SAA NNE MAALUM NA MWANDISHI ADAM SHAFI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Watunzi wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=17) +--- Thread: SAA NNE MAALUM NA MWANDISHI ADAM SHAFI (/showthread.php?tid=1404) |
SAA NNE MAALUM NA MWANDISHI ADAM SHAFI - MwlMaeda - 10-28-2021 Nimepokea simu. Simu ya maana. Adam Shafi yuko Majuu. Kaja kikazi Uholanzi. Yeye mtaalamu wa lugha ya Kiswahili. Baada ya kumaliza kapitia Uingereza katika mji mmoja wenye wakazi wengi wa Kitanzania, yaani Milton Keynes. Ni wastani wa saa moja kwa treni toka London. Mrefu, mchangamfu, mzungumzaji aliyesheheni “mastore” kibao. Nishakutana na waandishi wa kila sampuli. Wanaojificha: wakimya, wasioongea sana, wapole wanaokaa chumbani kati kati ya watu ukadhani hawapo. Wanaopiga kelele, wakijafaragua; ama wenye aibu…
Shafi ni mtu wa kawaida kabisa, naweza kuiita hulka, tabia na namna yake “Mfurahia Maisha” : kachangamkia uhai, haswa. Kaishi, anaishi…hamalizi. Kila mara atasema ana mikakati ya kufanya jambo fulani, kuandika kitabu kingine kipya, kuendeleza fasihi na Kiswahili….
Katika saa nne zote nlizokuwa naye ananikumbusha moja. Ikiwa umewahi kuvisoma vitabu vyake utagundua huchanganya kila kitu: furaha, simanzi, vita, amani, mapenzi, karaha, starehe, maonyo, mandhari, elimu na mengine tele. Ukiongea naye yuko hivyo hivyo. Mastore kibao. Anaelezea namna wachapishaji waliotafsiri moja ya vitabu vyake walivyotaka kumrusha fedha. Akawafungia safari hadi Paris kudai haki hiyo. Au alivyofiwa na mpenzi wake wa ujanani zamaaaani…pamoja na mtoto. Alivyotiwa jela ugenini ujanani (anamalizia kitabu kipya kuhusu kisa hiki, soma mbeleni); alivyofungwa Unguja baada ya mauaji ya Rais Karume. Hadi leo mguu wake wa kushoto ananionyesha bado una dosari (“pana ganzi pajani shauri ya kulala sakafuni”); alifungwa miaka miwili. Visa, kibao. Vyote vimepenyezwa angalau kiduchu ndani ya vitabu vyake. Vingine vishatafsiriwa lugha za kigeni. Kimoja kilishinda tuzo. Niko naye. Tunakula ubwabwa uliopikwa vizuri na binti yake kwa nyama za kukaanga…huku tukila huku tukiongea. Mazungumzo hayaishi. Ingawa masaa manne mengi kukaa na mtu (kwa huku Ulaya ambapo muda ni dhahabu) nahisi itabidi nipewe miezi ili kujua mengi zaidi ambayo nataka kuyafahamu. Anachonifurahisha ni hii picha akiwa na mjukuu wake wa miaka minne. Huyu ni mtu aliyeshaishi. Akaona mengi. Akazaa. Akalea. Aka…mcheki.
Waandishi ni watazamaji na wasikilizaji wakubwa wa jamii. Waandishi ndiyo hutukumbusha yaliyotokea. Kusingekuwepo waandishi tusingefahamu yaliyopita. Kila mmoja wetu kila siku anahangaika na maisha. Tunaamka, tunakula, tunakwenda kazini au masomoni. Tunarudi , tunalala, kesho yake hayo hayo: kila kukicha na kuchwa tunaona mengi, tunayapita, tunayasahau. Ila waandishi? Wasanii? Kazi yao kuweka kumbukumbu ya haya mambo. Kuyahadithia. Wapo waandishi wa aina nyingi. Wana habari. Waandishi wa elimu na historia. Washairi. Watunzi wa muziki na nyimbo. Sinema. Tamthiliya.Wapo waandishi wa fasihi kama Adam Shafi. Shafi alianza na kitabu cha “Kuli”, kinachoelezea mgomo maarufu wa wafanyakazi maskini , Unguja mwaka 1948. Anasema alikuwa na miaka minane tu. Na ingawa anakumbuka juu juu tukio hilo utotoni, alikuja kuhaditihiwa na mtu akaweka kumbukumbu na baadaye maandishini. (Unaona waandishi walivyo watu muhimu, kutukumbusha?)
“Kuli” kilichapishwa na Tanzania Publishing House (TPH) miaka ya Sabini. Lakini awali alichapisha “Kasr ya Mwinyi Fuad” ambacho kimeshatafsiriwa lugha tatu za kizungu: Kijerumani, Kifaransa na Kirusi.
Miaka ya karibuni, Shafi kaibuka na “Vuta Nkuvute” kilichopata Tuzo kwenye tamasha la vitabu, Dar es Salaam, mwaka 1998. Ni kisa cha mapenzi, tena mapenzi makali na mazito kati ya msichana wa Kihindi na Mwafrika. Humo mna siasa na harakati za uhuru na mengi mengine. Mseto mkubwa wa mapenzi na siasa, ambao si waandishi wengi wa KIswahili wamemudu kuuchanganya.
“Vuta Nkuvute” kilichapwa na Mkuki na Nyota. (Soma habari zao hapa : http://www.mkukinanyota.com) .
Mwaka 2003 mwanafasihi huyu alitoka na “Haini” ambacho kama anavyosema mwenyewe kiliogopwa na wachapishaji wengi nchini. “Haini” si mchezo. Kitabu cha moto, cha kuchachafya. Soma ukurasa wa kutisha wa mfungwa mmoja akipambana na chatu, ukurasa wa 172:
“Anaiangalia dunia kwa hofu na kukata tamaa, anachungulia kaburi. ..Alipomtazama yule chatu alimwona anaanza kujinyumbua, ananyeka, kichwa amekiinua,kama anayezindukana kutoka usingizini. Chakula chake amekwisha andaliwa, hana wasiwasi. Tayari kimo mle chumbani.”
Kama desturi visa vyote vya Shafi hujaa mateso, shida, majonzi, taabu za Mwafrika; lakini haviishii na hisia hizi za kukata tamaa na kutokwa machozi. Wahusika wake huteseka lakini mara wakaibuka, wakaamka na kupambana na matatizo yao. Matumaini ndiyo rangi ya suluhisho lake.
“…Moyo wa ujabali ukamjaa tele akahisi na nguvu kama za simba yuko tayari kuvaana na chatu yule kwa mikono yake miwili. Chatu naye amenyanyua kichwa anajiramba midomo. Huutoa ulimi wake halafu akaurudisha ndani na pale anapoutoa utadhani anatoa miali ya moto kutoka mdomoni. Wanatazamana. “Nani atakayeanza kushambulia?” Haramia anajuliza.”
Msomaji sin’takueleza yaliishia wapi. Maana ukijua hutatamkiwa kitabuni. Nnachokumbuka sikulala baada ya kusoma sura hii. Inatisha. “Haini” ni kitabu kinachosisimua sana. Kilinikumbusha visa vya mwandishi wa Kimarekani Stephen King, ambaye karibu vitabu vyake vyote vishafanywa sinema. Sinema yake maarufu ni ile ya kutisha sana iitwayo The Shining. Sidhani ntakosea nikisema maandishi ya Shafi hayapishani na waandishi wa aina hii hata kidogo. Vikitafsiriwa vitapendwa ulimwenguni kote. “Haini” yahusu namna Shafi alivyofungwa jela miaka miwili akiwa bado mwandishi wa habari (taaluma yake kikazi)…akifanya kazi gazeti la “Uhuru” ambalo enzi za miaka ya Sabini (alipowekwa kizuizini) visiwani liliitwa “The Nationalist.” Ubaya,walakini, mmoja. Kitabu hiki kimechapishwa Kenya na Longhorn (http://www.longhornpublishers.com). Bongo hakipatikani kirahisi bali duka moja tu mitaa ya Kinondoni.
Vitabu vyake vyote Shafi vinaonyesha maisha ya sasa na yale yaliyopita. Anapenda kuhusisha historia ya jamii. Kwa hivyo mbali na kustareheshwa unafahamishwa mambo yaliyopita ya zamani. Hali hiyo imo pia katika muswada wake mpya “Mbali na Nyumbani” ambao unaelekeza maisha ya ujanani wa mwandishi.
Namsikiliza mwanafasihi huyu aliyezaliwa Unguja mwaka 1940 akinisomea: “Mbali Na Nyumbani.” Anasema huchukua wastani wa miaka mitano kumaliza kitabu kimoja. “Huwa sina haraka hata kidogo…” Huandika kwanza kwa mkono halafu ndiyo akachapa katika tarakilishi (kompyuta)….”Mbali na Nyumbani” anafafanua, kinasimulia ujana wake kati ya mwaka 1960 na 1967 …akijaribu kuvuka Afrika kwenda Ulaya. Hapa alipo ukurasa wa 427 (cheki picha juu)anasimulia akiwa mpakani Sudan kuingia Misri. Anaposoma ananikumbusha mwaka 1978 nilipojaribu na mimi kustoawei kwa meli. Vijana enzi hizo tulitaka sana kupanda meli. Ubaharia ulikuwa kazi ya kutamanika, kutafutwa na kuotea. Miaka hiyo imepita. Leo Vijana bado wanaotea kuingia nchi zilizoendelea. Nchi za Magharibi. Maisha yalikuwa magumu enzi zile, bado magumu leo, miaka arobaini na sita baada ya Uhuru. Lakini Wazungu wamefunga mipaka. Hawataki wageni. Enzi hizo ilikuwa vile vile. Kupata “kitabu”ilikuwa kazi; leo pia iko kazi. Kupata visa ilikuwa kazi; leo pia iko kazi.
Miaka kumi na mitano iliyopita mtindo uliibuka kwa Mwafrika kujifanya mkimbizi. Hiyo ziku hizi imeshatafutiwa ufumbuzi. Wazungu washajua. Washajua mathalani kuwa Bongo hakuna vita. Yalipokuja mauaji na machafuko ya Burundi na Rwanda wengi tukaanza na sisi kujifanya wakimbizi kutoka sehemu hizo. Ujanja huo ulifaa hadi miaka michache iliyopita. Leo yamegeuka. Wahusika washagundua. Ukimbizi leo haufai tena kama sababu. Yuko jamaa kanieleza ujanja mpya. Kujifanya junya au firauni. Si mnajua tena kuwa jadi hii nchi za Kizungu inaruhusiwa? Mwanaume kuoa mwanaume au mwanamke kumwoa mwanamke mwenzako?
Mwezi jana ilipitishwa sheria Uingereza kuwa ukishtakiwa kuwa umemtania msenge au firauni unakwenda jela miaka Saba. Vituo mbalimbali vya polisi vina vitengo maalum vya kutetea maslahi ya wasenge, na vinaongozwa pia na polisi wasenge. Basi kusikia hayo walala hoi nao wamegundua mpya. Afrika tabia hii hairuhusiwi wala si mila yetu. Basi ukitoka kwenu ukisema umeteswa kwa kuwa wewe msenge, ah unakaribishwa mikono miwili. “Kwani watakucheki?” anauliza mpambe aliyenieleza. “Watakucheki vipi? Watakufungua makalio?”
Basi, ndoto na njozi za kutoka Afrika kwenda Majuu hazikuanza leo. Kitabu kipya cha Mzanzibari Shafi, kitaonyesha harakati hizo miaka ya zamani kabla wengi hatukuzaliwa. “Mbali na Nyumbani” anasema kimeshauliziwa na wachapishaji kadhaa hapa Bongo na Kenya. Pichani chini Adam Shafi akinisomea muswaada.
Lakini swali niulize. Wangapi wanamfahamu Adam Shafi? Kwa wasomaji wa vitabu vya hadithi na fasihi, jina hili ni la kusisimua na kuvutia. Kwa wapenzi wa lugha yetu tukufu ya Kiswahili huyu ni mjumbe. Walii. Tarishi. Al Watan. Mpiganiaji. Mbunge wa lugha hii. Ndugu msomaji nikupe mfano? Hebu kumbuka Wabongo wangapi wanaodai eti hawana msamiati wa kutosha kujielezea Kiswahili. Utamsikia mtu kasoma, ana shahada, ana ujuzi na utaalam wa hali ya juu akisema : “Ah siwezi kuandika barua kwa Kiswahili…” Ilhali (lakini) anaongea Kiswahili fasaha lakini kuandika anashindwa. Anatumia Kiingereza. Kiingereza chenyewe marea nyingi kibovu. Afadhali hicho Kiingereza kingekuwa kizuri. Msikilize babu na gwiji wa fasihi ya Kiswahili, Ustaadh Shaaban Robert akituasa katika Utenzi wa Adili:
“…Lugha humpa hadhi
Kutumia ajuaye.”
Kisa cha kusema haya yote nini?
Ukitaka kuboresha lugha, ( yeyote ile) soma vitabu. Soma hadithi. Soma mashairi. Kama vile ambavyo wanamuziki hujiendeleza kwa kusikiliza miziki ya aina mbalimbali, msamiati, lahaja na lugha huendelezwa kwa kusoma vitabu. Kwako msomaji unayegomba huwezi kujieleza vizuri kwa Kiswahili, au kuandika Kiswahili…katafute vitabu vyake Adam Shafi, utafaidika na kustareheka.
Watanzania tunasemwa hatusomi. Baa ziko nyingi kuliko maduka ya vitabu na maktaba. Taifa lenye watu wasiosoma linajichimbia kaburi la ujinga.
Nikiwa na Shafi, mjini Milton Keynes alipopitia juma lililopita. Picha imepigwa na Hawa Yaxley.
Hebu onja (kidogo) baadhi ya ubingwa wake wa matumizi ya lugha katika nukuu zifuatazo (hapa ni vitabu viwili tu):
“Alihisi Shihab alikuwa kama aliyemtupia mshipi akaumeza pamoja na ndoana, chambo na chubwi.” (Vuta Nkuvute).
“Aziz alitaka kuibusu midomo ya Khadija. Amemwinamia, uso umembadilika, uchu wa mwanamke umemtawala akili zake zimehama kutoka kichwa cha juu zimehamia kichwa cha chini. Alipotaka kumbusu Khadija alimtemea mate yakamtapakaa uso mzima. Alimwachia mkono mmoja ili ajipanguse yale mate, Khadija akaukamata mkono wake akaung’ata, Aziz akasikia maumivu makali yakipanda mpaka utosini.” (Haini).
“Midomo aliitafuna tafuna nakuimungunyua mungunyua kama mtafuna tambuu…” (Vuta Nkuvute).
“Tokea siku ile aliposokomekwa ndani mle, furaha kwake ilikuwa adimu na huzidi kugubikwa na majonzi pale anapowaza kwamba kosa alilolifanya ni kule kuchinja jogoo lake mwenyewe…” (Haini)
“Amle Mbiza, amle Mboza? Aliwaona kama wote wawili wamemsimamia mbele ya macho yake, achague mmoja. Huyu mmoja keshaolewa, mke wa watu, amemfungia safari kutoka Mombasa mpaka Unguja. Akimwoa kitakuwa chuo chake cha pili. Huyu mwingine bado mbichi, mwari, bikira, atakapomwoa itabidi arusi aijibishe mwenyewe. Arusi ijibu; yeye ajithibitishe urijali wake na mwenzake athibitishe ubikira wake.” (Vuta Nkuvute).
Je unataka kuwasiliana naye Shafi? Mwandikie barua pepe: ashafi40@yahoo.com
CHANZO>>>> |