban aliwapisha wale Wahindi wane naye akapanda juu ya gari la mizigo. Lakini hatupati tena habari hii. Kisa cha tatu ni kile cha
Mpwapwa, Kikombo. Kwa kuwa walifika saa kumi za usiku, aliambiwa akae juu ya gari hadi saa moja Asubuhi ‘wakati mwendeshaji wetu alipoingia nyumbani mwake kulala.’ Mpwapwa ni pahali penye baridi kali sana hasa, huo mwezi wa Julai alipofika Shaaban. Mimi ni mzaliwa na mkulia wa huko; kwa hivyo nafahamu. Lakini licha ya kumwacha kupigwa na baridi, kumwacha nje mtu mgeni kaka yeye, tena mahali kama hapo, si uungwana. Na pia, kulikuwa na shida ya nyumba. Hata hivyo, jambo kuu la Shaaban ni kwamba hakuziacha shida hivi hivi tu bila ya kutafuta sababu zake. Na, ingawa alikuwa mfanyakazi wa ‘cheo cha juu, hakupigapiga kelele. Alivumilia. Katika mwaka huo huo Shaaban
akahamishwa kurudi tena Tanga. Safari hii uhamisho wake ulisababishwa na ombi lake mwenyewe la kutaka kumwezesha bintiye aendelee na masomo ya juu huko Tanga. Na hakuomba kwenda Tanga tu, bali kokote kwingine ambako bintiye angeweza kusoma. Kisomo cha bintiye ni mwangwi wa mawazo yaliyomo katika tenzi zake za usia. Shaaban anaona kuwa ni sharti watoto wapelekwe skuli; wote-wavulana kwa wasichana. Anasema, ‘Wakati tulionao sisi sasa, kosa la kumwelimisha mtoto haliwezi kusameheka hata kidogo pasipo mapatilizo. Mtoto yeyote anyimwaye makusudi nafasi ya kujifunza matumizi yak soma, kuandika na hesabu ana haki ya kuwalaumu wazazi wake katika maisha yake atakapojiona kuwa amefungiwa milango yote ya kusitawi baadaye.’ Haya, sikieni wazazi! ‘Bahati ilinifanya mshairi tangu
1932.’ Hivi aanzavyo kusema juu ya ushairi wake. Mbali na kazi yake maalumu, Shaaban alikuwa mshairi mashuhuri. Mashairi yake bado yanasomwa sana shuleni, vyuoni na hata majumbani kwa sababu yanafunza na kutia moyo katika kupambana na maisha ya dunia hii. Watu wengi husahau kwamba wanaweza kufanya mambo zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kama vile Shaaban alivyokuwa mfanyakazi na mshairi pia. Leo tuna mfano mzuri wa Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius K. Nyerere. Yeye ana kazi kemkem za Uraisi na uongozi wan china, pamoja na hayo, anatoa mawazo yake vitabuni. Mpaka sasa hivi ameandika vitabu vimgi sana ambavyo ni msingi wa maendeleo ya nchi yetu. Hali kadhalika Shaaban naye, katika enzi zake alijishughulisha na maandiko au fasihi. Ameandika mawazo yake kwa njia za hadithi na mashairi. Kama Mheshimiwa Waziri wa Elimu wa mwaka 1966, Bwana Solomon N. Eliufoo, alivyosema katika dibaji ya kitabu hiki hiki tukizungumzacho, ‘Alikuwa mshairi maarufu…..na kila aliyewahi kusoma tungo zake…hakukosa kupata fundisho fulani…Mbinu ya kalamu yake mpaka dakika ya kufa kwake ilikuwa ya hekima tupu (au kwa kileo tusemavyo ya Folosofia).’ Huo ni mfano kwa wale wenye mawazo mazuri ya kuendelezea nchi na wenye kipawa cha kuandika, waandike ili mawazo yao yasomwe na wana wao na wa wenzi wao na vizazi hata vizazi. Yeyote anayeipenda nchi yake
haitumikii tu bali huwa kama kipima-joto cha mahospitali. Huweza kuona hali ya nchi ilivyo, akafanya kila bidii ili kuleta maendeleo. Kufanya hivyo kunategemea wakati na mazingira yenyewe. Shaaban anaonesha kuwa aliipenda sana nchi yake Tanganyika. Kwanza aliitumikia bila manung’uniko na kwa bidii zake zote, kisha akaipigania kuikomboa iwe huru. Lakini vipi? Alikuwa na ari ya siasa. Anasema, ‘Alivyokuwa kila mtu ndivyo nilivyokuwa mimi vile vile. Nilitekwa na uzalendo….Sikupenda kuwa mgeni katika nchi ya asili na uzazi wangu. Sikutaka kuwa mtazamaji wakati wananchi wengine walipokuwa wachezaji, nikajiunga na chama….cha siasa cha Waafrika kilichoundwa…1929.’ Hiki ndicho chama kilichokuwa asili ya TANU ambacho kilizaliwa 1954 kikawa na wanachama wengi zaidi na kupigania uhuru na utawala chini ya uongozi wa Julius Nyerere. Serikali haikupenda wafanyakazi
wake wawe wafuasi wa chama cha 1929, kama ambavyo vile vile haikupenda wawe wafuasi wa kile cha 1954. Kwa hivyo ilijitahidi kila mara kuwawekea vipingamizi na hatimaye ikawazuia kabisa kuwa wanachama. Mawazo yake Shaaban juu ya Rais wa chama na wakuu wenzake ambao kazi zao zilikuwa ni za kujitolea yalikuwa ni kuwaonea huruma na kuwatia moyo kupigana vita hivyo. Huku kazi, huku siasa, na huku
uandishi. Yote haya aliyafanya Sheikh Shaaban. Katika fasihi yake Shaaban alichukua wazo juu ya ujane kwa kufikiria ubora na ubaya wake kwa nchi yake yenye eneo la maili mraba 365,000 iliyokuwa na jumla ya watu chini ya milioni 10. Ushairi ndio sanaa aliyoitumia kutolea mawazo yake juu ya ujane, akasema, ‘Ujane una matata si jambo la kutumia.’ Mara dhoruba ya ukinzani ikaanza, huyu akisema hivi na yule hivi hata magazeti mazuri yakachafuka. Lakini, hata hivyo, alipata watetezi wengi walioandika kutetea ujane, nay eye mwenyewe binafsi alipenda nchi ijae watu-lakini sharti watu hao wawe wamezaliwa kwa ndoa ya halali. Ndipo aliposema: ‘Mume ni
mume, ingawa gumegume, ana sifa ya Mtume; Na mke ni
mke, ingawa kikwekwe, ana manufaa yake.’ Katika mwaka 1959 ikambidi kuacha
kazi. Akawa amefanya kazi miaka 33, na umri wake miaka 57. Kwa kazi zote alizozifanya, pamoja na dhiki za mahamisho mengi, cheo chake hakikupanda zaidi ya ukarani! Mtu kama yeye, kama ingekuwa anaacha kazi leo, angepewa zawadi nyingi-kiinua mgongo. Angefanyiwa karamu na kuletewa kalamu mbalimbali za shukrani kwa kazi alizofanya, na pia kumtakia heri kwa siku zake za usoni. Lakini haya Shaaban hakuwa na bahati nayo. Mzungu mmoja tu ndiye aliyempelekea zawadi. Hata hivyo Shaaban hakunung’unika. Kwake yeye ushairi na kalamu ya kuandika ndivyo vitu vilivyokuwa bora zaidi! Anasema, ‘Mbinu hufuata mwendo. Mwendo niliopenda kabisa maishani ulikuwa huu.’ Kisha baada ya kustaafu, Shaaban alimshukuru Mwenyezi Mungu aliyemlinda na kumwendeleza kazini, na kuwa naye siku zote katika miaka yote ile 33 ya usumbufu. Jambo moja zaidi, ambalo hakuna
aliyelitazamia, lilitokea. Alidaiwa kurudisha gharama ya usafiri iliyotolewa idhini na Mudir wa Idara alipostaafu. Sababu? Waliokuwa wakipata usafiri wa bure ni wale waliokuwa wakirudi kazini au makwao nje ya Tanganyika! Yeye Mwafrika Mtanganyika safari ya kurudi nyumbani kwao ilionekana kama ambaye anakwenda ‘Uingereza au Bara Hindi.’ Shaaban Robert hakuwa mzalendo
mwenye kuipenda, kuitumikia, na kuipigania Tanganyika tu, bali pia alikuwa na ule moyo wa kutaka kuwaona binadamu wote ni sawa. Kwa hivyo, mawazo yake yalivuka mpaka wa shida za Tanganyika, akalifikiria bara zima la Afrika. Jicho lake la mawazo likatua huko Afrika Kusini ambako Kaburu hadi leo bado anawanyonya na kuwabagua watu weusi ambao ndio wananchi halisi. Shaaban hakuvumilia ukatili uliotendeka huko na uliutia moyo wake machungu. Maoni yake kuhusu usawa wa binadamu wote ni hivi: ‘Wajibu wa watu katika maisha ni kuwiana hisani, usawa, adabu, heshima na mapenzi…Katika Afrika Kusini wajibu huu ulimezwa na ubaguzi wa kutisha. Watu waliusiana chuki, kiasi na makanio. Pumzi ya kila mmoja ilijaa hofu, kutoridhika na manung’uniko, sumu juu ya sumu. Shaaban alifurahi kuona Serikali
ya Tanganyika huru ikivunja uhusiano wa Kibiashara na Afrika Kusini ‘mpaka tabia yake itakapokuwa imebadilika kuwa njema na ya amani kwa watu wa rangi zote.’ Na ndivyo Serikali yetu ilivyofanya hadi leo hii. Biashara nyingi ziliathirika kwa msuso huo. Hata yeye Shaaban, baadhi ya kazi zake za sanaa ya ufasihi-zilizokuwa zinapigwa chapa na Chuo Kikuu cha Witwatersrand, kama Kielezo cha Insha ambacho sasa kinachapwa na Oxford University Press-ziliathirika. Mawazo yake juu ya athari hiyo ni haya: ‘Walakini, ikiwa change ndogo kama ilivyokuwa yangu mimi ya sadaka, ilisaidia kupatikana kwa ufanifu wa uhuru na amani kwa watu katika Afrika Kusini, hasara hii ilikuwa si kubwa ilinganishwapo na furaha ya ushindi uliotazamiwa kuja kwa watu mwisho; ushindi uliokuwa si wa mweupe, mwekundu wala mweusi, lakini uliokuwa wa wote; na fahari ya kila taifa katika dunia.’ Yeye alikuwa na nia moja tu: kukomboa utukufu wa mwanadamu, hata kama ilikuwa kwa kujitoa mhanga. Kazi za uandishi za Shaaban ni
nyingi, nazo zilipata neema kwa vile baadaye vitabu vyake vilipata kupigwa chapa hapa hapa Tanzania. Pia huko Kenya kazi zake nyingi zilipigwa chapa, na Julai 1960 duka lake likafunguliwa. Alipoona wengi hawanunui vitabu vyake aliwapa bure. Wakamshukuru, naye akafurahi kwa mara nyingine tena kwa change ya namna hii. Kutoa misaada kwa namna hii ni tendo la kiujamaa. Hivyo ndivyo alivyojaribu kuitenga nafsi yake kando ili awatumikie watu. Kama alivyomuusia mwanawe, mwenye msaada ampe asiye nao. Shaaban alitoa alichokuwa nacho. Hivi nivyo alivyoishi mtu aliyetoa mawazo yake
katika Wasifu wa Siti binti Saad na Adili na Nduguze na mahali pengi pengine. Je alitimiza lengo lake la kuwa na ‘jina’ ulimwenguni? Msomaji utaweza kulijibu swali hilo wewe mwenyewe. Mimi naona maisha yake ni kielelezo kikubwa, na yalikuwa ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu. Katika kuhakiki vitabu viwili vya
kwanza nilisema lengo kuu la Shaaban kuandika ni kutaka watu waishi kwa kupendana. Huu ndio msingi wa kuishi kwa Kujitegemea na kuishi kwa ujamaa. Tumemwona alivyoishi na wakeze, wanawe, wafanyakazi wenziwe, wananchi wa Tanganyika, na hata jinsi alivyotandaza mawazo yake kwa wanaadamu wote. Matendo yake yatakamilisha mawazo yake. Maisha ya Shaaban Robert, kama
yalivyoandikwa katika Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, yameandikwa na Shaaban mwenyewe. Wengine wanaweza kusema kwamba hakujiweka kwenye mizani na kujiandika bila kujipendelea. Mimi naona amejiandika bila kujipa jambo lolote lisilo lake, wala hakujirefushia jambo lolote ambalo ni fupi. Amekuwa na kiasi. ‘Maisha yalikuwa matendo, siyo usingizi,’ Na sasa tumeona kwamba ingawa
maisha ya mtu yanafungamana na pengine huongozwa, na mazingira yake-binadamu wenzake, mahali alipo, na wakati wenyewe aishio-yeye mwenyewe ndiye mwenye jukumu lote kwa yale ayajazayo katika nafasi ile. Mawazo ya kujitegemea, kama ayatoavyo Shaaban katika Wasifu wa Siti Binti Saad, na mawazo ya ujamaa yaliyomo katika Adili na Nduguze na popote pale, yamo tena katika Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. |